Biashara yaanza biashara asubuhi Ligi Championship

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:21 AM Sep 24 2024
TIMU ya Biashara United
Picha:Mtandao
TIMU ya Biashara United

TIMU ya Biashara United ilianza vema kampeni yake ya kutaka kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani, Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara, dhidi ya Maafande wa Transit Camp, katika mchezo wa raundi ya kwanza Ligi ya Championship iliyoanza wiki iliyopita.

Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa na Januari Benson na kuipa pointi tatu mbele ya mashabiki wa timu hiyo.

Wakati Biashara United iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu wa 2021/22 ikianza vema, timu ya Polisi Tanzania iliyoteremka msimu wa 2022/23, ilianza vibaya Ligi ya Championship kwa kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Mbuni FC.

Polisi Tanzania pamoja na kuwa nyumbani, Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, ilishindwa kabisa kukabiliana na maafande wenzao wa Mbuni FC wenye maskani yake Arusha na kujikuta ikipoteza nyumbani katika mchezo wa kwanza.

Kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, wenyeji, Kiluvya FC ya Pwani, walishindwa kuutumia vema uwanja wa nyumbani kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Stand United.

Bao la Stand United, timu iliyoshuka daraja msimu wa 2019/20 kutoka Ligi Kuu, lilipachikwa nyavuni na Nassor Idd.

Michezo hiyo ilikuwa inakamilisha raundi ya kwanza ya ligi hiyo, ambapo baada ya kukamilika, Mtibwa Sugar inasimama kileleni baada ya wiki iliyopita kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Green Warriors.

Songea United inashika nafasi ya pili, Mbuni FC ikiwa nafasi ya tatu, Stand United ikikamata nafasi ya nne na Biashara United nafasi ya tano.

Hizi ndiyo timu tano zilizopata ushindi kwenye raundi ya kwanza, zote zikiwa na pointi tatu na zinaachana tu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.