Umma wafurika kortini kesi mauaji Katibu wa CCM ikiahirishwa tena

By Francis Godwin , Nipashe
Published at 08:36 AM Feb 19 2025
Washtakiwa watano wa mauaji ya ali-yekuwa Katibu wa Chama Cha Mapin-duzi Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Christina Kibiki wakifikishwa kwa mara nyingine katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa jana.
PICHA: FRANCIS GODWIN
Washtakiwa watano wa mauaji ya ali-yekuwa Katibu wa Chama Cha Mapin-duzi Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Christina Kibiki wakifikishwa kwa mara nyingine katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa jana.

KESI ya mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilolo, Christina Kibiki imeahirishwa hadi Machi 3 mwaka huu kwa kile kilichodaiwa upelelezi haujakamilika.

Ombi la kuahirisha kesi hiyo liliwasilishwa mahakamani huko jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Rehema Mayagilo na Mawakili wa Serikali, Radhia Njovu na Cecilia Mrisho.

Mawakili hao walidai kuwa kwa mujibu wa sheria, upelelezi unapaswa kukamilika ndani ya siku 90 na kwamba zimebaki siku 30, hivyo wanaomba mahakama kuahirisha kesi hiyo.

Mawakili wa Utetezi Barnabas Nyalusi, Gloria Mwandelema na Neema Chacha waliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa wiki moja kwa kile walichodai inavuta hisia za watu wengi wanaofika kwa ajili ya kusikiliza.

Baada ya Mahakama kusikiliza pande zote mbili, iliridhia kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 3 mwaka huu.

Hakimu Rehema alisema upelelezi unatakiwa ukamilike ndani ya siku 90. Hadi kufikia jana, kesi ilikuwa imefikia siku 60, hivyo bado kuna muda wa siku 30 za kukamilisha upelelezi. 

Hakimu Rehema, akijibu ombi la upande wa utetezi juu ya kesi hiyo kurudi baada ya siku saba, alisema washtakiwa ambao makosa yao hayana dhamana, wanatakiwa kurudi mahakamani kwa siku zisizozidi 15, hivyo washtakiwa wamepangiwa kurudi mahakamani baada ya siku 15 ambayo ni Machi 3, mwaka huu.

Washtakiwa wote waliendelea kuwa kimya bila kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya mauaji.

Washtakiwa walirudishwa rumande hadi Machi 3 mwaka huu, kesi hiyo itakapoletwa kwa ajili ya kutajwa tena.

Katika viunga vya mahakama hiyo, ndugu, jamaa na marafiki walijitokeza kufuatilia mwenendo wake.