Coastal kambini mapema Julai

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 07:41 AM Jun 25 2024
Nembo ya Klabu ya Coastal Union.
Picha: Mtandao
Nembo ya Klabu ya Coastal Union.

UONGOZI wa Klabu ya Coastal Union umesema utaingiza kambini mwanzo mwa Julai kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya kimataifa pamoja na yale ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa timu hiyo, Steven Mguto, alisema malengo yao ni kufanya vema katika mashindano hayo kwa kusajili wachezaji watakaoongeza ushindani. 

"Tutaanza kambi mapema kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo, malengo yetu ni kushika nafasi ya juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kimataifa," alisema Mguto. 

Alisema msimu uliopita ulikuwa na ushindani mkubwa kutokana na maandalizi yaliyofanywa na kila timu kuhakikisha hazishuki daraja. 

Mgutoa alisema msimu ujao unatarajiwa kuwa na ushindani zaidi, hivyo kunahitaji kujipanga kikamilifu na kuwataka mashabiki wao waendelee kuwaunga mkono kama walivyofanya msimu uliopita.

"Ninaomba mashabiki wetu waendelee kutupa ushirikiano kama walivyotufanyia msimu uliopita ili tuweze kutimiza malengo yetu," alisema Mwenyekiti huyo. 

Aidha, aliwataka wachezaji wasibweteke kipindi hiki cha mapumziko na badala yake waendelee kufanya mazoezi ili wazidi kuimarisha miili yao.