SIKU chache zilizopita, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewaonya wanaotumia fedha za kigeni, kufanya miamala nchini, ikisisitiza kufanya hivyo ni kuhujumu uchumi wa nchi na ni kosa kisheria.
Ikaongeza kuwa, Kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha, kimeamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia sita kwa benki za kawaida katika robo ya kwanza ya mwaka 2025.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, anasema mtu anapofanya miamala ndani ya nchi, anatakiwa kutumia shilingi za kitanzania,vinginevyo yuko kinyume akihujumu uchumi wa nchi, kwa sababu anatumia shughuli za uchumi wa Tanzania kwa kutumia sarafu za nchi nyinginezo.
Kuhusu hatua ya kutobadili riba akasema, unalenga kuhakikisha kiwango cha ukwasi kinaendelea kuwa cha kutosha katika uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei kubaki chini ya lengo la asilimia tano.
Anataja hilo linawezesha kuongezeka kwa kasi ya ukuaji uchumi kufikia wastani wa asilimia 5.7 katika robo ya kwanza ya mwaka huu.
Gavana Tutuba akafafanua kwamba, ni uamuzi unaolenga kuweka utulivu wa thamani ya shilingi, dhidi ya fedha za kigeni, ili kuendelea kukabili mfumuko wa bei ubaki katika kasi ndogo, hali inayochangia jitihada za kuwafanya wananchi kutofanya miamala yao kwa kutumia fedha za kigeni nchini.
Kuhusu mwenendo wa uchumi wa dunia, Tutuba, anasema kamati hiyo imebaini kuwa ripoti zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia, zinaonesha ukuaji uchumi unakadiriwa kuwa imara katika mwaka uliomalizika.
Anasema katika robo ya nne ya mwaka 2024, kamati ikabaini mazingira ya uchumi duniani yameimarika kwa kiwango kikubwa, kasi ya ukuaji uchumi kuongezeka, mfumuko wa bei ukaendelea kupungua katika nchi nyingi, huku mazingira ya upatikanaji fedha kwa riba nafuu katika masoko yakiwa yameimarika.
Anasema, mazingira mazuri ya kiuchumi yanatarajiwa kuendelea katika robo ya kwanza ya mwaka huu, kutokana na kuongezeko mahitaji ya walaji.
Mengine anayataja katika hilo, ni kuwapo sera wezeshi za bajeti na kuimarika mazingira ya upatikanaji fedha kwa riba nafuu.
Anatahadharisha kwamba, ni mambo yanayoweza kuathiriwa na migogoro ya kisiasa duniani na mivutano ya kibiashara kuongezeka.
“Uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar umeendelea kuwa imara kwa mwaka 2024. Uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024.
“Unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.6 katika robo ya tatu na asilimia 5.7 katika robo ya nne ya mwaka 2024, kwa kuzingatia mwenendo huo, ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuwa sawia na matokeo ya ukuaji wa asilimia 5.4 kwa mwaka 2024.” anasema.
Pia, anataja hali ya ukuaji huu umechangiwa zaidi na ongezeko la shughuli za kilimo, usafirishaji, ujenzi, na biashara,” anasema Tutuba
SURA NZIMA MUUNGANO
Kwa upande wa Zanzibar, anataja uchumi anakua kwa asilimia 6.8 katika robo ya kwanza na asilimia 7.2 katika robo ya pili ya mwaka 2024, makadirio yajayo ni kwamba, utakua kwa viwango hivyo kwa robo mbili zinazofuata, hivyo kufikia wastani wa ukuaji asilimia 7.2 kwa mwaka ulioisha 2024.
Anazitaja shughuli zilizochangia kukua kwake kuwa ni pamoja na utalii, ujenzi na viwanda.
Kwa mujibu wa Tutuba, ukuaji wa uchumi kwa Tanzania Bara na Zanzibar, unatarajiwa kuendelea kuwa wa kasi ya kuridhisha, kwa takriban asilimia sita na asilimia 6.8.
“Ukuaji huu unatarajiwa kuchangiwa na ongezeko la uzalishaji katika shughuli za kilimo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi, maboresho katika usafirishaji na ugavi, nishati ya uhakika, pamoja na utekelezaji wa sera za fedha na kibajeti.
“Ukuaji wa fedha na mikopo kwa sekta binafsi uliendelea kuwa wa kasi ya kuridhisha mwaka 2024, ambapo ulifikia wastani wa asilimia 12.5 na asilimia 16.9, mtawalia’ anafafanua Tutuba
Eneo lingine analitaja Tutuba ni katika ukwasi wa fedha za kigeni, ulioongezeka kwa kiwango kikubwa katika robo ya nne ya mwaka 2024.
Anaitaja kuwa ni hali iliyotokana na kuimarika mazingira ya upatikanaji fedha duniani kutokana na kupungua kwa riba katika nchi zinazoendelea na kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni nchini.
Tutuba anataja ni kutokana na shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu, korosho na tumbaku.
Anasema thamani ya shilingi inatarajiwa kuimarika katika robo ya kwanza ya mwaka uliopo, kutokana na kuwapo ukwasi wa kutosha wa fedha za kigeni uliopatikana katika robo ya nne ya mwaka 2024,.
Hapo ana ufafanuzi wa utekelezaji wa sera ya fedha, uamuzi wa kubakiza Riba ya Benki Kuu kuwa asilimia sita, na bei za bidhaa katika soko la dunia kuwa nafuu.
Ni uamuzi anaoutaja utachangiwa na Benki Kuu kuendelea kusimamia utekelezaji wa kifungu cha sheria yake, kinachohimiza matumizi ya shilingi, unaofanya miamala ndani ya nchi kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni yasiyokuwa ya lazima.
Aidha, anasema Benki Kuu inatarajia kuendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, na kuongeza pale zitakapohitajika.
Gavana anaeleza akiba iliyopo sasa ni zaidi ya Dola za Marekani bilioni 5.5 ni kiwango kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa zaidi ya miezi minne.
Kuhusu mikopo kwa sekta binafsi, anasema: “Ukuaji wa fedha na mikopo kwa sekta binafsi uliendelea kuwa wa kasi ya kuridhisha mwaka 2024, ambapo ulifikia wastani wa asilimia 12.5 na asilimia 16.9, mtawalia.
“Katika robo ya nne ya mwaka 2024, ujazi wa fedha ulikua kwa wastani wa asilimia 14.8 kwa mwaka ikilinganishwa na asilimia 13.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2023, huku mikopo kwa sekta binafsi ikikua kwa wastani wa asilimia 16.8 ikilinganishwa na asilimia 17.8.
“Mwenendo huu unatokana na ongezeko la mahitaji ya mikopo mipya kufuatia kuimarika kwa uchumi wa dunia na hapa nchini, pamoja na kupungua kwa vihatarishi katika ukopeshaji kufuatia kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu kufikia asilimia 3.6 mwezi Novemba 2024 kutoka asilimia 4.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2023” anasema Tutuba
Tutuba anafafanua kuwa nakisi ya urari wa malipo ya nje ilipungua kufikia asilimia 2.7 ya Pato la Taifa, ikiwa ni nakisi ya chini kabisa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, na ikilingashwa na asilimia 3.7 mwaka 2023.
Anasema hali hiyo, ilitokana na ongezeko la mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yanayo kadiriwa kufikia takriban asilimia 20 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 18 katika mwaka uliotangulia, kutokana na ongezeko la shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu, korosho na tumbaku nje ya nchi.
Uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje ya nchi ulikuwa asilimia 21 ya Pato la Taifa ukilinganisha na asilimia 20.3 mwaka 2023.
Anasema katika robo ya nne ya mwaka 2024, urari wa malipo ya kawaida ulikadiriwa kufikia nakisi ya dola za Marekani milioni 643.4, ikiwa ni takriban nusu ya nakisi iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Tutuba, anasema akiba hiyo inatarajiwa kubaki katika kiwango hicho katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 kutokana na juhudi zinazofanywa na Benki kuu katika kuongeza akiba ya fedha za kigeni, ikiwamo kununua dhahabu hapa nchini.
Hata hivyo katika mazungumzo yake, anasema Kamati itakutana tena wiki ya kwanza ya mwezi Aprili kwa ajili ya kutathmini mwenendo wa uchumi na kuamua Riba ya Benki Kuu itakayotumika katika robo ya pili ya mwaka (Aprili hadi Juni) 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED