TRA yaandaa bonanza la michezo wiki ya mlipakodi

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 01:30 PM Jan 17 2025
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akizungumza na baadhi ya Wafanyabiashara wa Kariakoo(hawapo pichani) kuelekea kwenye bonanza la Wiki ya Mlipakodi litakalofanyika Januari 19 mwaka huu katika viwanja vya Kidongo Cheundu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akizungumza na baadhi ya Wafanyabiashara wa Kariakoo(hawapo pichani) kuelekea kwenye bonanza la Wiki ya Mlipakodi litakalofanyika Januari 19 mwaka huu katika viwanja vya Kidongo Cheundu.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania(TRA), imeandaa bonanza litakalokutanisha wafanyabiashara wa Kariakoo na wafanyakazi wa mamlaka hiyo Jumapili ya kesho ikiwa ni kuelekea kilele cha wiki ya mlipakodi Januari 23, mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema lengo la bonanza hilo ni kujenga mahusiano mazuri baina ya pande hizo mbili.

Kwa mujibu wa Mpogolo, bonanza hilo litahusisha michezo mbalimbai ikiwamo ya kukimbia, kuvuta kamba, kukimbiza kuku na michezo mingineyo.

"Bonanza hili pia linafanyika kwa kusema asante kwa kuendelea kulipa kodi na tumepanga kuendelea kulifanya kwa ukubwa zaidi  ili pamoja na mambo mengine lisaidie kulinda afya za watu wetu,"alisema Mpogolo.

"Na bonanza hili litaanza kwa kutembea umbali wa kilomita tano katika eneo la Kariakoo na kuhitimishwa eneo la Kidongo Chekundu ambako ndiko kutakuwapo na michezo mingine."

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Severin Mushi, akizungumza na baadhi ya Wafanyabiashara(hawapo pichani) kuelekea bonanza la Wiki ya Mlipakodi litakalofanyika Januari 19 mwaka huu katika viwanja vya Kidongo Chekundu.
Mpogolo aliwataka wafayabiashara wote katika eneo hilo la Kariakoo, kushiriki bonanza hilo ili kupata fursa ya kutafakari mambo mbalimbali hususani yanayohusiana na shughuli zao.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa eneo hilo la Kariakoo, Severin Mushi, aliwataka wafanyabiashara hao, kutumia bonanza hilo kama fursa ya kuzungumza na Kamishna Mkuu wa TRA kwa kuwa ni miongoni mwa watakaoshiriki ili kuendelea kupata elimu katika mambo mbalimbali yanayowatatiza kuhusiana na kodi.

"Hiii ni fursa nzuri kwetu wafanyabiashara wa Kariakoo, kushiriki bonanza pamoja na viongozi ambao wanaweza kutupatia majibu au kutuelimisha kwenye baadhi ya mambo yanayotutatiza ni muhimu, tusiiache ipite,"alisema Mushi.

Alisema kauli mbiu katika bonanza hilo  ni kuzima zote na kuwasha bonanza la TRA' na kwamba wameitumia hiyo ili kuleta hamasa kwa wale wote watakao jitokeza kushiriki katika
bonanza hilo.
1