Ndolezi autaka ubunge Kigoma Kusini

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 01:33 PM Jan 20 2025
Waziri Kivuli wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Bunge, Sera, Vijana, Kazi na Ajira wa chama hicho, Mhandisi Petro Ndolezi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Kivuli wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Bunge, Sera, Vijana, Kazi na Ajira wa chama hicho, Mhandisi Petro Ndolezi.

SIKU chache baada ya Chama cha ACT Wazalendo kufungua pazia kwa wanachama wake kutangaza nia ya kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, Waziri Kivuli wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Bunge, Sera, Vijana, Kazi na Ajira wa chama hicho, Mhandisi Petro Ndolezi, ametangaza rasmi nia ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Kusini.

Mhandisi Ndolezi alitangaza nia hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Kijiji cha Nguruka, Kata ya Nguruka, jimbo la Kigoma Kusini. Akiwahutubia wananchi, alieleza kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili wakazi wa jimbo hilo.

“Jimbo la Kigoma Kusini linakabiliwa na changamoto kubwa katika sekta ya miundombinu ya barabara, ukosefu wa pembejeo za kilimo, migogoro ya ardhi, na huduma duni za afya. Nitatoa maelezo ya kina kuhusu mipango yangu wakati wa kampeni endapo nitapata ridhaa ya kugombea,” alisema Mhandisi Ndolezi.

Aidha, alibainisha kuwa amekuwa mstari wa mbele kutetea ajenda za vijana kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Baraza la Taifa la Vijana. Aliweka mkazo katika kujenga uchumi wenye uwezo wa kuzalisha ajira nyingi kwa lengo la kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana. Pia alisisitiza umuhimu wa kuwepo mifuko ya hifadhi ya jamii jumuishi inayowahusisha wote, na sio tu wale walio katika sekta rasmi, ambao kwa Tanzania ni asilimia 9 ya nguvu kazi ya taifa, huku asilimia 91 wakibaki nje ya mifumo hiyo.

Chama cha ACT Wazalendo kilifungua rasmi milango ya watia nia ya kugombea nafasi za urais, ubunge, na udiwani kupitia tamko lililotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, Januari 15 mwaka huu. Tangu pazia hilo lifunguliwe, kwa nafasi ya urais, waliokwisha tangaza nia upande wa Tanzania Bara ni Kiongozi wa Chama Dorothy Semu, na upande wa Zanzibar ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman.