IBRAHIM TRAORÉ; Anayevutia mamilioni ya vijana Afrika

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 10:38 AM Jan 29 2025
Rais Ibrahim Traore wa Burkina Faso.
Picha: MTANDAO
Rais Ibrahim Traore wa Burkina Faso.

MWONEKANO wake na falsafa zake, kiongozi wa serikali ya kijeshi Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, kumemjengea umaarufu si nchini mwake tu bali barani Afrika.

Wakati orodha ya washiriki wa nchi takribani 24 ikitajwa kuwa  washiriki wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliomalizika jana Dar es Salaam, akiwamo Traoré, mitandaoni kijana huyo amejiongezea umaarufu.

Kapteni Traoré (37), Oktoba, mwaka 2022 aliingia madarakani baada ya kufanyika mapinduzi na kuondoshwa ikulu Paul-Henri Sandaogo Damiba. 

Muda mfupi, Traoré alitangaza katika televisheni ya taifa, amempindua madarakani kiongozi huyo wa kijeshi.

Kijana huyo ana falsafa zake ikiwamo kupinga anachodai Waafrika wamerithishwa na utawala wa kikoloni. Wiki chache zilizopita amepiga marufuku majaji wa nchi mwake kuvaa mawigi yenye mtindo wa kikoloni ya Ufaransa na Uingereza.

Vijana wanaojiita kizazi cha Gen Z, huko mitandaoni wanamtaja kama ndiye wamtakaye kulingana na wakati huu. 

Kiongozi huyo amesubiriwa kwa hamu kubwa kushiriki kwenye mkutano huo, Dar es Salaam, lakini hajaonekana.

Mitandaoni wengi wanaeleza nia yao ya kumwoana ana kwa ana, hasa mwonekano wa mavazi yake kijeshi akiwa na silaha yake muda wote.

Hivi karibuni pia anashika kasi mitandaoni baada ya nchi yake kulipa deni la nje lenye thamani ya dola bilioni 4.7 wakati huo huo akichukua udhibiti wa sekta ya madini ya dhahabu yenye faida kubwa nchini Burkina Faso.

Hatua hiyo imeibua hisia nyingi ndani na kimataifa, ikiashiria mabadiliko yanayoweza kutokea katika mtazamo wa Afrika wa uhuru wa kiuchumi na usimamizi wa rasilimali.

Baadhi ya maoni mtandaoni yalikuwa haya @BarakaMboyi anasema: “Mwamba kweli ni mzalendo Mwamba kweli ni mzalendo wa kweli kiukweli tumpe maua yake, viongozi wa Afrika waone mfano kwa Traoré.

HISTORI ILIPOANZA

Kapteni Traoré, Septemba 30, 2022, anamwondosha madarakani Luteni Damiba.

Awali, Damiba, anaanza kumwondoa Rais Roch Marc Chrisitian Kabore, aliyeingia kwa kupindua pia.

Kapteni Traore, anaeleza sababu ya kuidhinisha mapinduzi hayo, ni kutokana na kushindwa kwa Luteni Damiba, kukabiliana na waasi.

Mbali na viongozi wa kijeshi, vipo  vikosi vya wanamgambo, viongozi wa kimila na kidini, wakuu wa taasisi na wageni maalum wa rais wa mpito.

Mbele ya wajumbe wa Baraza la Katiba, Kapteni Ibrahim Traoré anainua mkono wake wa kulia na kuapa kwa heshima yake kuhifadhi, kuheshimu, kuheshimisha na kutetea katiba, makubaliano ya mpito na sheria.

 Kufanya kila linalowezekana kuhakikisha haki kwa wakazi wote wa Burkina Faso.

USALAMA KWANZA

'Nitapigana hadi pumzi ya mwisho', anasema akihutubia wananchi wake bila kutumia karatasi zenye maandishi.

"Hakuna hasara kubwa itakayotokea kwa kuiondoa Burkina Faso katika hali hii. Dira yetu itakuwa watu daima. Kwa taifa langu, nitapigana hadi pumzi ya mwisho,” anasema baada ya kula kiapo.

Anajitokeza sana katika vita dhidi ya waasi nchini Burkina Faso alikozaliwa kati ya 2019 na 2022. Alipandishwa cheo hadi kapteni mwaka wa 2020.

Muda mfupi baada ya kufanya mapinduzi dhidi ya utawala wa Damiba, Septemba 2022, Traore alikiri kwamba umri wake wa miaka  34 (wakati huo),  ungekuwa mada ya mjadala kati ya wale wanaotilia shaka sifa zake za urais.

“Najua kwamba ni mdogo kuliko wengi wenu hapa. Hatukutaka kilichotokea (mapinduzi dhidi ya Damiba), lakini hatukuwa na chaguo," aliwaambia maaofisa wa serikali Oktoba 2022.

MAVAZI

Rais huyu huvaa mavazi ya kijeshi katika maonesho mengi ya umma.

Marais wenzake ambao mara nyingi huvalia suti zao za bei ghali, Traoré, mrefu zaidi huwa katika mwonekano wa kijeshi.

Akiwa na urefu wa zaidi ya futi sita, huvaa bareti nyekundu na glavu za kijivu.

Katika uongozi wa kijeshi, Traore yuko katika cheo cha Captain, ni neno la Kifaransa. Kuna safu tatu juu ya ile ya kapteni, nao ni Luteni na Kanali.

Kwa kuwa koloni la zamani la Ufaransa, Burkina Faso ilipitisha muundo wa amri ya kijeshi ya Ufaransa.

Baada ya kuhudumu katika nyadhifa za chini katika jeshi la Burkina Faso, hatua kubwa ya Traoré ilikuja mwaka 2014, alipotumwa Mali kama mwanajeshi chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, MINUSMA.

Akiwa na umri wa miaka 26 wakati huo, Traoré alishinda "shambulio tata" la wanamgambo wenye itikadi kali katika eneo la kaskazini la Timbuktu, chanzo ambacho hakikutajwa jina kiliiambia Radio Omega.

“Tatizo ni kuona wakuu wa nchi za Kiafrika, ambao hawaleti chochote kwa watu wanaohangaika, wakiimba wimbo sawa na mabeberu wanaotuita ‘wanamgambo’. Matokeo yake, wanaishia kututaja sisi kuwa watu wasioheshimu haki za binadamu,” Traoré alisema.

"Sisi, wakuu wa nchi za Kiafrika, lazima tuache kutenda kama marimoti ambao wanacheza kila wakati mabeberu wanapovuta kamba zetu."

Alikwenda mbele kuwakashifu marais wa Afrika ambao "wanafurahi kupokea vitu na misaada ya bure."

BBC, DW, MITANDAO