UBUNIFU unabadilisha namna ya kutangaza vivutio vya watalii Zanzibar. Ni kazi ya vijana wapigambizi wanaotumia mbinu na madaha ya kuvutia ili kutangaza na kukaribisha watalii visiwani.
Katika mbinu hiyo, wapigambizi au maarufu wapiga makachu, wanajirusha kutoka juu na kuchupa hadi baharini kwa madaha, wakibeba mabango yenye majina na picha za watu maarufu na vivutio kadhaa.
Ni pamoja na picha ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, bendera za mataifa mbalimbali na maneno ya ukaribisho mfano karibu Zanzibar ufurahie maajabu mengi.
Serikali inawasifu wapigambizi hao kwa kufanya juhudi za ziada kuiunga mkono kuitangaza Zanzibar kitaifa na kimataifa kwenye utalii.
Nipashe inakutana na vijana hao eneo la Forodhani wakifanya makubwa si kutangaza utalii visiwani humu pekee lakini pia wamekwenda mbali zaidi kwa kuonesha dhamira njema kwa maendeleo ya kiuchumi kupitia kuonesha vivutio na rasilimali zilizopo.
Wanasema maendeleo ya visiwa duniani hutegemea kukuza utalii, ujenzi wa hoteli za nyota tatu hadi tano, mvuto wa fukwe za bahari na usalama wa wageni.
Aidha, kukua kwa utalii lazima kuendane na miundombinu hasa barabara ,viwanja vya ndege, usafiri wa ndani, umeme wa uhakika ,matibabu na maji safi na salama.
Hivyo kujitolea kwa vijana wapiga makachu kwenye ufukwe wa Forodhani si kwamba kumeendelea kuitangaza Zanzibar kiutalii ,lakini pia huwavutia watalii wengi wa ndani na nje kutembelea visiwani.
Endapo Wizara ya Utalii Zanzibar moja ya kazi yake ni kufanya matangazo ya kuutangaza utalii kimataifa, basi wapiga makachu wamechemsha bongo zaidi na kuibua ajira hivyo wanastahili kulipwa na kuheshimika.
Kazi kubwa imekuwa ikifanywa na vijana hao ya kujirekodi huku wakiwa hewani na kuchupa baharini wakipiga mbizi kwa madaha, mitindo mbalimbali wakiwa na mabango.
"Karibu Zanzibar, Zanzibar hakuna matata, Zanzibar ni njema atakaye aje, njoo Zanzibar ucheze na sisi, au uogelee na pomboo.”
Zanzibar au Unguja na Pemba hakuna madini ya kutosha lakini rasilimali zake chini ya bahari zinaweza kuendesha maisha ya wananchi ikiwa zitatumika kwa haki, usawa na uwazi, wanasema.
Bahari yake yenye samaki wengi wa aina mbalimbali, misitu yake midogo ya Jozani na Ngezi inawavutia watalii wengi na watafiti wa tiba na dawa za miti.
Kuna mtandao wa barabara kutoka Unguja zinazofika maeneo yote ya kaskazini mashariki na kusini ambako ndiko kwenye hoteli kubwa za kitalii na zaidi bado zipo fursa nyingi ambazo zikitumika kikamilifu zinaweza kubadili mfumo wa maisha kwa Wazanzibari na kuanza kuishi kwa ubora zaidi.
MWINYI AWATAMBUA
Rais Dk Mwinyi anasema wapiga makachu wameiheshimisha Zanzibar kwa sababu kazi wanayoifanya inaonekana dunia nzima kwa kulitangaza taifa na uzuri wake.
Anasema hatua hiyo ya vijana kwa ubunifu bila shaka imeongeza idadi ya watalii wanaofika Zanzibar.
“Video zenu zimesambaa dunia nzima na nimekuwa napokea ujumbe mbalimbali wa pongezi kutokana na kazi yenu mnayoifanya ya kuitangaza nchi hongereni sana vijana wangu”anasema Dk. Mwinyi.
Zanzibar imefungua milango wazi kwa fursa za biashara na uwekezaji na tayari imewakaribisha wadau mbalimbali kushirikiana nao kwenye maono ya ukuaji wa uchumi endelevu na ustawi wa utalii wa muda mrefu.
Hatua hiyo, itaiwezesha Zanzibar kuwa kituo bora cha ushindani kwa utalii kwenye ramani ya dunia, anasema Rais Mwinyi.
Utalii wa Zanzibar umejikita zaidi katika fukwe hivyo ni vyema kuwekeza katika utalii mwingine ikiwemo wa michezo na uwekezaji, aidha Rais Dk. Dk.Mwinyi anajivunia miaka minne ya uongozi wake akiona kwamba sekta ya utalii inapiga hatua kubwa na kuwa uti wa mgongo wa uchumi huku ikichochea uwekezaji wa miradi mbali mbali kwa vijana.
“Utalii unaendelea kuwa tegemeo la kukuza uchumi na uwekezaji ambapo naahidi mazingira mazuri yanaimarishwa na kuona Zanzibar inakuwa kituo bora Afrika katika utalii.” Anasema Rais.
Kadhalika, kwa mujibu wa Rais Zanzibar imefungua milango katika fursa za biashara na uwekezaji ambapo sekta hiyo imepata mafanikio kufuata kujitangaza duniani kote.
Aidha, anaahidi kuhakikisha hakuna vikwazo vitakavyokwamisha maendeleo ya sekta hiyo ambayo inachangia ajira kwa vijana akiongeza.
“Katika miaka minne tumeupa utalii kipaumbele kuona unachangia pato la taifa na kukuza uchumi sambamba na uwekezaji, unaozalisha ajira kwa vijana.”
''Nilipoingia madarakani niliahidi kufanya kazi na sekta binafsi kuendesha nchi na leo mafanikio tunayaona katika upande wa utalii ambapo wenzetu wanafanya kazi vizuri na serikali”.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhan Soraga, anasema sekta ya hiyo inapiga hatua na katika mwaka wa fedha 2024-2025 wataimarisha utalii wa majengo ya kale na kutangaza vivutio viliopo.
Anayataja mafanikio makubwa ya kuimarika kwa sekta ya utalii ikiwemo kuwepo kwa amani na utulivu ambao ndiyo dira itakayowafanya watalii kuendelea kuja Zanzibar.
''Katika kipindi cha miaka minne tumeimarisha sekta ya utalii na kufungua milango ya kuitangaza nje na miongoni mwa mambo yaliyowavutia wageni ni kuimarika kwa amani na utulivu,''anasema.
Waziri Soraga, anaongeza kuwa serikali ikichukua jitihada mbalimbali kuhakikisha inaweka mazingira bora na wezeshi kuinua sekta hiyo ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
"Tutaendelea kushirikiana na wadau kupeleka ajenda ya kukuza utalii mbele ili Zanzibar iwe mfano katika eneo hili," anaahidi.
Hivyo anawakaribisha wadau kuwekeza Zanzibar kwasababu ambayo ni salama kwa mitaji na biashara zao na kwamba miaka minne imeakisi maendeleo endelevu ya sekta hiyo na kukuza biashara na maendeleo hivyo matarajio yake huduma zitaongezeka.
Akilizungumzia eneo la Forodhani kwa wapigaji makachu, anasema ni kivutio kikubwa kuendelea kutangaza Zanzibar kwa sababu utalii ni muhimu.
Mmoja wa wapiga makachu Hassan Othman, anasema ni furaha kwao kuona jambo wanalolifanya linathaminiwa na kuonekana katika mataifa mbalimbali dunianina kuchangia kukuza utalii.
Anasema imekuwa fursa kwa vijana kupata ajira kwa sababu hupata fedha wanazotunzwa na watalii mbalimbali.
Albaina Ally ni mwanamke wa kwanza kuruka makachu katika eneo hilo la Forodhani anasema baada ya kuona umchezo huo ukifanywa na wanaume pekee alishawishika na yeye kushiriki ili wanawake nao wasiachwe nyuma katika fursa mbalimbali ikiwemo za utalii.
“Mwanzo ilikuwa ngumu lakini nikasema ngoja nijaribu, siku ya kwanza nilishindwa kutokana na mazingira ya eneo lenyewe lakini vijana wanaume Forodhani wakaniunga mkono na uthubutu wangu umevuta wanawake wengi kujikita katika mchezo huu,”anasema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED