ZIKIWA zimebaki siku 16 watanzania kuchagua viongozi wao kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, baadhi ya vyama vimeendelea kulia kutokana na wagombea wao kuenguliwa.
Chama cha ACT-Wazalendo kimesema katika Jimbo la Rufiji, wagombea wao 382 wameenguliwa, wakijumuisha wa nafasi ya wenyeviti wa vijiji 28, vitongoji 90 na wajumbe 264.
Kukiwa na kilio hicho ACT - Wazalendo, vyama vingine vya upinzani vimedai kuwa wagombea wake wengi majina hayaonekani kwenye orodha ya walioteuliwa tangu Novemba 8, mwaka huu na kuanza mpango wa kukata rufani kutaka warejeshwe.
Viongozi wa vyama hivyo wamedai kuwa wakiwa katika harakati za kukata rufani, hata wachache walioteuliwa siku hiyo, nao jana walianza kuenguliwa.
Miongoni mwa vyama ambavyo vimeendelea kulia kukumbwa na kadhia hiyo mbali na ACT, ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF).
CHADEMA imesema kuwa ikiwa inapambana kushughulikia rufani kwa wagombea wake ambao majina yao hayakuonekana siku ya kwanza baada ya orodha ya walioteuliwa kutoka, limeibuka lingine kwa wagombea waliokuwa wameteuliwa nao kuanza kuenguliwa.
"Tulikuwa bado tunashughulikia suala la kukata rufani na mpaka sasa ni baadhi tu ya maeneo ambayo rufani zetu zimepokewa ila maeneo mengi walifunga ofisi na kutokomea," alidai Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema.
Katika mazungumzo na Nipashe jana, Mrema aliendelea kusema, "Wakati tunapambana kushughulikia hao walioenguliwa juzi (Novemba 8), tumepata taarifa nyingine kwamba bado watu wetu waliokuwa wameteuliwa awali nao wanaendelea kuenguliwa muda huu. Mfano, Manispaa ya Iringa, walioteuliwa wote, wameenguliwa.
"Tarime Vijijini, Sumbawanga, Same, Buhigwe, Manonga, Igunga, Rufiji, Tunduma na maeneo mengi ya nchi, bado watu wetu wanaenguliwa, hivyo tunaendelea na hatua ya kukata rufani japo hatujui kama tutawakuta wahusika ofisini ili wapokee rufani zetu au watafunga, tutajua idadi yote kamili baadaye baada ya kazi ya kuengua itakapokamilika," alisema Mrema.
Alisema sababu kuu ambayo wameambiwa wagombea wao wanaenguliwa ni kutokana na kuwekewa pingamizi.
"Kwa mfano, Iringa wagombea wetu wameambiwa wamewekewa pingamizi ila hawajapewa nakala kama ulivyo utaratibu ili wajibu hayo mapingamizi. Maeneo mengine wanapigiwa simu kuambiwa wameenguliwa," alisema Mrema.
Msemaji wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Chama cha ACT-Wazalendo, Rahma Mwita, naye alilalama wagombea wengi wa chama hicho waliokuwa wamepitishwa, nao kuenguliwa kwa madai ya kuwekewa pingamizi, wakidaiwa kwamba hawajui kusoma na kuandika.
"Wale waliokuwa wameenguliwa ile siku ya kwanza Novemba 8, majina yalipotolewa, tulifanikiwa baadhi yao kukata rufani wakarejeshwa, lakini tatizo lingine limeibuka wameondolewa tena, eti wamewekewa pingamizi.
"Si wao tu hata maeneo mengi ambako wagombea wetu walipita, nao wameondolewa. Kwa mfano, maeneo ya Ruangwa, Lindi, Kibiti, Rufiji, Bariadi, wameondolewa wote," alisema Rahma.
Alisema chama hicho kinapanga kukaa kikao na kitatoa tamko la msimamo wa chama wakati wowote.
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano kwa Umma wa CUF, Mohamed Ngulangwa, alisema ombi kubwa la chama hicho ni serikali iwarejeshe wagombea wote walioenguliwa.
"Sisi tumesema hili tangu jana (juzi) baada ya wagombea wetu wengi kuenguliwa. Lakini kubwa ni wito wetu kwa serikali, kwamba wagombea wote walioenguliwa kwa hila kwa vyama vyote vya upinzani, warejeshwe bila urasimu ili wananchi wakachague viongozi wanaowataka Novemba 27," alisema Ngulangwa.
Juzi baada ya kuwekwa hadharani majina ya walioteuliwa na wasioteuliwa kugombea nafasi za uenyekiti na ujumbe, baadhi ya vyama vilitoka hadharani na kudai wagombea wake ‘kukatwa’ huku vikionesha kutoridhishwa na sababu zilizotolewa.
Kwa mujibu wa kanuni 18 GN Na.571 na 574, ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (2024), uteuzi wa wagombea ulipaswa kufanywa Novemba 8, mwaka huu.
Pingamizi kuhusu uteuzi wa wagombea ni kuanzia Novemba 8 hadi 9 na uamuzi wa pingamizi ulipaswa kutolewa kuanzia Novemba 8 hadi 10 jana, hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya 23.
Rufani dhidi ya uamuzi kuhusu pingamizi zitapokewa kuanzia Novemba 10 na 13 na uamuzi wa kamati ya rufani utatolewa kuanzia Novemba 10 hadi 13 mwaka huu, hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya 23.
Kadhalika, kampeni za uchaguzi huo zitafanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni kuanzia Novemba 20 hadi 26, kwa mujibu wa kanuni ya 26.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED