MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga, juzi walishindwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya kimataifa kwa mara ya tatu mfululizo.
Ni baada ya kulazimishwa suluhu dhidi ya MC Alger kutoka nchini Algeria na kuhitimisha safari yao msimu huu iliyoishia kwenye Kundi A Ligi ya Mabingwa Afrika.
Msimu wa 2022/23, Yanga ilifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho na kuvuka hadi fainali, ikaukosa ubingwa kwa USMA Alger ya Algeria kwa tofauti ya bao la ugenini.
Ilifungwa mabao 2-1 nyumbani na kwenda kushinda bao 1-0 ugenini, hivyo matokeo ya jumla yakawa 2-2, Waalgeria wakanufaika na bao walilofunga, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Msimu uliopita ilifanikiwa pia kufika hatua ya robo fainali, Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa penalti 4-3, Aprili 5, mwaka jana, mechi iliyochezwa Sauzi, baada ya suluhu ya mechi zote mbili, ya kwanza ikichezwa Machi 30, mwaka jana, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Juzi, ilitaka kufanya hivyo kwa mara ya tatu kwenye mechi za kimataifa na mara ya pili, Ligi ya Mabingwa, ikihitaji ushindi wa aina yoyote, lakini ilishindwa kufanya hivyo mbele ya mashabiki wao, huku wapinzani wao wakihitaji ushindi au sare ambayo waliipata.
Matokeo hayo yameifanya MC Alger kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifikisha pointi tisa, ikimaliza mechi sita za Kundi A, ikiwa nafasi ya pili na kuiacha Yanga ikimaliza nafasi ya tatu, ikiwa na pointi nane.
Vinara wa kundi hilo ambao walifuzu mapema ni Al Hilal Omduraman ya Sudan, iliyomaliza ikiwa na na pointi 10, juzi ikipokea kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, mechi iliyochezwa Uwanja wa Mazembe.
Katika makala haya, tunakuletea takwimu zote za mechi ya juzi, pamoja na msimamo wa kundi kwa mtindo wa namba, twende sasa...
539# Yanga ilipiga idadi hii ya pasi, zikiwa ni nyingi zaidi dhidi ya wapinzani wao katika mchezo wa juzi.
260# Hizi ni pasi zilizopigwa na wapinzani wa Yanga, MC Alger katika mchezo wa juzi uliomalizika kwa suluhu.
84# Ni pasi za Yanga zilizopigwa kwa usahihi zaidi katika mchezo wa raundi ya sita, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger, ikiwa pia imeongoza kwa kufanya hivyo.
69# Yanga ilimiliki mpira mara idadi hii katika mchezo wa juzi, ikiongoza kwa umiliki zaidi kuliko wapinzani wao.
66# Namba hii inasimama kama pasi za usahihi zilizopigwa na MC Alger katika mchezo huo wa mwisho wa Kundi A.
31# MC Alger ilimiliki mpira mara namba hii, ikiwa ni kiwango cha chini kuliko wenyeji wao Yanga, licha ya matokeo kuwa suluhu, kwani walionekana kucheza zaidi nyuma ya mpira.
19# Ni idadi ya faulo zilizopigwa na Yanga katika mchezo husika, ikiwa ni timu iliyopata faulo nyingi kuliko wapinzani wao.
18# Haya ndiyo mashuti ya jumla yaliyopigwa na Yanga katika mchezo wa juzi katika kile ambacho wachezaji wa timu hiyo walikuwa wakitafuta angalau bao moja ili kuweza kufuzu.
14# Hizi ni faulo ambazo MC Alger walifanikiwa kuzipata kwenye mchezo wa juzi, pungufu ya faulo sita ambazo wenyeji wao walizipata. Namba hii pia inasimama kama idadi ya kona ambazo Yanga imezipata katika mchezo huo.
10# Ni muda ambao mechi kati ya timu hizo mbili ulianza kwa saa za Afrika Mashariki na kumalizika saa 12 na ushehe hivi jioni.
9# Idadi ya pointi zilizoifanya MC Alger kushika nafasi ya pili na kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka Kundi A.
8# Pointi ambazo Yanga imekusanya hadi mwisho wa mchezo wake wa Kundi A, ambazo bado hazikuiwezesha kutinga hatua ya robo fainali.
6# Idadi ya michezo ambayo timu zote zimecheza kwenye Kundi A, ambazo zimeziwezesha timu ya Al Hilal Omdurman ya Sudan na MC Alger kufuzu hatua ya robo fainali.
3# Yanga ilipiga idadi hii ya mashuti kwenye lango la wapinzani wao ambayo yalilenga lango. Pia ni idadi ya kadi za njano zilizotolewa kwenye mchezo wa juzi ambazo zote zilielekezwa kwa timu moja tu, MC Alger, huku Yanga ikiwa haijapata kadi yoyote. Namba hii pia inasimama kama ni idadi ya mashuti yaliyopigwa na MC Alger katika mchezo huo.
2# Timu zote mbili ziliotea mara idadi hii katika mchezo wa juzi, ambao hata hivyo, Yanga ndiyo ilitawala zaidi kuliko wapinzani wao ambao walitumia muda mwingi kukaa nyuma ya mpira na kushambulia kwa kushtukiza.
1# Ni idadi ya kona ambayo MC Alger ilipata, pamoja na shuti lao pekee lililolenga langoni kwa Yanga katika mchezo huo.
0# Hakukuwa na kadi ya njano wala nyekundu kwa Yanga, pia hakukuwa na kadi yoyote nyekundu kwa wageni MC Alger na hapakupatikana bao kwa timu yoyote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED