TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Dodoma imekusanya Sh. milioni 308.6 ndani ya siku 10 baada ya kuendesha msako wa makusanyo yatokanayo na leseni za biashara, ushuru wa huduma na ushuru wa mabango kwa wafanyabiashara wa kata za Madukani, Uhuru na Majengo za jijini.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Victor Swella, aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa robo ya kwanza ya mwaka huu.
Alisema msako huo ulifanyika kwa ushirikiano wa ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma. Kati ya fedha hizo, Sh. milioni 107.5 ni za leseni ya biashara na Sh. milioni 194.8 zimetokana na ushuru wa huduma, huku Sh. milioni 6.2 zikitokana na ushuru wa mabango.
Alisema msako huo umetokana na TAKUKURU kupata taarifa za kuwapo watu wanaofanya biashara bila kuwa na leseni na wengine wanakwepa kulipa ushuru sahihi kwa Halmashauri ya Jiji.
"Tulianza ufuatiliaji katika kata hizi tatu na kukusanya kiasi hicho cha fedha na tutaendelea na zoezi hili katika maeneo mengine ya biashara, lengo ni kutaka kila mmoja alipe ushuru sahihi, na wafanyabiashara wafanye biashara wakiwa na leseni ili kuepuka upotevu wa mapato," alisema Swella.
Alisema TAKUKURU pia imebaini upungufu katika miradi 40 yenye thamani ya Sh. bilioni 6.3 kati ya miradi 58 ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Dodoma, ikiwamo ya uboreshwaji miundombinu ya shule za msingi na sekondari.
Swella alisema taasisi hiyo inaendelea na ufuatiliaji wa miradi hiyo na kutoa ushauri wa namna bora ya kurekebisha upungufu uliopo na kuchukua hatua za kudhibiti mianya ya rushwa.
Swella pia alisema taasisi hiyo imepokea malalamiko yenye viashiria vya rushwa kutoka kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Alisema malalamiko mengi ni yale ya wagombea kukatwa majina na kuongeza kuwa taasisi hiyo imerejesha suala hilo kwa vyama husika vya siasa.
Swella alisema moja ya vipaumbele ambavyo TAKUKURU wamejiwekea ni pamoja na kuongeza kasi ya uelimishaji umma kuhusu madhara ya rushwa katika uchaguzi na ufuatiliaji utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED