Maandalizi mashindano ya Gofu Lina Tour yashika kasi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:32 AM Jun 26 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Mmoja wa washiriki wa mashindano ya Gofu Lina Tour, Madina Idd, akiwa mazoezi. Mashindano hayo yatafanyika viwanja vya Gymkhana Arusha kuanzia Julai 11, mwaka huu.

WACHEZAJI wa gofu wa kulipwa, Nuru Mollel aliyeshinda raundi ya kwanza katika viwanja vya TPC Moshi na Hassan Kadio aliyeutwaa ubingwa wa raundi ya pili mjini Morogoro, ndiyo vinara katika orodha ya wachezaji waliosajiliwa kucheza katika raundi ya tatu ya mashindano ya kumuenzi mchezaji wa gofu kwa wanawake, Lina Nkya, mjini Arusha katikati ya mwezi ujao.

Mashindano hayo ya aina yake yanayoandaliwa kwa pamoja na familia ya Nkya kwa kushirikiana na Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU) na kile cha wachezaji wa Kulipwa (TPGA), yanakutanisha wakali wa gofu ya kulipwa na ridhaa nchini.

Arusha Gymkhana wanakuwa wenyeji wa raundi ya tatu baada ya zile mbili za mafanikio makubwa katika viwanja vya TPC na Morogoro.

Akizungumza na mwandishi wetu jana, Mkurugenzi wa Mashindano hayo, Yasmin Chali, ametaka wale ambao hawajajiandikisha kufanya hivyo mapema maana nafasi zilizosalia ni chache.

Alisema mashindano yataanza rasmi Julai 11 na kumalizika Julai 14, mwaka huu, mjini Arusha.

Chali alisema jumla ya mashimo 72 yatachezwa katika siku hizo nne, ikiwa na maana kutakuwa na mbio za mashimo 18 kila siku.

“Kila kitu kinakwenda vema katika maandalizi yetu na viwanja vya Gofu vya Arusha viko katika ubora unaotakiwa kwa ajili ya mashindano haya,” alisisitiza Chali. 

Aliongeza kuwa pia kutakuwa na mashindano kwa ajili ya wachezaji wa kawaida na kitengo hiki kwa mujibu wa Chali kinajulikana kama 'Subsidiary Event'.