Morrison aitupia Yanga kijembe

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:57 AM Feb 03 2025
Bernard Morrison
Picha: Mtandao
Bernard Morrison

KUELEKEA mchezo wa keshokutwa kati ya Yanga na KenGold FC, utakaochezwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, winga mpya wa timu hiyo, Bernard Morrison ametupa kijembe kwa timu yake hiyo ya zamani, akisema siku hiyo timu yao itajulikana kwa jina la MC KenGold.

Morrison, ambaye anajulikana kwa vituko na vimbwanga, akiwa ndani na nje ya uwanja, ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii, akisema inaonekana timu yake hiyo ya zamani inahofia timu zenye majina yanayoanzia na MC.

"Jumatano tutabadilisha tu jina letu kuwa 'MC KenGold' ili tupate matokeo mazuri. Kwa sababu inaonekana wanaogopa majina yanayoanza na MC," aliandika Morrison jana mchana, kitu ambacho kinaweza kufanya mchezo huo uwe gumzo na kuvutia mashabiki wengi.

Ikumbukwe kuwa Yanga ilitolewa kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kushindwa kutinga robo fainali baada ya kulazimishwa suluhu dhidi ya MC Alger ya Algeria, katika mchezo wa mwisho wa Kundi A, uliochezwa, Januari 8, mwaka huu, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kabla ya hapo, ilifungwa mabao 2-0 na timu hiyo ikiwa ugenini, Desemba 7, mwaka jana, katika mfululizo wa michezo hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Iwapo atacheza, utakuwa ni mchezo wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu msimu huu akiwa na timu hiyo, tangu alipojiunga nayo dirisha dogo la usajili.

"Mimi nimejiunga KenGold si kwa sababu ya pesa, au nimepata ofa nzuri, mimi nilikuwa majeruhi wa muda mrefu, niliumia wakati nipo FAR Rabat ya Morocco, sasa unapopona si vizuri kwenda kwenye timu kubwa ambazo zina presha na mahitaji makubwa, kwa hiyo nimekuja hapa kama mtu anayeanza upya maisha.

"Kitu muhimu ni kuisaidia KenGold kubaki kwenye ligi, siyo kwamba tumepata ofa nzuri sana," alisema mchezaji huyo raia wa Ghana.

Aliingia nchini akijiunga na Yanga 2020, alipocheza kwa nusu msimu kabla ya kuhamia Simba ambapo alicheza hadi 2022, aliporejea tena Yanga, akihudumu kwa msimu mmoja hadi 2023 na kutimkia FAR Rabat, kwa kuchukuliwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi.