Ubungo yapokea msaada vifaatiba, wodi ya watoto

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 11:19 AM Jan 28 2025
Meya wa Ubungo, Jafari Nyaigesha (katikati mwenye bluu) na kushoto ni Mganga Mkuu wa Halmashauri Ubungo, Dk.Tulitweni Mwinuka pamoja na viongozi Kanisa la Yesu Kristo Siku za Mwisho, wakizundua jengo
Picha: Mpigapicha Wetu
Meya wa Ubungo, Jafari Nyaigesha (katikati mwenye bluu) na kushoto ni Mganga Mkuu wa Halmashauri Ubungo, Dk.Tulitweni Mwinuka pamoja na viongozi Kanisa la Yesu Kristo Siku za Mwisho, wakizundua jengo

KITUO cha Afya Kimara, kilichoko Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, kimepokea vifaatiba vya shilingi milioni 91 na kuanza kutoa huduma za kliniki za kibingwa na kuanzisha wodi ya watoto wachanga.

Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Kimara, Dk. Malamla Chaulenzi, amesema kukamilika kwa huduma hizo, kutaisaidia kurahisisha matibabu ya watoto hao, kwa ipo idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa na kuondoa usumbufu ya kwenda umbali mrefu kufuata huduma muhimu.

Amesema kukamilika kwa huduma hizo, ikiwamo miundombinu ya  majengo na vifaatiba kumewezeshwa na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, kwa asilimia kubwa kwa ushirikiano kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa.

Meya wa Ubungo, Jafari Nyaigesha, amesema wanawashukuru wadau hao, kwa kuiunga mkono serikali kwa kuisadia jamii na kuipa kipaumbele huduma za afya nchini, ni mfano wa kuigwa kwa mashirika, taasisi na watu mmoja mmoja, wenye fursa ya kuisaidia jamii yao.

Ubungo yapokea msaada vifaatiba, wodi ya watoto
“Tunalipongeza kanisa hili kwa kuweka kipaumbele kuwekeza katika afya, hasa ya mama na mtoto na kubwa zaidi, tumeshukuru wamefuata miongozo ya nchi na kuheshimu tamaduni zetu za Kitanzania pasipo kukengeuka maadili,” amesema.

Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, Juventus Rubona, amesema kanisa hilo limetumia kiasi cha shilingi milion 688 katika kuwezesha gharama zote za jumla, kukamilisha kuanzishwa kwa huduma ya Mama na Mtoto katika kituo hicho.

Ubungo yapokea msaada vifaatiba, wodi ya watoto
Pia ujenzi wa jengo, miundombinu, ununuzi wa vifaatiba, ikiwamo na kuongeza watumishi watakaowezesha kufanya kazi kwa weledi mkubwa katika kituo hicho, ili kuboresha huduma za kiafya ziende kwa wakati na tija.

Amefafanua kanisa hilo limejikita zaidi kuwekeza kwenye huduma za kijamii, ikiwamo afya, elimu na nyingine, kwa kuwa Mungu ndio ameamrisha hivyo na fedha zinazofanya hivyo zinatokana na zaka wanazotoa waumini.