MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imemtia hatiani Joshua Kiloso na kumhukumu kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi kilo 275.
Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki katika masijala ndogo Arusha mbele ya Jaji Immaculate Banzi baada ya pande zote mbili kufunga ushahidi.
Katika hati ya mashtaka, ilidaiwa kuwa Juni 6, 2023, katika kijiji cha Losinoni Juu, wilayani Arumeru, mkoa wa Arusha, mshtakiwa alikutwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya bangi kilo 275.
Mshtakiwa alikana mashtaka na upande wa mashtaka kwa kuthibitisha makosa hayo, uliita mashahidi watano na vielelezo saba.
Katika shauri hilo, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Mseley Mfinanga aliyesaidiwa na Amanda Lushakuzi na upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Zuberi Ngawa.
Akisoma sehemu ya ushahidi, Jaji Banzi alisema shahidi wa pili alidai walipata taarifa mshtakiwa anajihusisha na biashara ya dawa za kulevya na walichukua hati ya kufanya upekuzi nyumbani kwake.
Inadaiwa walifanya upekuzi katika nyumba yake maeneo ya Losinoni Juu na kukuta viroba vikiwa na majani makavu yaliyosadikiwa kuwa dawa za kulevya pembeni mwa kitanda.
Shahidi alidai walikuta viroba 11 vyenye dawa hizo na mshtakiwa alipoulizwa, alikiri kwamba ulikuwa mzigo wake.
Inadaiwa shahidi wa tatu alichukua sampuli ya majani kwa ajili ya uchunguzi na baada ya uchunguzi taarifa kutoka kwa mkemia ilibainisha kuwa majani hayo yalikuwa bangi.
Mshtakiwa, wakati wa kujitetea, alikana kuhusika katika tukio hilo, alikana kukamatwa eneo la tukio, ambalo ni nyumbani kwake na pia alikana kuitwa Joshua Akwii Msila na kudai jina lake halisi ni Joshua Msila Kiloso.
Alidai kuwa Mei 27, 2023 alikuwa Ngaramtoni anauza viazi na maparachichi ndipo alipokamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi KIA, alikaa wiki tatu, akahamishiwa Polisi Boma akawekwa mahabusu siku mbili na kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha ambako alikaa mahabusu hadi Juni 15, 2023 alipopelekwa mahakamani.
"Mahakama imezingatia ushahidi wa pande zote mbili. Hoja iliyopo ni endapo upande wa mashtaka wameweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka yoyote.
"Kwa mujibu wa kanuni, ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka kwamba mtuhumiwa alisafirisha kilo 275.0 za bangi kama inavyodaiwa kwenye shtaka," alisema.
Jaji alisema kuna ushahidi wa moja kwa moja wa shahidi wa pili unaodai mshtakiwa alikamatwa nyumbani kwake, walifanya upekuzi na kukuta viroba 11 vya bangi na kwamba ushahidi huo unaungana na ushahidi wa mashahidi wengine walioshuhudia upekuzi.
"Kama mshtakiwa anadai hakukamatwa eneo la tukio, alitakiwa kusema hayo mapema wakati wa usikilizwaji wa awali, mshtakiwa alikana kuitwa Joshua Akwiina kudai huyo ni mtu mwingine.
"Hakuna ubishi kwamba jina hilo ni tofauti na Joshua Msila Kiloso na kisheria ni watu wawili tofauti," alisema Jaji Banzi.
Alisema kwa mujibu wa shahidi wa pili ni kwamba mshtakiwa alijitambulisha mwenyewe jina hilo na alijitambulisha hivyo ili kukwepa kesi.
"Baada ya kupitia ushahidi, mahakama inaona upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kosa dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka, mshtakiwa alikutwa na bangi viroba 11 nyumbani kwake, hivyo mahakama inamtia hatiani kwa kosa aliloshtakiwa nalo la kusafirisha dawa za kulevya.
"Kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya, mtuhumiwa akitiwa hatiani, adhabu ya lazima ni kifungo cha maisha. Katika kosa hilo sina chaguo lingine bali kumpa adhabu ya lazima, hivyo mahakama inamuhukumu kifungo cha maisha gerezani Joshua Msila Kiloso kwa jina maarufu Joshua Akwii Msila.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED