Utapeli unavyowaliza watu Mlimani City

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 12:00 PM Jan 20 2025
Fedha.
Picha: Mtandao
Fedha.

JANUARI 14 mwaka huu ilikuwa mbaya kwa Christina (jina la pili limehifadhiwa) baada ya kutapeliwa Sh. milioni tisa na aliowaita wauzaji madini feki, akiwa eneo la Mlimani City, mkoani Dar es Salaam.

Akisimulia namna alivyotapeliwa, Christina anasema kuwa siku hiyo alitoka kazini kwake, akaenda kununua mahitaji ya familia eneo la maduka ya Mlimani City, akakumbana na baa hilo ambalo limemsababisha kupoteza fedha hizo.

"Nilipomaliza kununua mahitaji, wakati ninatoka nje nikiwa pale maeneo yanakopaki magari ya wateja, akatokea mama mmoja amejifunga kanga, akiwa anaonekana kama amebeba kitu hivi.

"Akanisalimia akaniambia 'samahani dada nimetoka humo ndani, nilikuwa ninauliza wapi ninaweza kwenda kuuza madini yangu, lakini wamenielekeza kwamba ni huku nje nivuke barabara, ninaomba kama unapajua unielekeze'.

"Nikamwambia sipafahamu, wakati tuko kwenye mazungumzo hayo, akatokea kijana mmoja hivi amevaa suti akaniambia 'huyu mama ana madini halafu anazurura nayo msaidie mwanamke mwenzio asije akatapeliwa, mpeleke pale karibu na Kanisa la Kakobe, kuna dada anahusika na biashara hizo, utaona kuna hospitali imeandikwa Edward'", anasimuliaa huku akibubujikwa machozi.

Christina anasimulia baada ya kuelezwa maneno hayo, aliingiwa na huruma na kuamini moja kwa moja mama huyo anahitaji msaada, ikabidi ampeleke.

"Kwahiyo tukaongozana mpaka tukafika pale na kilichonifanya niendelee kubaki pale hata sielewi ni kitu gani, kabla ya kuondoka pale Mlimani City yule mama  alimshukuru yule kijana akamwambia akifanikiwa kuyauza yale madini atatugawia Sh. 2,000,000 mimi na yule kijana.

"Yule kijana akasema 'hapana, utatupatia tu Sh. 500,000 ila ya kwangu utaiacha hapo mnapokwenda. Huyu anayekusindikiza (Christina) utampa mkononi kesho kwa sababu ameacha mambo yake kwa ajili ya jambo lako'," anasimulia Christina.

Anasema kabla ya kuondoka Mlimani City, kijana huyo akawa amepiga simu kwa huyo dada atakayewapokea na yule mama mwenye madini akaomba ile namba kisha akampigia kumwambia 'tunakuja akamjibu mkifika hapo, mnisubiri kidogo ninatokea benki'.

"Tukafika karibu na hiyo hospitali tukasubiri kidogo huyo dada akaja akatupeleka moja kwa moja kwenye gari lake akasema huko ndiko kuna kifaa cha kupima hayo madini.

"Tukaingia mimi nikawa nimekaa siti ya mbele yule mama akawa amekaa nyuma, gari lile vioo vyake mtu wa nje hawezi kuona kinachoendelea ndani, akatoa kitu kama kipimajoto, akasema hicho ndicho kinapima madini ikiwaka rangi ya kijani ujue yapo vizuri na ikiwaka nyekundu ujue feki," anasimulia.

Anasema baada ya hapo, akamwambia yule mama ampatie hayo madini ili ayapime kwanza kuona kama yapo sawa, alipompatia akayapima ikawaka taa ya kijani akasema yako vizuri.

Anasimulia baada ya kuyapima akapiga simu kwa mtu aliyemwita kwa jina la Fadher, akaweka sauti ya juu akamweleza kwamba madini ameyaona na ameyapima yako vizuri, akamjibu 'huyo mama tutampa Sh. milioni 200'.

"Baada ya kuongea na huyo Fadher kwa simu akamwuliza yule mama kama ana akaunti ya benki, akamwambia hana. Akaniuliza mimi nikamwambia ninayo, yaani hata sijui nilikuwa nimepumbazwa na nini na sijui ilikuwaje nikakubali.

"Akaniuliza 'ina shilingi ngapi?' Nikamwambia ina Sh. milioni 10. Akaniambia 'hizo fedha ni nyingi kwa sababu tukiongeza na hizo Sh. milioni 150 itaonekana wewe ni mwizi kwa sababu itakuwa imeingia fedha nyingi kwenye akaunti yako.

Kwahiyo chakufanya toa milioni tisa ibaki moja kwenye akaunti yako, ili tuweze kukuingizia hizo fedha halafu Sh. milioni 50 utaibeba tu kwenye pochi'.

Ikabidi nikubali wala sikushtuka kwa lolote! Nikawaambia twende benki Mlimani City ndani nikatoe wakasema twende kwa wakala kule huwa kunakuwa na foleni nikakubali tukaenda kwa wakala wa kwanza tukafanikiwa kutoa Sh. milioni mbili tukaenda kwa wakala wa pili tukatoa Sh. milioni saba tukaziweka kwenye pochi," anasimulia. 

Anasema kuwa baada ya kutoa wakarudi katika gari wakamwambia ampatie zile fedha yule mama (muuzaji madini) halafu waongozane kwenda benki ndani Mlimani City, ili akakutane na ‘Fadher’ ili wamwingizie hiyo fedha katika akaunti yake.

"Kwahiyo tukatoka mimi na huyo dada tukamwacha huyo mama katika gari peke yake, nikiwa nimeshamkabidhi kiasi hicho cha fedha, tukawa tunakwenda benki kwa ajili ya kukamilisha huo muamala, tulipoingia katika jengo hilo karibu na wanapouza piza, yule dada akaniuliza 'umekumbuka kuchukua yale madini kwa yule mama ili tumwoneshe Fadher alipe hizo fedha?'

"Nikamwambia "hapana!" Akasema 'nenda kayachukue' nikamwambia 'twende pamoja', akasema 'nenda tu usijali', tukabishana kwa muda, lakini baadaye nikakubali kurudi peke yangu.

“Looh nimefika pale lile gari sijalikuta, nikakimbia kurudi Mlimani City ndani huyo dada sikumkuta tangu hapo sijawaona tena, ndivyo nilivyotapeliwa, nilipumbazwa! 

"Sikukumbuka hata kutizama namba ya gari wala hatukubadilishana namba za simu, basi baada ya hapo nikaenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi nikapewa RB," anahitimisha simulizi yake.

MASHUHUDA

Miongoni mwa wateja wanaokwenda kupata huduma katika eneo hilo, Jamali Nyanganane anasema tukio hilo si la kwanza kutokea eneo hilo.

"Ukiangalia hilo eneo la Mlimani City kuna huduma nyingi za kijamii zikiwamo za kibenki, ni eneo ambalo lina kila aina ya utapeli.

"Ni kama wiki tu imepita, alitokea mama mmoja amepewa dola feki, na aliyemtapeli kwa kujifanya alikuwa anafanya kazi za ndani kwa mchina amelipwa dola hivyo anaomba ampe fedha kidogo ili ampatie zile dola.

"Yule dada alijifanya hawezi kubadili zile fedha, kwa maelezo yake siku hiyo zilikuwa na thamani ya Sh. milioni tatu yeye aliambiwa ampe Sh. milioni  1.5

"Na yeye bila kuwaza alikubali akiamini atakapokwenda kuzibadili atakuwa na faida kubwa alipofika benki akaambiwa dola zote alizokuwa nazo ni feki," anasimulia Nyanganane.

Anashauri kamera za ulinzi katika eneo hilo ziongezwe ili linapotokea tukio kama hilo na mengine iwe rahisi kufuatilia kumkamata mtuhumiwa.

"Wanaotapeli wanakuwa hawajavaa kitu chochote cha kuficha sura, hivyo kamera katika eneo lile ziongezwe, ninadhani hiyo itasaidia kuwakamata wanaojihusisha na vitendo hivyo.    

KAULI YA POLISI

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro anathibitisha kuwapo matukio hayo, akieleza kuwa kwa sasa yamepunguza kulinganisha na kipindi cha nyuma. Wengi wanatapeliwa kwa sababu ya tamaa.

"Tumekuwa tunatoa elimu mara kwa mara, lakini watu si wasikivu, ukiona unashawishiwa kupata fedha nyingi kwa mara moja, shtuka! Huo ni mtego.

"Tumetoa elimu na elimu kuanzia kwa wale wa 'tuma kwenye namba hii', wanaofanya hivyo kwa kutumia njia ya madini, na mambo ya dola kwenye mitandaoni huko tumeshaelimisha sana," anasema Kamanda Muliro.

Anasema watu wengi huwa wanaingia katika mtego huo, wakidhani watapata zaidi, mwisho wa siku wanaishia kutapeliwa.

Anasema wengi wanaofanya utapeli wa namna hiyo, huwa wanakuwa zaidi ya wanne na wote wanakuwa lao moja japo kwa namna wanavyoigiza unaweza kudhani kama si watu wanaofahamiana.

Kamanda Muliro anashauri watu wanapokutana na hali hiyo, wajaribu kuwaza zaidi ya mara mbili, hata kwa kutumia hesabu za kufikiria, akihadharisha "ukiona mtu anakuletea dili mezani ambalo linakupa faida kubwa kwa mara moja, jua hapo unatapeliwa".

Anasema wapo wengi waliokamatwa na kufikishwa katika vyombo vingine vya sheria ikiwamo mahakamani, huku akionya wanaotapeli watu kuacha kwa kuwa ni kinyume cha sheria na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.