Wizi madini waumiza kichwa Shinyanga, imejipanga kwa makali ya kisu ikomeshe

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 11:17 AM Nov 15 2024
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, akionesha fedha Sh.milioni 97 na madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 930.88 yenye thamani ya Sh.milioni 93, zilizokuwa zinatoroshwa na watu Ilogi wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Picha:Marco Maduhu
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, akionesha fedha Sh.milioni 97 na madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 930.88 yenye thamani ya Sh.milioni 93, zilizokuwa zinatoroshwa na watu Ilogi wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

KUNA walakini wa kiutawala, kuhusu utoroshaji madini, mamlaka zote za usimamizi mkoani hapa zikilalamika kuwapo mipenyo yenye athari za moja kwa moja kiuchumi.

Huo ni utoroshaji madini unaofanywa kwa asilimia kubwa na wachimbaji wadogo, wakishirikiana na baadhi ya watumishi wa sekta hiyo.

Jambo hilo linatokea huku tovuti ya Wizara ya Madini inafafanua wachimbaji wadogo wa madini, wamekuwa wakichangia Pato la Taifa katika eneo hilo kwa asilimia 40 kufika  mwaka 2023. 

Mwaka 2019 serikali kupitia Tume ya Madini, ilianzisha masoko ya madini kwa nchi nzima, hasa kwenye maeneo yanakochimbwa madini, lengo ni kusaidia wachimbaji wadogo kuuza madini kwa urahisi na kupata fedha halali, kuzuia utoroshaji wa madini pamoja na serikali kupata mapato kupitia tozo mbalimbali.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kwamba masoko hayo ya madini katika miaka ya nyuma yalisaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti mianya ya utoroshaji madini, na kuzuia kuwapo na mtiririko haramu fedha zake.

Waziri wa Madini, Athony Mavunde akiwa mkoani Tanga Septemba 15 mwaka huu, akifunga Kikao Kazi cha Menejimenti ya Tume ya madini, anasema mkoa wa kimadini Kahama, ndio unaoongoza kwa utoroshaji madini.

Hilo linatolewa ufafanuzi na Ofisa Madini mkazi mkoa huo wa kimadini, Winfrida Mrema, anayekiri utoroshaji madini umekuwa ukisababisha serikali kukosa mapato na watu kujipatia fedha haramu kinyume cha utaratibu.

Anasema, kwa sasa wapo kwenye msako wa kuwakamata wanaojihusisha na utoroshaji huo wa madini, na kuna kundi la waliokamatwa.

Hapo anadokeza kuwapo ofisa mmoja wa madini anayetuhumiwa kushiriki vitendo hivyo na wapo kwenye mikono ya sheria, huku hatua za kikao kisheria zikichukua nafasi.

“Utoroshaji wa madini ni tatizo kubwa kwa serikali kukosa mapato, mfano mwaka 2023 tulipangiwa kukusanya kiasi cha fedha Sh. bilioni 29.75, lakini tukakusanya bilioni 24.9,” anasema Winfrida.

Anaeleza kwamba, mwaka huu kiserikali wamepangiwa kukusanya Sh. bilioni 34.6, lakini hadi Septemba wameshakusanya Sh. bilioni 32.12 sawa na asilimia 92.63.

Hapo ofisa huyo anafafanua ni mwenendo mzuri, hasa ikitokana na kuanza kudhibiti mianya ya utoroshaji madini.

DC KAHAMA

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita anaeleza hatua walizochukua kudhibiti mianya ya utoroshaji madini, kwa kushirikiana na Tume ya Madini.

Hapo anataja walianza kufanya vikao na wadau wa madini kubaini sababu zinazochangia  kukithiri kwa utoroshaji, hasa kwenye machimbo na masoko ya madini.

Anasema baada ya kukaa nao, wadau walitoa hoja na sababu za madini kutoroshwa, ikiwamo madai ya kuwapo tozo nyingi kutoka kwenye halmashauri, na kuwapo upungufu wa masoko ya madini.

Mboni anasema, baada ya masoko mengine kufungwa likiwamo la Segese likabaki moja tu la Kahama Mjini.

“Hoja hizi tulizipokea na tupo kwenye utaratibu wa kuzifanyia kazi na katika kuendelea kudhibiti mianya ya utoroshaji madini.

“Pia tumeimarisha ulinzi zaidi kwenye uwanja wa ndege Kahama, machimboni dhahabu na kwenye masoko ya madini, yani kila sehemu tumeweka watu wetu,” anasema Mboni.

Anasema kwamba msako bado unaendelea wa kuwakamata watu ambao wamekuwa wakitorosha madini, na ambao huwakamata wamekuwa wakiwachukulia hatua kali za kisheria na kuwafungia leseni zao.

Mkuu wa Wilaya anasema, msako huo, katika Mgodi wa Mwime wameshawafungia wachimbaji watatu kujihusisha na madini na kwamba katika soko la madini Kahama, wamewafungia pia lesseni zao wafanyabiashara watatu kutokana na kuhusika na utoroshaji huo wa madini. 

Anasema, baada ya kudhibiti tatizo hilo la utoroshaji madini kwa kiasi kikubwa, wameanza kuvunja rekodi ya ukusanyaji mapato, ambapo kwa mwezi Julai pekee wamekusanya Sh. bilioni 11, lakini awali walikuwa wakikomea Sh. bilioni 9.

MRATIBU UWEKEZAJI 

Mratibu wa Uwekezaji mkoani Shinyanga Dotto Maligisa, anasema tatizo la utoroshaji madini Kahama, linasababishwa na jengo la soko la madini kuwa dogo, na hivyo wafanyabiashara wa madini kukosa usiri na kuhofia usalama wao.

Mwenyekiti Mpya Soko la Madini, Mkoa wa Kimadini Kahama, Zabroni Ngereja, akichukua nafasi ya aliyekuwapo, anasema wamefanikiwa kudhibiti tatizo la utoroshaji madini uliokuwapo hapo awali kwa asilimia 99.

Anatahadharisha kwamba, mfanyabiashara atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo vya utoroshaji madini, iwe ndani ya soko, maeneo ya wachimbaji au kufadhili utoroshaji, watamuondoa asiendelee kufanya biashara hiyo na kutowachafua.

“Utoroshaji wa madini ambao upo kwa sasa hivi ni kwenye maeneo ya machimbo madogo, ukiwamo mgodi wa Nyangarata, Nyikoboko,Nyamishiga, Masabi na maeneo mengine. Huko ndipo serikali  inapaswa kwa sasa kuwekeza nguvu nyingi,”anasema Ngereja.

MCHIMBAJI 

Mchimbaji Mdogo wa madini kutoka machimbo ya Mwime Kahama, Joseph Masunga, anasema tatizo la utoroshaji madini linasababishwa na uchache wa masoko na tozo nyingi.

 Mfanyabiashara wa madini Mpanzu Nswila, anasema kwamba utoroshaji huo wa madini ni hasara kwa taifa kwa kukosa mapato na kushindwa nchi kunufaika na rasilimali zake na kunufaisha mataifa mengine.

RPC SHINYANGA

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi, anasema wamekuwa wakikamata watu wanaojihusisha na utoroshaji wa madini, na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Anasema walishakamata watu sita wakitorosha madini ya dhahabu wilayani Kahama, yenye uzito wa gramu 930.88 yenye thamani ya Sh. milioni 93.

Anasema uchunguzi wa awali, walibaini watuhumiwa hao walikuwa wakitorosha madini kuyapeleka nje ya nchi, kwa lengo la kukwepa kulipa kodi na tozo za Serikali, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

“Tatizo hili la utoroshaji madini lipo sana katika wilaya ya Kahama. na sisi kama Jeshi la polisi tumekuwa tukifanya msako na doria mbalimbali na kuwakamata watuhumiwa wakitorosha madini na kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria,”anasema Magomi.

MKUU WA MKOA

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, anasema tamko la waziri wa madini Anthony Mavunde, kusema mkoa wa kimadini Kahama unaongoza kwa utoroshaji wa madini ni aibu kwa mkoa, na kwamba na siyo habari njema bali wanapaswa kudhibiti tatizo hilo.

Anasema tayari wameshabaini maeneo mbalimbali ambayo hufanyika biashara hiyo haramu ya utoroshaji madini, ikiwamo kwenye viwanda vya kukoboa mpunga.

“Biashara ya utoroshaji madini ambayo inafanyika Kahama hufanyika pia kwenye viwanda vya kukobolea mpunga, wakati shughuli za kukoboa zikiendelea kumbe kuna madalali wanafanya biashara haramu za madini, hii ni aibu kwetu kama mkoa,” anasema Macha.

Anasema katika misako ambayo wanaendelea nayo ya kudhibiti mianya ya utoroshaji madini, kwamba wakikuta biashara hiyo haramu ikiendelea tena kwenye viwanda vya kukoboa mpunga, wahusikawatachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kuruhusu biashara hizo.

Anasema, mkoa wa kimadini Kahama unafanya vizuri katika uzalishaji wa madini, lakini tatizo jingine ni soko la madini kuzidiwa, na kuagiza iwekwe mikakati ya kuongeza ukubwa wa soko hilo, ili kudhibiti tatizo la utoroshaji wa madini na watu kuuza mali katika masoko hayo.