Tenga afurahishwa kiwango Mashindano ya Taifa ya Watoto

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 04:35 PM Jun 24 2024
MWENYEKITI wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Leodgar Tenga.
Picha: Mpigapicha Wetu
MWENYEKITI wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Leodgar Tenga.

MWENYEKITI wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Leodgar Tenga amefurahishwa na viwango vilivyoonyeshwa na vijana katika mashindano ya Taifa ya Watoto ya kuogelea yaliyomalizika mwishoni mwa wiki kwenye bwawa la kuogelea lililopo katika Shule ya Kimataifa Tanganyika(IST) Masaki Dar es Salaam.

Tenga aliyasema hayo baada ya kumalizika kwa mashindano hayo yaliyoshirikisha klabu mbalimbali kutoka mikoa ya Tanzania Bara pamoja na Visiwani Zanzibar. 

"Vijana wameonyesha uwezo mkubwa katika mashindano haya ambayo yalikuwa na upinzani mkubwa, hii imetokana na juhudi kubwa inayofanywa na makocha wao" alisema Tenga.

Alisema anawapongeza viongozi wa Chama cha Mchezo wa kuogelea Tanzania (TSA) kwa juhudi wanayoifanya kuhakikisha mchezo huo unazidi kukua, pamoja na wazazi ambao wanawaunga mkono vijana wao. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama hicho Amina Mfaume alisema mashindano yalikuwa na muamko mkubwa kwani watoto wengi wamevunja rekodi kwa kupunguza muda. 

"Mashindano yalikuwa na muamko mkubwa watoto wengi wamefanikiwa kupunguza muda jambo ambalo linazidi kutupa matumaini ya kuona mchezo wetu unazidi kukua, alisema Mfaume.