Simba SC : Mpanzu alifunga usajili wetu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:59 AM Jan 17 2025
news
Picha:Mtandao
Elie Mpanzu.

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba imeweka wazi sababu za kutofanya usajili wa mchezaji mpya katika kipindi cha dirisha dogo kilichofungwa juzi zaidi ya winga, Elie Mpanzu, ni kutokana na kuwa na kikosi bora na kilichokamilika.

Kabla ya msimu huu kuanza, Simba ilisajili wachezaji 17, ikiwa ni idadi kubwa ya wachezaji kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, pia iliacha mastaa wake kadhaa kwa sababu mbalimbali ikiwamo kushuka viwango.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliliambia gazeti hili jana baada ya vikao kati ya viongozi na benchi la ufundi, hawakuona sababu ya kuongeza mchezaji mwingine, hivyo kikosi kilichopo kitaendelea kucheza mechi za Kombe la Shirikisho Afrika, Ligi Kuu na michuano ya Kombe la FA.

Ahmed alisema hayo kufuatia klabu hiyo kukaa wakati timu mbalimbali zikiwa katika pilikapilika kuimarisha vikosi vyao huku zikihakikisha zinakamilisha mchakato huo kabla ya dirisha la usajili halijafungwa.

"Ukiona watu wanasajili kipindi hiki cha dirisha dogo ambacho hakuna wachezaji bora sana walio sokoni ujue walikuwa na mapungufu, ndiyo maana wamesajili, siyo suala ya kujivunia sana hasa kipindi hiki cha dirisha dogo, inabidi tu tujivunie viongozi wetu na benchi letu la ufundi kuwa dirisha kubwa tulilitumia vizuri sana kunasa wachezaji ambao mpaka sasa wapo katika ubora wao.

Tumekariri lazima dirisha la usajili likifika lazima timu isajili, au mmetuzoea kila dirisha ni lazima tusajili kwa sababu hatukuwa na timu bora na ya ushindani kwa miaka kadhaa nyuma, ndiyo maana kila dirisha ilikuwa ni lazima kuingia sokoni kusaka wachezaji kwa ajili ya kuboresha timu yetu, nadhani mazoea ndiyo yanawatesa watu hivi sasa na kushangaa kuona mpaka sasa hatujasajili.

Hii inatokana na ubora wa timu tuliobayo hivi sasa, tuna kikosi cha wachezaji ambao wanajitosheleza kabisa, ndiyo maana viongozi wetu na benchi letu la ufundi hawakuona sababu yoyote ya kusajili mchezaji mwingine katika kipindi hiki zaidi ya Elie Mpanzu pekee," Ahmed alisema.

Hata hivyo alisema Mpanzu walimsajili muda mrefu na muda ulipofika walikamilisha taratibu za uhamisho, hivyo kwao wanaona ni kama kipindi hiki hakuna mchezaji waliyemsajili.

"Huyu tulimsajili kwa muda mrefu, sema tu dirisha kubwa lilikuwa limefungwa, ndiyo maana tumekuja kumwingiza katika dirisha hili dogo, kwa maana hiyo safari hii hatujaona umuhimu wa kufanya usajili mpya kwa sababu ya ubora wa kikosi tuliochokuwa nacho.

Tungekuwa na uhitaji tungeweza kumsajili mchezaji yoyote yule ndani na nje ya nchi, lakini tuna wachezaji wazuri sana safari hii," alitamba Ahmed.

Alisema kikosi walichonacho kwa sasa japo kina wachezaji wengi wenye umri mdogo na si wazoefu, lakini kwa muda mfupi wamewapa matokeo chanya, lakini wakiwa na faida ya kufundishika na kuendelea kukua.

"Ni kikosi kinachoweza kutupa mafanikio makubwa, pia tunaweza kukikuza kwa sababu kina wachezaji vijana wanaoweza kuendelea kufundishika, ikumbukwe pia mafanikio haya ya kuongoza ligi na kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika yasiwasahaulishe, bado tunatengeneza timu, tuko katika mchakato huo na unaonekana kwenda vizuri," aliongeza meneja huyo.

Alisema pia kikosi chao kinaendelea vyema na mazoezi kwa ajili ya mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.