KUCHOMA MKE KWA MAGUNIA YA MKAA: Mawakili wa utetezi wajitoa katika kesi

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 01:23 PM Nov 14 2024
Mshtakiwa Khamis Luwongo maarufu kwa jina la Meshack anayetuhumiwa kumuua mke wake, Naomi Marijani akizungumza na Wakili wake, Mohamed Majaliwa ndani ya chumba cha wazi cha Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kabla ya kesi yake kuanza kusikilizwa.
Picha:Grace Gurisha
Mshtakiwa Khamis Luwongo maarufu kwa jina la Meshack anayetuhumiwa kumuua mke wake, Naomi Marijani akizungumza na Wakili wake, Mohamed Majaliwa ndani ya chumba cha wazi cha Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kabla ya kesi yake kuanza kusikilizwa.

JOPO la mawakili wanne wanaomtetea mfanyabiashara Khamis Luwongo (38) anayetuhumiwa kumuua mkewe Naomi Marijani na kisha kuuchoma moto mwili wake kwa kutumia magunia mawili ya mkaa, wamejitoa kumtetea kwa madai anawadharau na hawaheshimu.

Vilevile, mshtakiwa Luwongo amedai hawezi kuwalazimisha kwa sababu anayeteseka ni yeye wao, wanarudi nyumbani kulala na wake zao, huku akirudishwa gerezani, ndiyo maana wanaomba tu mapumziko ya kutaka kwenda kula.

Mawakili hao, Mohamed Majaliwa, Mikidadi Zidadi, Fatuma Abdul na Jaquim Kamuli, waliomba juzi mbele ya Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kujiondoa baada ya mshtakiwa kutokuwa na imani nao.

Luwongo alifikia hatua hiyo baada ya Wakili wake, Majaliwa kuomba mahakama mapumziko kidogo kama ya dakika 30 kwa sababu kesi ilianza kuanzia saa 4:42 asubuhi hadi saa 7:12 mchana bila mapumziko, lakini mshtakiwa hakukubaliana na suala hilo.

Mshtakiwa alinyoosha mkono mbele ya Jaji Hamidu Mwanga, na alipotakiwa asimame na kuzungumza, alidai kuwa anaona mawakili wake hawako makini na kesi yake, hivyo anaomba mahakama asimame mwenyewe kujitetea.

"Mawakili wangu hawako 'serious', kama wao wamechoka mimi niendelee mwenyewe. Ni kesi ya muda mrefu, wao wanataka kwenda nyumbani, mimi ninakwenda gerezani, break (mapumziko) ya nini, waseme wameshindwa niulize mwenyewe maswali kwa mashahidi," alidai Luwongo.

Baada ya mshtakiwa kudai hayo, Wakili Majaliwa alidai kuwa hawezi kumwudhi bosi wake, kwa hiyo waendelee na shahidi wa upande wa mashtaka.

Jaji Mwanga alimtaka Wakili wa Serikali Mkuu Yasinta Peter azungumze naye kuhusu hoja hizo, alibariki hoja ya mapumziko kidogo kwa sababu kuna wengine wanaumwa, wanakunywa dawa na wengine wagonjwa wa kisukari, wanahitaji mapumziko.

Baada ya hoja hizo, Jaji Mwanga alimwita shahidi mara tatu kwa kumtaka asimame juu, lakini hakusikia ndipo aliposimama jaji akamwuliza 'shida nini?'. Akadai kuwa mawakili wake wanamchanganya.

"Usichanganyikiwe, hii kesi inaisha, tupate mapumziko kidogo turudi hapa ndani saa 8:50 mchana," alisema Jaji Mwanga. 

Baada ya ahirisho hilo, mshtakiwa Luwongo alitoka kizimbani kwa hasira akielekea nje huku akimwelekeza askari magereza kwamba waondoke.

Ilipofika saa 9:21 mchana, mahakama ilianza tena baada ya mapumziko, Wakili Peter alieleza mahakama kwamba hakuna kilichobadilika, jopo ni lilelile, wakamwita shahidi ili waendelee na usikilizwaji.

Baada ya Jaji kumwuliza Wakili Majaliwa kwa upande wao, alianza kwa kuomba radhi kwamba mahakama haiwezi kuendelea na kesi hiyo kwa sababu tayari mteja wake ameonesha kutokuwa na imani naye, na pia alidai ifikie hatua mawakili waheshimike.

"Samahani sana Mheshimiwa Jaji, mimi siwezi kuendelea, mteja wangu ameonesha dharau na pia hatuheshimu, anasema hatupo 'serious' wakati nimeacha shughuli zangu zote nipo hapa, kuna kesi yangu Mahakama ya Temeke imefutwa kwa sababu ya kesi hii.

"Ifikie hatua wateja wetu watuheshimu, mimi siwezi kuendelea, nimekaa naye gerezani zaidi ya mwaka mmoja halafu anasema mimi sijui maumivu ya mahabusu, amenikosea sana, siwezi kuendelea naye," alidai Wakili Majaliwa.

Wakili Mikidadi naye akasimama, akaeleza mahakama kwamba anaomba ajiondoe kwa sababu amechoka na dharau za mteja wao na pia ameonesha kutowaamini.

"Mheshimiwa Jaji, siwezi kuendelea, nimechoka na hiki anachokifanya mteja wetu, hatuamini! Mimi mwenyewe kwa sasa simwamini," alidai Wakili Abdul kwa upole sana kuonesha hajapendezwa na kitendo alichokitenda mteja wao.

Naye Wakili Kamuli ambaye alipangwa na mahakama kumtetea mshtakiwa huyo, pia aliomba ajitoe kwa madai kuwa mshtakiwa hana imani naye, isije ukatoka uamuzi akadai wao ndiyo wamesababisha.

"Mnajua ninyi ni maofisa wa mahakama, mnatakiwa kuisaidia. Kama mnataka niwatoe, ninataka mshtakiwa mwenyewe aseme kwani yeye amewakataa? Unajua suala hili ni kunyongwa hadi kufa na huyu ni shahidi wa 12?" alisema Jaji Mwanga.

Baada ya hoja hiyo, Jaji Mwanga alimgeukia Mshtakiwa Luwongo na kumwuliza kama amewakataa mawakili, akadai kwamba hana haja ya kuwabembeleza, waondoke kwa sababu kuna mawakili wengi tu wanakwenda gerezani kutaka kumtetea.

Baada ya Jaji kusikiliza hoja hizo, aliwaondoa mawakili hao katika kesi hiyo kama walivyoomba. Kesi imeahirishwa hadi Novemba 18 mwaka huu, mshtakiwa amepewa muda wa kutafuta wakili, lakini alisisitiza anataka kujitetea mwenyewe.

Mshtakiwa Luwongo ambaye ni mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam, anadaiwa kuwa Mei 15, 2019, akiwa Gezaulole, Kigamboni, alimuua Naomi Marijani.