Mwanamke mmoja mkazi wa Mtaa wa Nguzo-Forest, Kata ya Boma, Manispaa ya Morogoro, amezua sintofahamu baada ya kuzuia mwili wa binti yake, Irene Joseph Akaro (30), kufanyiwa taratibu za mazishi kwa Imani kuwa hajafa na ataweza kufufuka ikiwa mwili wake utaombewa katika makanisa ya Kipentekoste, hususan Kanisa la Ufufuo na Uzima.
Hali hiyo imeibua mvutano wa kifamilia kati ya mama wa marehemu na baba wa marehemu. Upande wa baba, ambao wote wanaishi nyumba moja, umesisitiza kwamba mwili wa Irene ufanyiwe taratibu za Kikristo kwa mujibu wa imani ya Katoliki, ambapo ungetolewa heshima za mwisho kabla ya kusafirishwa kwenda Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
Mama wa marehemu, ambaye jina lake halikupatikana mara moja, amekataa mwili wa binti yake kuhifadhiwa au kufanyiwa ibada ya mazishi ya kawaida, akidai kuwa mwili unapaswa kupelekwa kanisani kwa maombi ya kufufuliwa. Akizungumza huku akidhibitiwa na ndugu waliokuwa wakipinga suala hilo kujadiliwa hadharani, mama huyo amesema: “Hii ni imani yangu. Wanipashe ruhusa nimpeleke mwanangu kanisani akaombewe. Najua hajafa, na naamini baada ya maombi ataamka.”
Viongozi wa Kanisa Katoliki waliokuwepo eneo hilo wameonya kuwa ikiwa mwili wa marehemu utapelekwa kwenye makanisa ya Kipentekoste, wao hawatashiriki tena kwenye taratibu za maziko. Hali hiyo iliwahuzunisha wanafamilia upande wa baba, ambao waliona kufanya hivyo ni kwenda kinyume na imani yao.
Askofu Mkuu Willy Mpala wa Kanisa la The Light of Christ Mobile Church, madhehebu ya Kipentekoste, amesema kuwa makanisa yao yanaamini katika maombi na ufufuo, na inawezekana mama wa marehemu alipewa ufunuo kuwa binti yake akipelekwa kanisani ataweza kufufuka.
“Sisi hatuamini sana katika ibada za maziko, bali tunaamini katika maombi na Ufufuo. Huyu binti alizaliwa katika imani ya Katoliki, akaja Kipentekoste, lakini alirudi tena Katoliki kabla ya kufariki. Hata hivyo, mama yake ana haki ya kushikilia imani yake,” amesema Askofu Mpala.
Miongoni mwa majirani waliokuwa wakishuhudia mvutano huo, Mbaraka Ahumani amesema: “Kila mtu anakufa. Huyu marehemu amekufa, na ndugu wanapaswa kuukubali ukweli huo. Ninashauri azikwe Morogoro ili watu wengi waliomjua waweze kushiriki.”
Marehemu Irene alijulikana kwa kushiriki biashara ndogo ndogo, kama vile uuzaji wa viatu katika eneo la Luna, Manispaa ya Morogoro.
Hadi mwandishi anaondoka eneo la tukio, familia haijafikia muafaka wa jinsi mwili wa marehemu Irene utashughulikiwa. Mazungumzo ya kifamilia yalikuwa yakiendelea, huku upande wa mama ukishikilia msimamo wa maombi ya kufufua, na upande wa baba ukitaka mazishi yafanyike kwa mujibu wa imani ya Katoliki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED