MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetangaza vifurishi vipya vya bima katika makundi mawili ya Serengeti Afya na Ngorongoro Afya, kifurushi cha chini kikiwa ni Sh. 240,000 na cha juu Sh. 6,388,400 kwa mwaka.
NHIF imeainisha pia mafao yatakayotolewa kwa kila kifurushi na ukomo wa matumizi ya gharama za matibabu kwa mnufaika kwa mwaka ni Sh. milioni 22 kwa Kifurushi cha Serengeti Afya kwa anayelazwa na kutwa Sh. milioni tatu, huku Kifurushi cha Ngorongoro Afya ni Sh. milioni nane kwa anayelazwa na Sh. milioni mbili kwa asiyelazwa.
Kwa mujibu wa tangazo lililowekwa kwenye tovuti ya NHIF, watoto wa miaka 0-17, mmoja analipa Sh. 240,000 kwa Kifurushi cha Ngorongoro Afya na Sh. 660,000 kwa Kifurushi cha Serengeti Afya.
Umri wa miaka 18-35 mgawanyo ni kwa mtu mmoja; wanandoa; mtu mmoja na mtoto mmoja; mtu mmoja na watoto wawili; mtu mmoja na watoto watatu; mtu mmoja na watoto wanne; wanandoa na mtoto mmoja; wanandoa na watoto wawili; wanandoa na watoto watatu; na wanandoa na watoto wanne.
Gharama kwa kila kundi kwa Kifurushi cha Ngorongoro Afya zinaanzia Sh. 432,000 hadi 1,684,800 huku Serengeti Afya zikiwa ni kuanzia Sh. 792,000 hadi 3,880,800.
Gharama kwa kundi la miaka 36-59 kwa Kifurushi cha Ngorongoro Afya zinaanzia Sh. 540,000 hadi Sh. 1,890,000 huku kwa Kifurushi cha Serengeti Afya zinaanzia Sh. 1,620,000 hadi Sh. 5,454,000.
Gharama kwa umri wa miaka 60 kuendelea kwa Kifurushi cha Ngorongoro Afya ni Sh. 708,000 kwa wanandoa, huku wanandoa na mtoto mmoja ni Sh. 1,345,200. Kifurushi cha Serengeti Afya kwa umri huo kwa wanandoa ni Sh. 3,336,000 na wanandoa na mtoto mmoja ni Sh. 6,336,400.
Mafao yanayotolewa kwa wanachama wa vifurushi vya bima ya afya ikiwa na mafao tofauti kwenye mabano (idadi ya huduma) ambayo ni Kifurushi cha Serengeti Afya; huduma za dawa (907), upasuaji mkubwa na mdogo (565), vipimo vya maabara na uchunguzi (315), vifaa tiba visaidizi (17), ada ya kujiandikisha na kumwona daktari (inapatikana) na huduma za kulazwa (inapatikana).
Kwa Kifurushi cha Ngorongoro Afya; mafao ni kila eneo kwenye mabano ni huduma za dawa (286), upasuaji mkubwa na mdogo (60), vipimo vya maabara na uchunguzi (88), vifaa tiba visaidizi (hakuna), ada ya kujiandikisha na kumwona daktari (inapatikana); na huduma za kulazwa (inapatikana).
Katika tovuti hiyo imeandikwa: “Vifurushi vya Bima ya Afya vya NHIF ni mpango unaowezesha mwananchi mmoja mmoja au familia kuchagua na kuchangia huduma za matibabu kabla ya kuugua na kisha kuwa na uhakika wa matibabu kwa kutumia bima ya afya bila kikwazo."
Ppia kumeainishwa faida za kujiunga na vifurushi vya bima ya afya kwamba ni wigo mpana wa huduma za matibabu za msingi, kubingwa na bingwa bobezi; punguzo la asilimia 10 ya mchango wa mtegemezi kwa wanaojiunga kwa familia.
Faida nyingine ni matibabu nchi nzima katika vituo vya matibabu zaidi ya 10,000 kuanzia ngazi ya zahanati hadi Hospitali ya Taifa, na kwamba utaratibu wa rufani utatumika katika Hospitali za Rufani za Kanda na Taifa.
Taarifa hiyo inataja mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kujiunga na vifurushi vya bima ya afya na kwamba kila mnufaika atakuwa na ukomo wa matumizi ya gharama za huduma kwa mwaka, hivyo wanachama wanashauriwa kufuatilia matumizi yao kwa ukaribu na kuepuka matumizi holela.
Mwanachama atasubiri kwa siku 30 kabla ya kuanza kupata huduma baada ya kukamilisha taratibu za usajili na kulipia; mwanachama atatakiwa kuhuisha uanachama wake ndani ya siku 30 baada ya kufika ukomo wa uanachama wake.
Pia mwanachama atakayeshindwa kuhuisha uanachama wake ndani ya kipindi husika atahesabiwa kama mwanachama mpya na atakuwa na muda wa kusubiria kwa siku 30.
TOTO AFYA
Taarifa kwenye tovuti hiyo inaeleza mafao ya wanufaika wa Toto Afya kwa makundi yanayolipa Sh. 50,400 kuwa ni huduma ya kumwona daktari wa kawaida, bingwa na bingwa mbobezi; huduma za vipimo vya maabara, CT-Scan, MRI, Ultra Sound, X-ray, ECHO na ECO; baadhi ya dawa za magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, selimundu, magonjwa ya moyo na magonjwa ya figo.
Nyingine ni huduma za kulazwa wodi ya kawaida, chumba cha wagonjwa mahututi (ICU na HDU); baadhi ya huduma za upasuaji mkubwa na mdogo wa magonjwa ya tumbo; huduma za kuchuja damu; huduma za saratani; huduma ya kinywa na meno kama kuziba, kung’oa, kusafisha na meno bandia; huduma za mazoezi tiba na mtengamao; huduma za dharura na vifaa tiba pandikizi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED