TUME ya Rais ya Maboresho ya Kodi, imefika mkoani Pwani, kwa ajili ya kukusanya maoni, pamoja na kupokea mapendekezo ya namna ya kuboresha masuala ya kodi nchini.
Tume hiyo ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Maimuna Tarish na Mjumbe Prof. Florens Luoga, ambaye pia ni Gavana mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).Tume hiyo, ilikutana na wawakilishi wa wafanyabiashara, wawekezaji, viongozi wa wamachinga, vyama vya wafanyakazi na wajasiriamali mjini Kibaha.
Mbali ya makundi hayo pia, zilikuwapo taasisi wezeshi ikiwamo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani, pamoja na wadau wengine wa mkoa huo.Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, akifungua mkutano wa kukusanya maoni hayo amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa kuunda tume hiyo.
Amesema lengo la rais kuunda tume hiyo ni kutaka kufanya maboresho ya kodi, kuondoa malalamiko kati ya wakusanya kodi na walipakodi na kwa kufanya hivyo itasaidia kila mmoja kufanya vizuri kazi yake bila vikwazo.
Tarish, amesema kuwa rais aliunda tume hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wadau na wafanyabiashara mbalimbali.Gavana wa BoT mstaafu ambaye ni Mjumbe wa Tume hiyo, Prof. Luoga, amesema kuwa mara ya mwisho kuundwa tume hiyo ilikuwa miaka 35 iliyopita.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani, Abdallah Ndauka, amepongeza hatua ya rais kuunda tume ya maboresho ya kodi, huku akielezea kikwazo cha wafanyabiashara wengi kukosa uelewa kuhusu sheria na sera ya kulinda mitaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED