“HALI ilikuwa ngumu kwenye familia zetu muda mwingi ni kuwaza nitapata maji leo? Kukaa kisimani kusubiri maji wakati mwingine kulazimika kukesha kuyangoja yakusanyike huku tukiwaacha watoto pengine wagonjwa peke yao usiku nyumbani.”
“Upo muda unapata changamoto za akili na hata kuchanganyikiwa kwa kukosa maji nyumbani. Hakuna ya kupikia, kufulia wala kunywa lakini pia kuwaacha watoto peke yao nyumbani na kutembea usiku na hata wa manane ni adha,” anasema Saida Munishi.
Ni mkazi wa Kitongoji cha Mjembe kata ya Kibindu, mkoani Pwani, akitaja machungu yanayoumiza kinamama wakati wa kusaka maji anapozungumza na Nipashe.
Anaongeza kuwa ni mengi hasa umbali na kisima walichokuwa wakitumia kukosa maji ya uhakika au kuwa vigumu wengi kuyapata.
Ni jambo lililosababisha kutumia muda mwingi kusaka huduma hiyo, kuwaza na kuwazua lakini pia kuongeza hofu kwa wanafamilia wengine wanaobaki nyumbani hasa watoto na wenye mahitaji wakiwamo wagonjwa.
“Kuna wakati wanaume pia wanakuwa na wasiwasi tunapochelewa kisimani lakini ilifikia kipindi wakaanza kuwaisindikiza wake zao. Ni hasa wanapokosa maji mchana inawalazimu kwenda kukesha kisimani kusubiri maji na tunarejea nyumbani usiku mnene,” anasimulia.
Anasema hali hiyo inathibitisha ukweli kuwa ukosefu wa huduma muhimu za kijamii hasa maji, tiba na nishati vinarudisha nyuma maendeleo ya wanawake na kuongeza pengo la ukosefu wa usawa kijinsia, kijamii na kiuchumi.
Anasema pia kunasababisha baadhi ya shughuli zao kwenda kinyume na mipango huku wakiwa chanzo cha watoto kuchelewa kula, kusoma, kuwa na mazingira masafi kisa kukosekana maji.
Saida anaishukuru serikali kwa kuwachimbia bwawa la maji linalowawezesha kupata maji karibu na maeneo yao na pia kufanya vizuri shughuli zake za mama lishe ambazo awali alikuwa akifanya kwa kusuasua kutokana na shida ya maji.
“Lakini pamoja na shukrani tunachoomba sasa ni Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) watuunganishie maji yafike karibu na makazi yetu. Vituo vya maji vikiwa maeneo ya nyumbani shughuli nyingi za maendeleo zitafanyika,” anasema.
Anaeleza kuwa kwa sasa watoto wao wanaishi kwenye mazingira safi tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuwepo kwa bwawa hilo ambapo maji ya kufulia yalipatikana kwa nadra.
Fatuma Ramadhani mkazi wa Mjembe, anasema eneo ambalo walikuwa wakifuata maji kabla ya kuwapo bwawa hilo walitembea zaidi ya saa moja tofauti na sasa ambapo maji yanapatikana karibu na yanawawezesha kufanya shughuli zao za nyumbani na kiuchumi kwa wakati.
Bwawa hilo ambalo ni chanzo cha kisima kitakachojengwa Mjembe unakwenda sambamba na ujenzi wa kisima hicho ambacho ni kati ya 40 vinavyojengwa mkoani Pwani.
Mbali ya Mjembe katika kata ya Kibindu pia wakazi wa Kitongoji cha Diagala Kijiji cha Dihozile wamefikishiwa huduma ya maji ya kisima na kuondokana na kutumia maji ya malambo.
Mmoja wa wakazi wa Diagala, Lucy Kilekeni anaishukuru serikali kwa kuwafikishia huduma hiyo na kuwaondolea adha ya kununua dumu la lita 20 kwa Sh 1,000.
Lucy anasema kabla ya mradi huo kufika katika kitongoji chao walikuwa wanalazimika kutumia maji ya lambo na kununua ya kunywa yaliyokuwa yakipatikana mbali.
Meneja wa RUWASA, Beatrice Kasimbazi anasema visima hivyo vinachimbwa kupitia mradi wa uchimbaji wa visima.
Anasema visima 40 vitakavyochimbwa kwa mkoa wa Pwani vipo katika mradi wa visima 900 vitakavyochimbwa katika mikoa mbalimbali kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi.
Aidha, kupitia mradi huo wa visima wakazi 32,750 katika mkoa huo wanatarajia kunufaika na kwamba vingi vitachimbwa katika majimbo nane kati ya tisa.
Beatrice anasema Sh bilioni 2.4 zitatumika katika utekelezaji wa programu hiyo inayofanyika na kwamba utekelezaji wa mradi huo wa visima kwa mkoa wa Pwani ulianza Agosti 2024.
Meneja huyo anasema mbali ya mradi wa visima pia ipo miradi 35 yenye gharama ya bilioni 35.8 ambazo inaendelea kutekelezwa.
Anasema ikikamilika itahudumia wakazi 180,528 na kuongeza hali ya upatikanaji wa maji kwa asilimia 8.1 na hivyo kuufanya mkoa kuwa na asilimia 88.4 ya upatikanaji wa maji ifikapo Desemba mwaka huu.
Mhandisi anasema katika mradi wa visima maeneo yaliyopewa kipaumbele ni yale ambayo hayakuwa na huduma ya maji kabisa hicho ndio kilikuwa kigezo kikubwa.
"Kati ya visima hivi 40 vinavyojengwa Pwani itapata visima virefu 35 . Vinachimbwa na vitano vinatumia vyanzo mbadala ikiwamo mabwawa na ifikapo Januari 30 vyote vitakuwa vimekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi," anasema .
Halikadhalika anasema ushirikishwaji wa wananchi na elimu vinaendelea kufanyika kuhakikisha miradi hiyo inalindwa kwa ajili ya kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji na miundombinu ya maji.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Maji, Kundo Matthew anafanya ziara katika mkoa wa Pwani akikagua miradi ya visima inayosimamiwa na RUWASA pamoja na mingine ya DAWASA.
Akiwa katika ziara hiyo anasema ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwapatia maji safi na salama wananchi karibu na makazi yao jambo ambalo kwa mkoa huo linatekelezeka kwa kasi.
Katika ziara hiyo anazungumza na wananchi ambao aliwakumbusha kutunza miundombinu ya maji ili huduma hiyo iwe endelevu.
"Wananchi tunzeni miundombinu ya maji ili adha mliyokuwa mnaipata isijirudie, serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miradi ya maji ili shughuli zenu zisikwamishwe na kukosa huduma hii, ni mpango wa Raisi wetu wa kumtua mama ndoo kichwani tunautekeleza kwa vitendo," anasisitiza.
Miradi ya maji inayojengwa kwa mkoa huo gharama ya kununua maji ndoo moja kutoka kwenye vituo haizidi Sh. 100 kulingana na utaratibu uliowekwa na wananchi na yapo maeneo makundi maalumu wakiwamo wazee hupata huduma hiyo bure.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED