Serikali kuja na mpango wa nchi nzima kufanya mazoezi

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 10:12 AM Jun 24 2024
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa.

WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, wanaandaa mpango wa nchi nzima wa kushiriki michezo mbalimbali ya kushughulisha mwili ikiwamo mpira wa miguu na yoga ili kukabiliana na magonjwa yakiwamo yasiyoambukiza, imeelezwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Yoga, iliyoandaliwa na Ubalozi wa India nchini.

Maadhimisho hayo kwa mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Yoga kwa ajili ya mtu binafsi na kwa ajili ya jamii nzima.”

Msigwa alisema kwa sasa wizara hizo zipo kwenye mazungumzo kuhusu suala hilo ambapo mpango huo ukikamilika utahusisha pia, mazoezi ya kukimbia na michezo mingine.

“Siku ya Yoga ni muhimu kwa kuwa maudhui yake yanafaida kwa mtu binafsi na kwa jamii kama kaulimbiu isemavyo 'Yoga ni sehemu ya kujenga mwili. Kila mmoja akiamua mazoezi kuwa sehemu ya maisha yake atakuwa na afya njema na kukabiliana na magonjwa,” alisema.

Alisema wataalamu wanasema sehemu kubwa ya maradhi yanayosababisha vifo vya watu duniani kwa sasa ni yale yasiyohusisha kuushughulisha mwili.

Alisisitiza kuwa mtu akiwa na afya mbovu atatumia fedha nyingi katika matibabu, lakini mwenye afya njema atafanya kazi na kujenga uchumi binafsi na wa taifa.

Mwakilishi wa Balozi wa India nchini, Naibu Balozi Manoj Verma, alishukuru wadau mbalimbali waliojitokeza katika maadhimisho hayo yaliyohusisha pia wanafunzi kutoka shule mbalimbali.

Alisema mazoezi ya yoga yanahusisha upumuaji, kulegeza viungo vya shingo, mikono na miguu, jinsi mtu anavyotakiwa kusimama na kukaa na mikao ya kuegemea na kutafakari kwa kina.

Neema John ambaye ni mmoja wa washiriki wa mazoezi hayo, alisema mazoezi hayo ni mazuri na muhimu kwa wale ambao hawawezi kushiriki michezo kama kukimbia au kutembea mwendo mrefu, kwa kuwa hayatumii nguvu bali viungo vya mwili na akili.

Yoga inatambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), na mazoezi yake huhusisha vitu viwili, viungo vya mwili na fikra ambapo mtu anapata muda wa kufanya tafakuri kwa kukaa kimya peke yake hivyo kuimarisha afya ya akili.