UFUGAJI nyuki nchini kwa sasa, unachukua nafasi muhimu, kuimarisha maisha endelevu kimazingira na kuwezesha maisha ya pamoja, kati ya wanyamapori na binadamu.
Ingawa, kiasili umekuwa ukitambulika zaidi kwa faida za kiuchumi hususan za uzalishaji asali, sababu za kiikolojia nazo sasa zinachukua nafasi.
Umuhimu wake kiitaalam unatafsiriwa kwenda mbali zaidi ya kuboresha kilimo, ikitajwa nafasi ya suluhisho kwa changamoto za migogoro ya makazi na kijamii, kati ya binadamu na wanyamapori, mfano tembo na binadamu. Vilevile, kuna nafasi ya mwisho wa safari kuhifadhi bayoanuwai.
Kimsingi, ufugaji nyuki una umuhimu mkubwa kwa afya ya binadamu, kupitia bidhaa zake kama asali na nta.
Ikiendewa mbali, asali hutoa nishati na ina viambata vinavyoimarisha kinga ya mwili, huku ikitumika kwa tiba asili kwenye magonjwa kama mafua na vidonda.
Kwa mfano, asali imeonyesha kuwa na uwezo wa kuimarisha kinga ya mwili. kutokana na sifa zake, kama ilivyochapishwa kwenye jarida la Journal of Functional Foods, toleo la mwaka 2017.
Aidha, asali hiyo ina sifa ya kuwa na virutubisho muhimu kama protini, vitamini na madini kadhaa.
NGUVU YA UCHAVUSHAJI
Nyuki ni miongoni mwa wachavushaji muhimu zaidi katika mifumo ya ikolojia duniani. Wanachangia kwa kiasi kikubwa uchavushaji mimea ya mwituni na mazao.
Inatajwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya mimea ya maua duniani, inategemea nguvu ya uchavushaji.
Pia, nyuki hao bado wanachukua nafasi kitakwimu wakichangia kuchavusha takribani asilimia 70 ya mazao yanayoliwa na watu.
NAFASI YA WAFUGAJI
Kwa kuunga mkono ufugaji nyuki, watu huchochea uchavushaji unaoimarisha ukuaji mimea yenye afya kwa binadamu, vilevile una tija kwa uzalishaji unaohitajika kwa ajili ya kutunza makazi ya wanyamapori.
Ni kawaida kwa yuki wanapochavusha mimea, wanasaidia kuzalisha tena mifumo ya kiikolojia, ikiwamo misitu, na nyasi.
Bayoanuwai hiyo ina mtazamo wa kuunga mkono aina mbalimbali za wanyama, kuhakikisha makazi yanabaki imara na salama, pia chanzo cha chakula kwa wanyama.
Kwa jamii zinazoishi karibu na hifadhi au mbuga za wanyama, hilo likitajwa kusaidia kuleta uwiano kati ya uzalishaji kilimo na kuhifadhi mifumo asilia.
Ni hatua inayoongozana na kupuguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
MIFANO ILIVYO
Suluhisho bunifu kama ‘uzio wa nyuki’ safu za mizinga ya nyuki inayozunguka shamba zimetekelezwa katika sehemu mbalimbali Afrika, ikiwamo Kenya na Tanzania.
Ni mizinga inayotajwa kuzuia wanyamapori kuingia shambani, pia inatoa chanzo cha ziada cha mapato kupitia uzalishaji asali.
Faida hizo mbili zinatajwa kuufanya ufugaji huo wa nyuki kuwa njia bora inayopunguza gharama na hatari zinazohusisha migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, huku ikikuza maisha yao pamoja kwa amani.
USHUHUDA WA WAKULIMA
Mkulima kutoka kijiji cha Maharaka wilayani Mvomero, mkoa Morogoro jirani na Hifadhi ya Taifa Mikumi, anasema:
“Mwaka 2013 tulikuwa na programu ya kuzungushia mizinga ya nyuki kwenye mashamba yetu, ili kuzuia wanyama waharibifu. “Tuliona tofauti kubwa, kwani tembo waliokuwa wanavamia, wakawa wanaogopa sana! Kumbe nyuki walikuwa wanafumuka kutoka kwenye mizinga na kuwang’ata tembo wakawa wanaogopa,” anaeleza mkulimaVitus Pango Anaongeza:“Pia, zile kelele za nyuki kama wanavuma hivi nazo ni tishio kwao.”
NYUKI VS MAZINGIRA
Katika suala la kusaidia matumizi endelevu ya ardhi, ufugaji nyuki bado unabaki kuwa na matumizi kidogo ya ardhi, ikilinganishwa na shughuli nyingine za kilimo, hata kufikia hatua kuwa mbadala wa maendeleo endelevu kwa jamii za vijijini.
Tofauti na kilimo chenye matumizi makubwa ya ardhi ufugaji nyuki hauhitaji ukataji ama misitu au uharibifu wa mazingira asilia, bali unahimiza utunzaji wa mimea inayopandwa na ile asilia, ambayo ni muhimu kwa uchavushaji na uhifadhi wa makazi ya nyuki.
Kwa jamii zilizo katika maeneo yenye wanyamapori wengi, suala la ufugaji nyuki unatajwa kuwa chanzo chao cha mipango ya usimamizi endelevu wa ardhi.
Hapo wakulima wanawezeshwa kupata kipato pasipo bila kuingilia makazi ya wanyamapori au kujihusisha na yanayogusa uharibifu ardhi na mimea, kama vile uwindaji, pia ukataji misitu haramu.
Zao lake huwa ni kuchochea uwajibikaji katika kutunza mazingira, kwani wafugaji nyuki wanategemea afya ya mifumo ya ikolojia, ndipo wanapofanikisha riziki zao.
Lingine ni kuimarisha Uchumi na Kupunguza Umasikini, ufugaji nyuki pia unatoa fursa za kiuchumi, hususani kwa jamii zilizoko pembezoni mwa misitu, ikijumuisha wanawake na wakulima wadogo.
Asali na bidhaa nyingine za nyuki ni kama nta, sumu ya nyuki na maziwa yake, huhitajika kimataifa zikiwapa wafugaji wake chanzo cha kipato cha uhakika.
Hapo ndipo inaposhauriwa kwamba, suala la kuwawezesha kiuchumi wanajamii, pia wafugaji nyuki kunapunguza shinikizo utumiaji wanyamapori au kujihusisha na shughuli zisizo endelevu, kama uvunaji kuvuka wa rasilimali misitu.
“Kupitia asali tuliyoivuna kwenye eneo letu hili ambalo tuliweka mizinga takribani kumi ya majaribio,tulifanikiwa kuvuna lita 60 za asali.
“Ndani ya miezi mitatu, pesa iliyopatikana ilitusaidia kununua mahitaji yetu muhimu hapa kwenye eneo letu, ambalo linapakana na mbuga (Hifadhi) ya Mikumi (Morogoro) na mara nyingi wanyama huwa wanaingia kwenye eneo hili” anatamka mdau wake anayejitambulisha kwa jina la Daudi.
Akifafanua yu mdau mkubwa wa uhifadhi kijijini Mkata, Kata ya Msongozi mkoani Morogoro, anasema ni hali inayopunguza kwa pamoja uhifadhi, hata athari za mabadiliko ya tabianchi.
Katika ujumla wake, tafsiri kuu ni kwamba maeneo yenye mimea na misitu ni muhimu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa usalama wa ardhi kupitia kunyonya vimelea muhimu, pia inadumisha mzunguko sahihi wa maji ardhini.
INAVYOKUWA ENDELEVU
Wajibu mojawapo unatajwa katika ufugaji nyuki, wanaosimamia kufuatilia ustawi wa mazingira yake, wakielimisha jamii ustawi wa afya ya mazingira yake.
Katika namna pekee, wafugaji nyuki wanapopata uelewa wa kina wa uhusiano kati ya nyuki, mimea, na mazingira, wanakuwa mabalozi bora wa uhifadhi.
Ni miradi inayotajwa kuweza kukuza mtazamo wa uhifadhi, hata kuwahamasisha wanajamii kulinda wanyamapori na rasilimali zao za asili.
Programu za elimu zinazohusiana na ufugaji nyuki zinaweza pia kuhusisha shule na vikundi vya vijana na kuunda uelewa kuhusu jukumu la wachavushaji na umuhimu wa matumizi endelevu ya ardhi.
Ufugaji nyuki daima hauishii kuingiza kipato, ni chombo chenye nguvu ya kukuza uhifadhi wa mazingira na kuimarisha maisha ya pamoja, kati ya binadamu na wanyamapori, ikisaidia matumizi endelevu ya ardhi
· Mwandishi, pia ni Mshauri Elekezi katika taasisi inayohusika na mazingira, mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa wanyamapori. Kwa maoni anapatikana kwa baruapepe: [email protected]
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED