PSSSF kulipa mafao ya uzeeni Sh. bilioni 560.79 kwa mwaka 2024/25

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:07 PM Nov 13 2024
 PSSSF kulipa mafao ya uzeeni Sh. bilioni 560.79 kwa mwaka 2024/25
Picha:Mpigapicha Wetu
PSSSF kulipa mafao ya uzeeni Sh. bilioni 560.79 kwa mwaka 2024/25

KWA mwaka 2024/25 pekee Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unatarajia kuwalipa Mafao ya Uzeeni Wastaafu 11,622 jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 560.79.

Aidha, Mfuko pia utalipa pensheni ya kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni 980.33 kwa wanufaika wanaotarajiwa kufikia 190,000.

Hayo yamebainishwa Jijini Mwanza leo Novemba 13, 2024 na Mkurgenzi wa Mipango na Uwekezaji PSSSF, Fortunatus Magambo, kwa niaba ya mkurugenzi mkuu, katika semina ya mafunzo kwa wastaafu watarajiwa wa jiji la Mwanza wanaochangia PSSSF.

Semina hiyo inalenga kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuishi baada ya kustaafu utumishi wa umma, ambapo kauli mbiu inasema “Uwekezaji wenye Tija Utakupa Uhakika wa Maisha Baada ya Kustaafu.”

“Fedha hii ni nyingi, na hivyo ikiingia kwenye mzunguko itachachua uchumi, kwani elimu tunayowapatia inalenga kuwajengea uwezo wa namna ya kupanga maisha yao baada ya kustaafu ikiwa ni pamoja na fursa za uwekezaji wa mafao yao ili mafao hayo yaweze kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi na kuongeza fursa za ajira.” amefafanua Magambo.

Kwa upande wake, mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng'wilabuzu Ludigija, amewaasa wastaafu hao watarajiwa kuzingatia elimu watakayopewa na kuepuka ushauri kutoka kwa matapeli.