Chumvi ni bora lakini ni hatari zaidi zama hizi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:52 AM Nov 12 2024
Ukiongeza chumvi chakula kinakuwa kitamu zaidi lakini ni hatari. Unapaswa kuacha kuiongeza chumvi mbichi mezani kwenye mlo. Weka kiasi kidogo halafu ipikwe.
Picha:Mtandao
Ukiongeza chumvi chakula kinakuwa kitamu zaidi lakini ni hatari. Unapaswa kuacha kuiongeza chumvi mbichi mezani kwenye mlo. Weka kiasi kidogo halafu ipikwe.

CHUMVI hufanya chakula kuwa na ladha. Pia ni muhimu kwa maisha ya mwanadamu. ‘Madini ya ‘sodiamu’ yaliyoko katika chumvi ni muhimu kudumisha kiwango sahihi cha maji mwilini. Pia huwezesha seli kunyonya virutubisho.

“Chumvi ni muhimu katika maisha,” anaeleza Paul Breslin, profesa wa sayansi ya lishe katika Chuo Kikuu cha Rutgers nchini Marekani.

"Chumvi ni muhimu sana kwa seli za binadamu , ikijumuisha nyuroni  au mishipa ya fahamu yote , ubongo, mgongo na misuli yetu yote. Pia ni muhimu kwa ngozi na mifupa.” 

Lakini , Profesa Breslin anaonya, ikiwa hatuna sodiamu ya kutosha tutakufa maana seli na mishipa ya fahamu haiwezi kufanya michakato yake. 

Upungufu wa sodiamu mwilini husababisha kuchanganyikiwa, hasira, misuli kutofanya kazi vizuri, kukakamaa  na hata koma au kiharusi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza kula chumvi kiasi cha gramu tano kila siku yenye gramu mbili za sodiamu.

Lakini wastani wa kula chumvi kimataifa ni karibu gramu 11 kwa siku. Hilo huongeza hatari ya magonjwa ya moyo na mishipa, saratani ya tumbo, unene, maradhi ya mifupa na ugonjwa wa figo.

WHO inakadiria watu milioni 1.89 hufa kila mwaka kutokana na matumizi ya chumvi kupita kiasi. 

Katika nchi nyingi, matumizi ya chumvi kupita kiasi hutokana na kiasi kilichofichwa katika vyakula vilivyochakatwa.

Watu wa Kazakhstan hutumia karibu gramu 17 za chumvi kwa siku, zaidi ya mara tatu ya kiasi kilichopendekezwa na WHO.

Maryam anaishi Astana,  ambao ni mji mkuu wa Kazakhstan, anataja sababu za kula chumvi kwa wingi, : “Ni kutokana na urithi wetu. Kwa karne nyingi tulizunguka misituni, tukiwa na nyama ambazo zilipaswa kuhifadhiwa kwa kutumia chumvi."

"Familia zilihifadhi nyama kwa msimu wa baridi. Wanaweza kuhifadhi ng'ombe mzima, kondoo na hata nusu farasi."

Miaka minane iliyopita, binti wa Maryam alikuwa na matatizo ya kiafya. Daktari wake alimshauri apunguze vyakula vyenye sukari nyingi, mafuta na chumvi kwa wingi. Familia iliacha mara moja kuongeza chumvi kwenye chakula chao. Na hatimaye  Mariyam na jamaa zake walizoea maisha bila kuongezwa chumvi. 

Unapokula chumvi, ladha yake unaihisi  kwenye ulimi na kaakaa laini la koo.

“Chumvi hutia nguvu mwili na akili pia,” anasema Profesa Breslin.

Sodiamu huyeyuka kwenye mate. Kisha huingia kwenye seli za ladha na kuamsha seli moja kwa moja.

“Chumvi hupeleka mawimbi ya umeme ambayo huamsha mawazo na hisia. Kwa hivyo mwili na akili zetu huchangamka.” Anaongeza.

Athari ya chumvi kwenye mwili inategemea muundo wa vinasaba wa mtu. Zaidi ya watu bilioni moja duniani kote wanakabiliwa na shinikizo la damu. Kupunguza ulaji wa chumvi kunaweza kusaidia kuzuia hilo na kutibu tatizo hilo linalosababisha koma au  kiharusi wakati mwingine.

"Unapokuwa na chumvi nyingi, jambo la kwanza ambalo mwili wako hufanya ni kuiyeyusha. Kwa hivyo shinikizo la damu hupanda ili kusukuma maji ya ziada,” anaeleza Claire Collins, profesa wa lishe na milo katika Chuo Kikuu cha Newcastle nchini Australia.

"Ikiwa una udhaifu wowote katika mishipa yako ya damu, kama ile ya ubongo, inaweza kupasuka na kusababisha kiharusi."

Nchini Uingereza, wastani wa matumizi ya chumvi umepungua hadi gramu nane kwa siku, ambayo bado ni zaidi ya viwango vilivyopendekezwa. Upunguzaji huo unatokana na kanuni walizowekewa watengenezaji wa chakula kupunguza viwango vya chumvi.

Ulaji wa chumvi unaopendekezwa hutofautiana kutoka nchi hadi nchi. Kipimo cha mkojo kinaweza kugundua ikiwa mwili wako una chumvi nyingi au kidogo. 

KUIPUNGUZA 

Hata kama kiwango chako cha chumvi ni cha juu, kupunguza kunaweza kuwa sio rahisi sana. Lakini Prof Collins anahimiza kula  mkate au tambi au chakula kingine chochote ambacho kina kiwango cha chini cha chumvi.

"Ikiwa unapika chakula chako mwenyewe weka mitishamba na viungo badala ya chumvi." Anasisitiza. Ni maelezo ya BBC Swahili. 

CHUMVI NI UHAI

Kwa upande wa mitandao mingine, wanyama wote wenye damu moto, lazima wale chumvi ili kuishi. Ubongo wa binadamu pamoja na uti wa mgongo, vimo katika mfuko wa maji chumvi uitwao ‘cerebrospinal fluid (csf)’. Umajimaji huu huzunguka sehemu zote za ubongo na uti wa mgongo.

Machozi ni chumvi na jasho pia ambalo pia ni chumvi. Mifupa  ina uwazi katikati yake au  uroto ambamo seli za damu hutengenezwa. 

Uroto umefunikwa na tabaka nyingi za chumvi kalisiamu kama vile kamba inavyoshikizwa pamoja. ‘salt crystals’ au chenga chenga za  chumvi,  zinashikizwa pamoja na kalisiamu, na ndizo zinazoifanya mifupa  kuwa imara, na siyo kalisiamu pekee.

Mifupa inamiliki asilimia 27 ya chumvi yote mwilini. Wakati mwili unahitaji chumvi zaidi, huikopa toka mifupani, jambo hili likitokea, kalisiamu huondolewa pamoja na chumvi na kuifanya mifupa kuwa miembamba, laini na midhaifu.

Chumvi imeundwa kwa sodiamu na klorini, kwa pamoja inaitwa; ‘sodiamu kloraidi’  

VYAKULA NA CHUMVI

Wakazi wa ukanda wa pwani kuanzia Tanga hadi Mtwara huhifadhi vyakula kwa chumvi tena huwekwa nyingi ,mfano ni dagaa, nyama, papa na nguru pamoja na samaki  kutoka Morogoro wanaokaangwa na kujazwa chumvi.