MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,ametoa siku saba kwa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) ,kufanya ukaguzi wa ubora wa mbegu ya zao hilo wilayani Kishapu, na kumpatia taarifa.
Ametoa agizo hilo jana kwenye kikao chake na Maofisa Ugani na Watendaji wa Kata wilayani Kishapu, akiwa ameambatana na Balozi wa pamba nchini Aggrey Mwanri.
Alisema, kufuatia malalamiko ambayo yametolewa na maofisa ugani na baadhi ya viongozi, kwamba mbegu za pamba ambazo zimeanza kusambazwa wilayani humo kwa ajili ya msimu wa kilimo 2024/2025, zimeonekana kutokuwa na ubora,na hivyo kutoa siku saba zifanyiwe ukaguzi na kupewa taarifa juu ya hali za mbegu hizo.
“Mbengu zilizoletwa Kishapu kuna baadhi zimethibitika hazifai, hivyo kazi ambayo nimetumwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kurudisha heshima ya zao na Pamba, na kazi ambayo anaifanya Balozi wa Pamba Aggrey Mwanri,bila ya kuwepo kwa ubora wa mbegu za Pamba itakuwa bure,”alisema Macha na kuongeza.
“Bodi ya pamba mnapaswa kufanya ukaguzi wa Mbegu zote za pamba ambazo zimeanza kusambazwa kwa wakulima wilayani Kishapu, mjihakikishie kama mbegu hizo zinafaa, kama hazifai mlete mbegu zingine zenye ubora, ili kazii hii ambayo nimetumwa na Rais ifanyike kwa ufanisi, ni natoa siku saba nipate taarifa ya hali ya mbegu wilayani Kishapu”.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph Mkude,naye alikazia suala la ubora wa mbegu za pamba,kwamba mbegu za 2023/2024 ambazo zinasambazwa kwa wakulima zinalalamikiwa siyo nzuri, na tayari amesharudishiwa baadhi ya mifuko kutoka kwa wakulima.
Nao baadhi ya maofisa ugani wilayani Kishapu, walisema kwamba mbegu za pamba, ambazo wameletewa kwa ajili ya kuzisambaza kwa wakulima, zimeonekana kutokuwa na ubora.
Mkaguzi wa pamba wilayani Kishapu kutoka Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) Thomas Tiluhongerwa,akiangalia mbegu za pamba ambazo zinaelezwa kuwa ni mbovu, amekiri siyo nzuri sababu zina unyevuunyevu, na kubainisha huenda wakati wa kusafirishwa zilinyeshewa mvua.
Aidha, alisema watazifanyia ukaguzi mbegu zote za Pamba wilayani Kishapu ili kuona ubora wake, na kwamba ndani ya siku saba watampatia taarifa Mkuu huyo wa Mkoa juu ya hali ya Mbegu hizo za Pamba wilayani humo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED