MAWAKILI wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Fernidand Makole na Jebra Kambole, wameeleza utaratibu wa askari kumkamata raia, wakisema ni lazima ajitambulishe na awe na hati ya ukamataji.
Wamesema kwa mujibu wa sheria za Tanzania, taratibu za ukamataji zinamtaka Polisi akienda kumkamata mtuhumiwa ajitambulishe, aoneshe hati ya ukamataji (arrest warrant) na kwamba wakiwa na gari, liwe la Polisi linalotambulika.
“Waliohusika kwenye tukio la mfanyabiashara Deogratius Tarimo wawe ni Polisi au watu wengine, wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa wamekiuka sheria,” alisema wakili Makole.
Wakili Kambole ameandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, kwamba: “Usikubali kukamatwa na mtu kavaa kiraia, gari halina namba au namba za kiraia, watu ambao hawajatoa vitambulisho, watu wasiokwambia kosa lako na kwamba uko chini ya ulinzi na wasio na hati ya ukamataji.”
Mawakili hao wametoa elimu hiyo, baada ya kusambaa kwa picha mjongeo ikimwonesha mfanyabiashara Deogratius Tarimo, akikamatwa kwa nguvu na watu waliotaka kumwingiza kwenye gari ndogo aina ya Raumu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED