SERIKALI ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zimeanika namna zilivyotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025, huku maboresho ya bandari na safari za treni ya mwendokasi (SGR) yakitajwa kuleta mageuzi ya kiuchumi.
Katika taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Desemba 2024 iliyowasilishwa kwenye Mkutano Mkuu maalumu wa CCM jana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ilielezwa kuwa tangu kuzinduliwa safari za treni ya SGR Dodoma hadi Dar es Salaam Agosti 2024 hadi Desemba 11, 2024, zaidi ya abiria 1,200,000 wamesafiri na kuingiza mapato ya Sh. bilioni 30.
Akizungumzia kuhusu maboresho ya uendeshaji huduma za Bandari ya Dar es Salaam, Majaliwa alisema kuwa Mei 2024 hadi Novemba 2024, serikali imekusanya Sh. bilioni 62.44 kama tozo ya pango na mrabaha.
Alisema makusanyo hayo hayajumuishi tozo za huduma nyingine ambazo zinaendelea kutolewa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ikiwamo huduma kwa meli na tozo ya matumizi ya miundombinu ambazo kwa pamoja ni Sh. bilioni 451.39 kwa kipindi hicho.
Majaliwa alisema kuwa mafanikio hayo yamechagizwa na uwekezaji uliofanywa katika mitambo ya kisasa na kutumia mifumo iliyoboreshwa ya TEHAMA kuhudumia shehena ya makasha.
Alisema tani milioni 5.022 ambayo ni zaidi kwa asilimia 15 ya shehena zimehudumiwa kulinganishwa na tani milioni 4.375 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita.
"Idadi ya makasha iliyohudumiwa na DP World katika kipindi cha Mei, 2024 hadi Novemba, 2024 ilifikia makasha ya futi ishirini (TEUs) 139,719 sawa na ongezeko la asilimia 44 ya makasha (TEUs) 96,854 yaliyohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita," alisema.
Majaliwa alisema kuwa wastani wa muda wa meli kusubiri kushusha mzigo umepungua hadi kufikia siku saba kwa kipindi cha Mei, 2024 hadi Novemba, 2024 kulinganishwa na wastani wa siku 46 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita (Mei, 2023 hadi Novemba 2023).
Alisema kwa upande wa meli za makasha, hadi kufikia Oktoba 2024, DP World imefanikiwa kuondoa kabisa muda wa meli kusubiri kuingia bandarini na pindi zinapowasili katika Bandari ya Dar es Salaam huenda moja kwa moja gatini.
Alisema gharama za matumizi kwa Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa wastani wa asilimia 47.
Alifafanua kuwa awali matumizi yalikuwa wastani wa Sh. bilioni 34.52 kwa mwezi katika kipindi cha Mei, 2023 hadi Novemba, 2023 ambayo yamepungua hadi wastani wa Sh. bilioni 17.93 kwa mwezi katika kipindi cha Mei, 2024 hadi Novemba 2024.
MAJI, ELIMU
Majaliwa alisema miradi 1,633 ya maji imetekelezwa, ikiwamo 1,335 ya vijijini na 298 ya mijini na kuongeza upatikanaji maji vijijini kutoka asilimia 70.1 hadi asilimia 79.6 na mijini kutoka asilimia 84 hadi asilimia 90.
Waziri Mkuu alisema bajeti ya elimu bila ada imeongezeka kutoka Sh. bilioni 312.5 mwaka 2020 hadi Sh. bilioni 796.38 mwaka 2024 na wanafunzi wanaonufaika wameongezeka kutoka 14,940,925 mwaka 2020 hadi 16,155,281 mwaka 2024.
Alisema miundombinu ya shule za msingi na sekondari pia imeboreshwa na idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 16,656 mwaka 2020 hadi 19,783 mwaka 2024.
Vilevile, alisema shule 26 za sekondari za wasichana za kidato cha tano na sita zimejengwa katika mikoa 26, ili kuhakikisha wanafunzi wa kike wanapata elimu bora.
AFYA, UTALII
Majaliwa alisema sekta ya afya imeimarishwa kupitia ujenzi wa vituo vipya na kuboresha huduma, huku miundombinu na upatikanaji vifaa tiba, vikipewa kipaumbele.
Alisema vituo vipya vya kutolea huduma za afya 183 vimejengwa, vikiwamo vyenye uwezo wa huduma za dharura za uzazi. Idadi ya vitanda vya hospitali imeongezeka hadi 126,209, ikiwa ni uwiano wa vitanda 2.1 kwa kila watu 1,000 karibu sawa na viwango vya Shirika la Afya Duniani.
Majaliwa alisema idadi ya watalii imeongezeka kutoka 620,867 mwaka 2020 hadi watalii 1,924,240 Novemba, 2024. Vilevile, mapato yatokanayo na shughuli za utalii yameongezeka kutoka dola za Marekani milioni 700 mwaka 2020 hadi dola za Marekani bilioni 3.3 mwaka 2024.
Akizungumzia utekelezaji ilani hiyo kwa upande wa Zanzibar, Makamu wa Pili wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alisema maelekezo sita yaliyotolewa na CCM kwa Serikali ya Zanzibar yametekelezwa.
Alisema shule 114 za msingi na sekondari zimejengwa mijini na vijijini na kwamba kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutoka asilimia 55.4 kwa mwaka 2020 hadi asilimia 85.6 kwa mwaka 2023 kwa wanafunzi wa kidato cha nne huku cha sita ufaulu ukifikia asilimia 99.9.
Makamu wa Rais alibainisha kuwa katika sekta ya afya, ujenzi wa hospitali 10 za wilaya umekamilika na huduma za kibingwa zinapatikana Unguja na Pemba.
Alisema upatikanaji maji umefikia asilimia 88.22, visima 102 vimechimbwa, vijiji 222 vimefikiwa na umeme sawa na zaidi ya asilimia 72.
Pia alisema mchango wa utalii kwenye pato la taifa umefikia asilimia 30 na idadi ya watalii imeongezeka na kufikia 736,755 sawa na asilimia 183 kwa mwaka 2024 na mafanikio yamefikiwa kutokana na filamu ya ‘Royal Tour’, huku miradi ya utalii ikifikia 1,695.
Makamu wa Rais alisema masoko makubwa yamejengwa na vituo zaidi ya 14 vya wajasiriamali, kiwanda cha kuchakata mwani tani 30,000 kimejengwa na kitakuwa ni kikubwa kwa Afrika, kikitarajiwa kuzalisha ajira 25,000 rasmi na zisizo rasmi 66,000.
Pia alisema visiwa 21 vimetangazwa kwa ajili ya uwekezaji na tayari 15 vimepata wawekezaji, miradi 424 imeanzisha ajira rasmi zaidi 22,382 na zisizo rasmi zaidi ya 100,000.
Alisema pensheni jamii kwa wazee waliofikisha miaka 70 wanalipwa Sh. 50,000 kila mwezi na kwa wastaafu imefikia Sh. 180,000.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED