Wadau wa maziwa mkoani Mwanza wamefundwa kuhusu namna bora ya kuzingatia sheria za usajili wa biashara na taratibu za kuomba vibali, ili kukuza biashara zao na kufanya biashara yenye tija.
Kikao kazi kilichofanyika kati ya Bodi ya Maziwa na wadau mkoani Mwanza, kilifunguliwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Peter Kasere, ambaye alisema kuwa uzalishaji wa maziwa mkoani Mwanza kwa mwaka 2023/2024 ulifikia lita milioni 398.53, lakini wastani wa asilimia 0.6 tu ya maziwa hayo yalifanyiwa usindikaji kupitia viwanda vidogo vinavyopatikana mkoani humo.
Kasere alieleza kuwa ili kuimarisha tasnia ya maziwa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza imejielekeza katika kuboresha mazingira ya ufugaji wenye tija, huku ikihakikisha uwekezaji katika viwanda vya kusindika maziwa unakuwa mkubwa. “Mpaka sasa, Mkoa unajumla ya mashamba makubwa 15 ya ng’ombe wa maziwa na chama kikubwa cha ushirikika wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa (UWAWAMWA) ambacho kimeanza kuchakata mtindi na yogati. Pia, kuna viwanda vidogo 13 vya kuchakata maziwa,” alisema.
Kasere aliongeza kuwa jitihada za kuhamasisha kilimo cha malisho bora ya ng'ombe, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, pamoja na kuendeleza uanzishwaji wa kiwanda cha maziwa cha Mabuki, zinaendelea.
Afisa Sheria wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Haruna Maarufu, aliwahimiza wafanyabiashara wa maziwa kuzingatia sheria za usajili ili kuepuka adhabu zinazoweza kutozwa. “Usajili wa wadau wa maziwa unafanywa kwa mujibu wa Sheria ya Maziwa, Sura 262 ya mwaka 2004, kifungu 17(1) na 17(2), pamoja na kanuni ya usajili ya mwaka 2007 na marekebisho yake ya mwaka 2020 kifungu cha 4(1) na 4(2),” alisema Maarufu.
Afisa Masoko kutoka Bodi ya Maziwa, Hamisi Kiimbi, akitoa elimu kuhusu taratibu za kuomba vibali vya kutoa au kuingiza maziwa nchini, alisema kuwa serikali inatoa vibali ili kulinda afya za walaji na kuweka ukomo wa bidhaa hiyo sokoni.
Rehema Mwalugala, mfugaji wa ng'ombe, alieleza kuwa ni muhimu kuboresha ufugaji kwa kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu namna ya kufuga, kutunza, na kulisha wanyama kwa utaratibu mzuri ili kupata maziwa bora.
Maimuna Sarige, mfanyabiashara wa maziwa, aliongeza kuwa ili kuwa na kizazi kinachotambua thamani ya mifugo, elimu kuhusu maziwa inapaswa kutolewa mashuleni. “Serikali iangalie namna ya kuingiza maudhui ya elimu ya maziwa kwenye mtaala wa shule ili vijana waelewe umuhimu wa sekta ya maziwa,” alisema Sarige.
Alisisitiza kuwa serikali inapaswa kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo wanaotumia vifungashio vya madumu ya maji mitaani, kuwaelimisha kuwa maziwa yanayotolewa katika vifungashio hivyo si salama kwa matumizi. Pia, aliiomba serikali kuhakikisha wajasiriamali hawa wanapata vifungashio vinavyokidhi vigezo vya afya.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED