ABIRIA 14 wamenusurika kifo katika ajali iliyohusisha basi na treni ya mizigo iliyotokea juzi katika makutano ya reli Malagarasi na Nguruka, mkoani Kigoma.
Kwa muujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Shirika la Reli Tanzania (TRC), treni ya mizigo yenye namba za usajili Y611 iliyokuwa ikitokea Kigoma kuelekea Tabora, iligongwa na basi lenye namba za usajili T 545 DJW, mali ya kampuni ya Clasic linalofanya safari zake Kigoma-Dar es Salaam.
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kuwa ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia juzi na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi kulipita basi lingine lililokuwa limesimama mbele kwa ajili ya kupisha treni, hivyo kugonga treni.
Ajali hiyo ilisababisha mabehewa matano kati ya 30 kuanguka na kusababisha majeraha kwa abiria wa basi ambao kati yao, wanane walikuwa wanawake na sita wanaume na hakuna aliyepoteza maisha.
Kupitia taarifa hiyo, TRC ilitoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kufuata sheria na kuheshimu vivuko vya reli ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED