MBIO za Coast City awamu ya tatu zinatarajiwa kufanyika Novemba 30 mwaka huu zikiwa na lengo la kuchangia miundombinu ya kitaaluma katika Shule ya Msingi Pangani iliyopo Halmashauri ya Mji wa Kibaha.
Mwenyekiti wa Coast City Marathon Dk. Frank Muhamba ameyasema hayo leo Novemba 11,2024 alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari Mjini Kibaha kuhusiana na mbio hizo zinazofanyika zikiwa na malengo tofauti.
Akizindua vifaa vya michezo vitakavyotumika katika mbio hizo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Theresia Kyara amepongeza uwepo wa mbio hizo ambazo ni sehemu mojawapo ya mazoezi yanayowaepusha wananchi na magonjwa yasiyoambukiza.
Kyara amesema mbio hizo zimekuwa ni sehemu pia ya kuwajengea wananchi tabia ya kufanya mazoezi, kuibua vipaji pamoja na kuunga mkono juhudi za serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
"Wadau tuungane na waandaaji wa mbio hizo kwa kushiriki moja kwa moja kwani pamoja na lengo lao la kuchangia miundombinu ya elimu pia unafanya mazoezi na kuepuka na magonjwa yasiyoambukiza mwili inakuwa imara,".amesema.
Balozi wa Coast City Marathon Twaha Ambiere amesema mbio za mwaka huu ni za tofauti kwani wameweka vitu ambavyo ni vya asili ya Pwani ikiwemo madafu na pweza ambavyo vitakuwa ndani ya kifurushi kwa atakayejisajili kushiriki mbio hizo.
Ambiere amesema mbio hizo zitahusisha kilomita 2.5 kwa watoto, Km 5, 10 na 21 ambazo wadau wanatakiwa kujitokeza kujisajili kwa wakati Ili malengo yaweze kufikia .
Mmoja wa wadhamini wa Coast City Marathon mwakilishi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Hafsa Ally amesema katika awamu mbili zilizopita walishiriki kama wadhamini na awamu hii ya tatu wanaendelea kufanya hivyo kwakua mbio hizo zinalenga mambo ya maendeleo kwenye Jamii.
Wadhamini wengine ni Tigo,Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Lise Schools, Davis&shirliff na benki ya CRDB.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED