Sekondari Kibaha na somo la kemia kinara

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 01:41 PM Feb 20 2025
Mwalimu  Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha, George Kazi ambaye pia ni anafundisha somo la Kemia, akionesha vifaa mbalimbali vya kemikali wakati akitoa mafunzo mkoani Arusha.
Picha: Grace Mwakalinga
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha, George Kazi ambaye pia ni anafundisha somo la Kemia, akionesha vifaa mbalimbali vya kemikali wakati akitoa mafunzo mkoani Arusha.

SHULE ya Sekondari ya Wavulana Kibaha, iliyopo mkoani Pwani, imeandika historia ya kipekee katika sekta ya Elimu nchini kwa kuwa ya kwanza kitaifa katika somo la kemia.

Shule hiyo imepata wastani wa alama 1.0, kwenye somo la kemia, kiwango ambacho ni cha juu kwenye mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne mwaka 2024.

Watahiniwa wa mtihani wa kidato cha nne mwaka 2024 walikuwa 104, ambapo 83 walifanya mtihani wa somo la Kemia kati ya hao, 75 walipata alama A na wanane walipata alama B.

Lakini shule ya Kibaha haijafanya vizuri tu katika somo la kemia, hata masomo mengine, kama vile biolojia, ambapo ufaulu wa daraja la A ulipatikana kwa wanafunzi wote 104, fizikia ilipata alama B, na Hisabati alama B.

Matokeo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA) Dk. Said Mohammed na kuweka kwenye tovuti yao, ilionesha  kiwango cha ufaulu katika shule hiyo.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha iliyopo mkoani Pwani, wakiwa katika maabara kwa ajili ya mazoezi kwa vitendo darasani
Matokeo hayo yameifanya shule hiyo kushika nafasi ya nne kitaifa na kuwa ya kwanza kati ya shule zote maalum na za serikali nchini.

Akizungumza na Nipashe, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, George Kazi, anasema  mafanikio hayo yanatokana na malengo makuu matano ambayo walijiwekea, la kwanza lilikuwa ni kupata  wastani wa alama A kwa shule nzima, walifanikiwa kwani wanafunzi wote walifaulu kwa wastani wa daraja la kwanza.

Anasema kati ya masomo 12 yanayofanyiwa mtihani, tisa yalipata alama A ambayo ni Uraia, Jiografia, Historia, Kemia, Kiingereza, Biolojia, Kiswahili, Kilimo na Biashara, masomo ya Hisabati, Fizikia, na Uendeshaji wa Vitabu vya Hesabu (Bookkeeping) yakipata wastani wa alama B.

Anaeleza lengo lingine lilikuwa ni kuifanya kuwa shule ya kwanza kwa shule zote za serikali, limefanikiwa kwa sababu Kibaha ni shule pekee inayohudumiwa na serikali pamoja na Shirika la Elimu Kibaha.

Shule pia ilijiwekea lengo la kuwa bora zaidi kuliko shule nyingine maalum nchini, kama vile Ilboru, Mzumbe, Tabora Boys, Msalato, Kilakala, na Tabora Girls.

Mwalimu Kazi anasema kuwa kati ya watahiniwa 104 wa kidato cha nne mwaka 2024, wote walipata ufaulu wa daraja la kwanza, kati yao, wanafunzi 80 walipata alama kati ya saba na tisa, 16 walipata alama kati ya 10 na 13, na wawili walipata alama 15 na 17.

Kwa matokeo hayo, shule ilifikia wastani wa GPA ya 1.1, ambayo ni sawa na asilimia 98 ya ufaulu, na hivyo kukidhi vigezo vya kushika nafasi ya nne kitaifa, na ya kwanza miongoni mwa shule maalum na za serikali nchini.

Mwalimu Kazi anasema kwamba sekondari ya Kibaha inajipatia umaarufu kutokana na kutoa michepuo ya masomo ya sayansi kama CBA, ECA, PCM, PMC, na PCB.

Anasema michepuo hiyo  ni ya kipekee, na inalenga kuzalisha wataalamu wa afya, wahandisi, wakulima, na wafanyabiashara, mifumo ambayo inaendana na maono ya Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alieanzisha shule hiyo mwaka 1965  akishirikiana na nchi za Finland, Norway na Denmark kama sehemu ya mapambano dhidi ya umasikini, maradhi, na njaa.

MAFANIKIO YA SHULE KATIKA SOMO LA KEMIA

Mwalimu Kazi kufanya vizuri katika somo la Kemia ni matunda ya mafunzo maalum ya walimu kazini, yaliyotolewa kwa walimu kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP).

Walimu 12 wa masomo ya Sayansi na Hisabati katika shule hiyo, wamepata mafunzo ya kina ya ufundishaji, mbinu za tathmini, na matumizi ya teknolojia ya Tehama.

Mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya walimu na wanafunzi, ambao wamekuwa wakitumia mbinu za kujifunza kwa vitendo pamoja na matumizi ya teknolojia katika ufundishaji.

"Wanafunzi wengi hukutana na ugumu wa somo la Kemia kwa sababu ya matumizi ya kemikali, na usipokuwa mwangalifu unaweza kupata madhara, walimu walitumia mbinu za kisasa na za kipekee walizofundishwa ili kuhakikisha usalama wao na wa wanafunzi wakati wa mazoezi ya vitendo, na matunda ya juhudi hizo tumeyaona."anasema.

MCHANGO WA WAZAZI NA SERIKALI KATIKA MAFANIKIO YA SHULE

Mwalimu Kazi anasema wazazi wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya shule,  kwa kutoa msaada wa kifedha kwa walimu wa kujitolea, kufanya vikao vya mara kwa mara, na kushirikiana na shule ili kuboresha elimu.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha iliyopo mkoani Pwani, wakiwa katika maabara kwa ajili ya mazoezi kwa vitendo darasani
Serikali pia inaendelea kuboresha miundombinu ya shule, hadi sasa, mabweni mawili yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 160 yamejengwa, madarasa mawili, na matundu 10 ya vyoo.

Aidha, shule hiyo inaishukuru Bodi ya Michezo ya Kubahatisha kwa kutoa msaada wa Sh. milioni 64, ambao umetumika kujenga kisima chenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 100,000.

Kisima hicho kimesaidia wanafunzi kuondokana na adha ya kutafuta maji mtoni, asa wana uhakika wa kupata huduma ya maji hata kama maji ya Dawasa yatakosekana kwa wiki nzima.

Mwalimu Kazi anasema wajipanga kufanya vizuri zaidi kwa mwaka 2025, anaeleza kuwa wanafunzi 122 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne na kuwa na ufaulu wa daraja la kwanza kwa wote, wanaendelea kuboresha mikakati ya ufundishaji na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.

Katika hotuba yake Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa februari 2022, alieleza dhamira ya Serikali kuwekeza katika masomo ya Sayansi na Hisabati.

Anasisitiza kwamba nchi inahitaji wataalamu wengi katika sekta za sayansi, teknolojia, uhandisi, na hisabati ili kufanikisha malengo ya maendeleo  ni  muhimu kuboresha miundombinu ya shule za sayansi na kutoa mafunzo kwa walimu wa masomo hayo, hatua ambayo inaelekea kutekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia miradi mbalimbali wakishirikiana na wadau kufanikisha.

Akizundua Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 jijini Dodoma, Rais, Samia Suluhu Hassana anasema miongoni mwa mageuzi yaliyopo kwenye sera hiyo ni kufundishwa kwa somo la Tehama, mafunzo ya ufundi stadi kuanzia elimu ya msingi, na matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence).

Anasema lengo la sera hiyo ni kuwafanya wanafunzi kuwa na umahiri na ujuzi unaoakisi mahitaji kitaifa na kimataifa ili kushindana na kushiriki kikamilifu kwenye soko la ajira duniani.

Amesema sera hiyo itazalisha wanafunzi wenye maarifa, maadili, na ujuzi utakaowawezesha wahitimu wa ngazi mbalimbali kujiajiri, kuajiri wengine, na kuongeza uwezo wa ushindani kwenye soko hilo.

Rais Samia, anasisitiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kusimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu kwa lengo la kuwaandaa wanafunzi kuwa mahiri katika kukabiliana na changamoto za sasa na kujibu mahitaji ya dunia ya sasa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano  kwa Umma Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sylvia Lupembe anasema, wizara itaendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu nchini kwa kuhakikisha wanafunzi wanasoma sehemu nzuri, vifaa vya kutosha vya kujifunzia na kufundishia ili kuongeza ufaulu.

Amezipongeza shule zote nchini zilizofanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha nne na kuzihamasisha kuendelea kufanya vizuri na ambazo  hazikufanya vizuri kuongeza bidii.