Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia mtu mmoja anayetuhumiwa kusambaza picha za mjongeo zenye maudhui machafu, ambazo zimeunganishwa na majengo ya Shule ya Sekondari ya Baobab, hali iliyosababisha taharuki miongoni mwa wazazi na wafanyakazi wa shule hiyo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, picha hizo zilisambazwa kuanzia Desemba 31, 2024, na zilionyesha wasichana wakiwa na nywele za bandia, tofauti na wanafunzi wa shule hiyo ambao hufuata utaratibu wa kusuka nywele za asili kwa mtindo wa "Twende Kilioni."
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Morcase ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa tuhuma za kutengeneza na kusambaza picha hizo kwa nia ya kuaminisha umma kuwa vitendo hivyo vinafanywa na wanafunzi wa shule hiyo.
“Jeshi la Polisi lilipokea taarifa rasmi kutoka kwa uongozi wa shule ya Baobab mnamo Januari 3, 2025, na tumeanza kuchukua hatua za kuwafuatilia na kuwasaka watu wengine waliohusika,” amesema Kamanda Morcase.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Shajar, inayomiliki shule hiyo, Shani Swai, amesema picha hizo ziliibua hofu kubwa kwa wazazi na wafanyakazi wa shule. "Kutokana na ukosefu wa utaalamu wa kuchunguza picha hizo, tuliamua kuwasilisha suala hili kwa Jeshi la Polisi ili wachukue hatua stahiki," amesema Swai.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taaluma ya shule hiyo, Mhandisi Fredy Ntevi, amebainisha kuwa picha hizo zilionyesha wasichana wakiwa wamesuka nywele za bandia, jambo ambalo halilingani na utaratibu wa shule hiyo, ambapo wanafunzi wote hufuata mtindo wa nywele wa asili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED