Ripoti: Huduma za intaneti nyumbani, ofisini zaimarika

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:18 PM Jan 20 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanznaia, Dk. Jabiri Bakari.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanznaia, Dk. Jabiri Bakari.

HUDUMA za intaneti kupitia waya za faiba zilizounganishwa majumbani na ofisini na kasi yake zinazidi kuongezeka nchini, hali inayoashiria mwelekeo mpya wa utumiaji teknolojia zinazojumuisha watu wengi.

Hayo yanabainishwa katika Ripoti ya Hali ya Mawasiliano Tanzania ya Desemba 2024 iliyotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanznaia, Dk. Jabiri Bakari. 

Alisema ingawa teknolojia za faiba nyumbani (FTTH) na ofisini (FTTO) hazijaenea sana nchini, zina kasi karibu mara tatu ya teknolojia za simu za vifaa vya mkononi.

"Kasi ya teknolojia zinazowezesha intaneti inapitia kipimo cha megabaiti kwa sekunde (Mbps)," ilifafanua ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, laini 48,028,227 zilitumika kwa huduma za intaneti Desemba 2024, huku laini za FTHH zilikuwa 71,660 na FTTO 11,540 na zilizobakia zilitumia njia ya simu za mkononi. FTTO zina idadi ndogo ya laini 71,661 na 11,540 mtawalia.

"Huduma ya intaneti zinatolewa kupitia laini za simu, waya (faiba) na mawimbi. Idadi ya utumiaji intaneti inatokana na laini/waya ambazo zimetumia huduma ya intaneti angalau mara moja katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita bila kujali teknolojia iliyotumika," mkurugenzi huyo alisema.

Mkurugenzi huyo alisema idadi ya utumiaji wa intaneti imeongezeka kwa asilimia 16 kutoka milioni 41.4 kwa robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2024 hadi milioni 48 kwa robo ya mwaka iliyoishia Disemba 2024. 

"Simu 56,862,95 za kawaida au simu rununu na 23,419,299 zenye uwezo mkubwa, maarufu simu janja zilitumika mitandaoni Desemba 2024.

"Kasi ya kupakua data kwa teknolojia ya vifaa vya mkononi ilikuwa Mbps 10.8, wakati kwa teknolojia ya FTTH ilikuwa 31.8 Desemba 2024. Ilikuwa 13.2 na 40,9 mtawalia Septemba mwaka jana," inafafanuliwa katika ripoti hiyo.

Alisema hadi Desemba 2024 huduma za FTTH na FTTO zilitolewa na kampuni 48 zilizo na leseni ya TCRA ya programu tumizi za mawasiliano.

"Usajili wa intaneti ya waya wa faiba unajumuisha usajili wa mtu binafsi na wa taasisi. Teknolojia ya FTTH inawezesha watu wengi zaidi kwenye eneo ilipofungwa kupata huduma kwa mtandao unaowezesha watu wengi kujiunga na chombo kimoja kilichounganishwa," alisema.

Vilevile, inatoa fursa ya watumiaji kupata huduma nyingi zaidi zikiwamo filamu na burudani nyingine wakiwa majumbani.

"Wastani wa matumizi kupitia laini hizo ilikuwa ni gigabaiti (Gb) 4.49 kwa laini, ikiwa ni juu ya Gb 4.35 Septemba, uchambuzi wa ripoti umethibitisha," alisema.

Alisema pamoja na laini zinazotumia intaneti kuongezeka kutoka 46,084,364 Oktoba hadi 48,028,227 Desemba 2024, ripoti hiyo inasema watumiaji intaneti wanatumia asilimia 10.9 ya uwezo wa kuunganisha huduma ya intaneti kwenda nje ya Tanzania na kuingia nchini.

"Tanzania ina uwezo wa Gigabaiti kwa sekunde (Gbps) 17,200.00 kwa ajili ya uunganishaji huduma ya Intaneti ambako 1,868.32 tu ndizo zilitumika Desemba 2024. Kuna 15,331.68 zinazosubiri kuunganishwa," alisema.

Wakati huo vikoa viivyosajiliwa kwa jina la Tanzania, yaani vyenye dot tz vimeongezeka hadi 32,267 Desemba 2024 kutoka 31,584 mwishoni mwa Septemba 2024.