Tunaua utalii wetu, kugeuza wanyamapori matahira!

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 08:49 AM Jan 17 2025
news
Mchoraji: Msamba
Katuni.

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), huko nyuma liliwahi kuwa na Meneja Uhusiano wake mahiri, akiitwa James Lembeli, ambaye baada ya utumishi wake serikalini kukoma, aliingia kwenye siasa na kuwa Mbunge wa Kahama.

Akiwa Tanapa, aliitendea haki nafasi yake, kutokana na jinsi alivyoelimisha umma kuhusu hifadhi ya maliasili, akishirikiana vema na vyombo vya habari na akiwa tayari wakati wote kutolea ufafanuzi kwa lililotakiwa. 

Wakati wake, Lembeli alijiwekea utaratibu wa kuhakikisha wanahabari nchini wanaielewa vema sekta ya maliasili na utalii, akiwapangia ratiba za kutembelea hifadhi na mbuga za wanyama zilizoko nchini. 

Wanahabari walipewa fursa hizo bila gharama, wakifanya utalii wa mafunzo katika maeneo hayo kwa makundi, kwani isingewezekana kuwapeleka wote kwa pamoja, ingawa hata hivyo idadi ya wanahabari haikuwa imefumuka kama ilivyo sasa.

 Alifanya hivyo, akijua wazi kuwa wananchi wote wasingeweza kupata fursa ya kutembelea hifadhi na mbuga hizo, ila walipata ya kusoma, kusikiliza na kutazama kwenye vyombo vya habari na kuelimika. 

Ni bahati mbaya, kuwa Watanzania wengi hawakuwa wakijua umuhimu wa kufanya utalii wa ndani, wakiamini kazi ya kuzuru mbuga na hifadhi ni ya wageni waliofika nchini na kulipa fedha za kigeni na kuchangia Pato la Taifa. 

Hivi sasa, karibu asilimia kubwa ya Watanzania wanajua umuhimu wa utalii wa ndani, ambao idadi kubwa wanaenda kujionea wanyama   kwenye hifadhi na mbuga zetu, tofauti na zamani ambako walijua dhima yao ni kuwinda na kukausha vimoro.

 Hiyo fursa kwa kweli haikunipita, niliipata na kuitumia vema, Lembeli aliponipangia, mimi na mpiga picha wangu, Mpoki Bukuku (Allah aendelee kumpa pumziko la milele), kuzuru hifadhi za Katavi,Rukwa; Ruaha, Iringa na Udzungwa, Morogoro na kujionea, kujifunza na kufunza pia. 

Katika maeneo yote hayo, wahifadhi walikuwa wakituelezea jinsi wanyamapori wanavyotakiwa kuishi tofauti na wafugwao, nini chakula chao na maisha yao kwa ujumla, huku wakihadharisha kutupa taka dhidi ya katika hifadhi. 

Wakatuambia kuwa wanyama hao hawatakiwi kula chakula kingine zaidi ya kinachopatikana porini na ndiyo sababu hairuhusiwi kuotesha chochote hifadhini au mbugani. Yaani hairuhusiwi mimea wakimbizi au wahamiaji haramu katika hifadhi hizo.

 Wakisema ndiyo sababu hata magari yapitayo kwenye mbuga au hifadhi, mathalan barabara zipitazo Mikumi, Serengeti au Ngorongoro, hakuna mtu anaruhusiwa kutupa ganda la ndizi likaliwa na wanyama hao, sembuse karatasi na taka zingine.

 Nia yake ni kuhakikisha kuwa uasili wa maeneo waishimo wanyama hao, unabaki palepale, kwani hata mti uliokatika kwa kuangushwa na tembo au uzee na dhoruba zingine, haukuondolewa humo bali ulisalia kuwa makazi ya wanyama wadogo na wadudu.

 Pia, gogo lilisalia kama chakula chao, hivyo hakuna kigeni kilichoingizwa humo au kienyeji kilichotolewa kwa sababu yoyote ile, ili kulinda uasili wa eneo husika. 

Enzi hizo, hakuna aliyeruhusiwa kuwinda au kuingiza mnyama asiye wa pori na kufanya hivyo kuliendana na adhabu kali na bila shaka inaendelea kudumu.  

Lakini cha msingi, ilikuwa ni wanyamapori wabaki porini kwa utalii. Sijui ni nini kinatokea hivi sasa, tunaposhuhudia wanyamapori kwa kiasi kikubwa wakigeuzwa wa kufugwa mazizini katika maeneo kadhaa nchini, watu wakienda kuwaona na si kutalii, bali kuwalisha kwa kutumia visonzo.

Haishangazi tena, mnyama aliyeogopwa porini mpaka kuitwa mfalme wa pori au nyika, simba, anashikwa mkia, anakumbatiwa na binadamu na kutembea naye kama mwanasesere au tahira fulani hivi. 

Najiuliza hivi dhana ya utalii itaendelea kushika hatamu kwa aina hii ya matendo?

Tunaamini siku zijazo watalii watakuja nchini kutazama wanyama wanaolishwa kwa visonzo kama si kunyweshwa sharubati? Kama tumeamua kuacha haya yaendelee, kuna sababu gani ya kuzuia watu kukamata wanyama pori na kuwachinja kwa kitoweo?

Kigugumizi kimetoka wapi basi cha kufungua maduka ya nyama ya porini kama Serikali siku kadhaa zilizopita, ilivyoamua na baadhi kufunguliwa na ghafla kufungwa? 

Tukae chini tutafakari tena kama utalii utaendelea katika muktadha kama huu. Niko palee!