Utata mauaji Katibu wa CCM

By Francis Godwin , Nipashe
Published at 01:07 PM Nov 14 2024
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, Christina Kibiki.
Picha:Mtandao
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, Christina Kibiki.

UTATA umeibuka katika tukio la mauaji ya kinyama ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, Christina Kibiki (56), wajukuu wake wakidai kuwa kabla ya bibi yao kuuawa, alibakwa sebuleni kisha kuingizwa chumbani alikouliwa kwa kitu chenye ncha kali.

Asifiwe Kibiki, mmoja wa mashuhuda wa mauaji hayo, alidai kuwa wauaji hao walikuwa zaidi ya watatu, mmoja aligonga mlango kuwa ana shida na bibi yao.

"Baada ya kugonga mlango, walimwulizia bibi na wakati bibi anatoka nje kwenda kumsikiliza, ghafla walimgeuzia kibao na kuanza kumshambulia na kumvutia ndani, dada yangu alipojaribu kumsaidia alipigwa na kuanguka chini," alidai.

Shuhuda huyo alidai kuwa baada ya dada yake kuanguka chini, mtu huyo wasiyemjua, alimvutia ndani bibi yao na kuanza kumbaka na wakati huo wao walikimbia nje kupiga kelele kuomba msaada.

Alidai kuwa aliyekuwa anatenda ukatili kwa bibi yao, alikuwa na silaha mfukoni yenye mfanano na bastola, hali iliyowafanya kuogopa zaidi.

"Huyu mtu mmoja aliyekuwa akimbaka bibi, aliingia ndani pekee yake ila nje wenzake wawili walikuwa wakiimarisha ulinzi mmoja, alikuwa akinywa soda na mwingine akitazama watu ila sijui kama baadaye wote waliingia ndani," alidai.

Shuhuda huyo alidai kuwa baada ya kumfanyia ukatili huo sebuleni bibi yao, walimvutia chumbani kwake na kuanza kumchoma na vitu vyenye ncha kali kisha kumtupa kwenye boksi lililokuwa chumbani kwake.

Shuhuda huyo alimweleza mwandishi wa habari hizi aliyefika jana katika kitongoji cha Banawano, kijiji cha Ugwachanya, kata ya Mseke, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kupata undani wa tukio hilo lililotokea juzi saa tatu usiku wa Novemba 12 mwaka huu.

Ni tukio hilo lililoacha simanzi kwa familia, majirani na viongozi wa chama.

Kwa mujibu wa Asifiwe Kibiki, mjukuu wa marehemu, Christina alivamiwa na kijana ambaye hakutambulika mara moja.

Asifiwe alidai kuwa mvamizi huyo aliingia ndani ya nyumba kwa ghafla na kufanya unyama huo kisha kumwacha bibi yake akiwa hoi. 

"Baada ya shambulio, tulisikia mlipuko kama bomu, na majirani walikusanyika kwa ajili ya kutoa msaada, lakini watuhumiwa walikuwa tayari wametoroka," aliongeza.

Festo Mwangamila, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Banawano, alisema kuwa alipofika eneo la tukio baada ya kupigiwa simu, watuhumiwa walikuwa wameshatoweka. 

"Tukio hili ni la kwanza kutokea katika kitongoji chetu na limeleta hofu kubwa," alisema Mwangamila.

Laula Kilienyi, Diwani wa Viti Maalumu Tarafa ya Mlowe, akimzungumzia Christina, alimtaja kama kiongozi shupavu, mchangamfu na mpenda watu.

"Atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jamii na uongozi bora," alisema Diwani Kilienyi aliyekuwa anazungumza kwa huzuni.

Shakila Kiwanga, Diwani wa Kalenga, alielezea jinsi alivyopokea taarifa za tukio hilo saa tano usiku kutoka kwa mtoto wa marehemu. Alifuatilia haraka mkasa huo hadi Hospitali ya Tosa Maganga, ambako alikuta Christina akiwa na hali mbaya kiafya.

"Lakini baada ya muda mfupi, tulipata taarifa za kifo chake, jambo lililotuuma sana," aliongeza Kiwanga.

Wakati mjukuu wa marehemu huyo akidai bibi yake alibakwa kabla ya kifo chake, Dk. Thomas Malongo, Mkurugenzi wa Tiba katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa (Tosa Maganga), alisema walimpokea Christina akiwa hajitambui, huku akiwa na majeraha mengi mwilini na kuvuja damu puani na masikioni.

Alisema kuwa Christina amepoteza maisha kutokana na majeraha mawili ya vitu vyenye ncha kali na kuwa hawawajaona dalili za kubakwa.

"Madaktari walijitahidi kuokoa maisha yake kwa kuzuia damu kuvuja zaidi, lakini isivyo bahati alifariki dunia baada ya saa moja na nusu," alisema Dk. Malongo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini wahusika. 

"(Christina) alipigwa risasi kifuani na kitu kizito kichwani, na watuhumiwa walitoroka bila kuchukua kitu chochote nyumbani kwa marehemu," alisema Kamanda Bukumbi.

Alisema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa zozote zitakazosaidia kukamatwa kwa wahalifu hao ili kuhakikisha haki inatendeka.