MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umesikitishwa na kuahirishwa mara kwa mara, kusomwa kwa umamuzi mdogo wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika kesi ya kikatiba ya Onesmo Olengurumwa, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wakili Olengurumwa, ambaye ni Mratibu wa Kitaifa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, aliwasilisha malalamiko hayo jana kwa vyombo vya habari kuhusu Shauri namba 36 la Mwaka 2019.
Alisema shauri husika linapinga uhalali wa kikatiba wa vifungu na 178, 243, 244, 245, 246, 247, 248, 249, 250, 256, 257, 258 na 259 vya Sheria ya Mwenendo ya Makosa ya Jinai, Sura ya 20.
Vifungu ambavyo vinaruhusu mtuhumiwa kufunguliwa kesi katika Mahakama za Chini (Committal Proceedings) wakati upelelezi ukiwa haujakamilika kwa makosa ambayo Mahakama Kuu ndio ina mamlaka ya kusikiliza mashauri hayo.
"Shauri hilo ambalo liko mbele ya Jaji Manyanda, lilipangwa kwa ajli ya uamuzi mdogo kwa mara ya kwanza Novemba 28, 2024 lakini uamuzi haukusomwa kwa sababu haukuwa tayari na uliahirishwa hadi Desemba 10, 2024.
"Desemba pia uamuzi uliahirishwa hadi Desemba 20, 2024 ambapo pia uliahirishwa tena hadi Januari 14 mwaka huu na siku hiyo pia uamuzi haukusomwa na kuahirishwa hadi Februari 6, mwaka huu na pia haukusomwa tena hadi Februari 18, 2025.
"Leo Februari 18, 2025 (jana), uamuzi mdogo haujasomwa kwasababu Jaji hakuwepo mahakamani na ndipo msajili amepanga uamuzi mdogo wa kesi hiyo usomwe Februari 25," alisema.
Alisema mpaka leo ahirisho hilo la kusomwa kwa uamuzi mdogo ni la tano jambo hili linalosababisha adha na usumbufu mkubwa kwa mawakili wanao simamia kesi hiyo kwa kupoteza muda wao mwingi mahakamani kusubiri kusomwa kwa uamuzi mdogo.
"Kucheleweshwa kusomwa kwa wakati kwa maamuzi ya Mahakama katika kesi hii ni kinyume cha kanuni zinazoongoza mashauri ya kikatiba nchini, ambapo kwa mujibu wa kanuni ya 9(1) ya Kanuni za Sheria ya Haki Msingi na Wajibu (Mwenendo na Utaratibu) za Mwaka 2014 inaelekeza kwamba Jaji anapaswa kutoa uamuzi wa mapingamizi ndani ya siku 30.
"Katika shauri hili tangu Jaji Manyanda apangiwe kusikiliza shauri hili na kupangwa kwa uamuzi mdogo sasa ni zaidi ya siku 30 zinazohitajika kwa mujibu wa sheria," alisema Ngurumo.
Alisema THRDC inasikitishwa na ukiukwaji huo wa sheria na utaratibu wa kimahakama na jambo hilo lina fifisha imani ya umma kwa mahakama na kuathiri utawala wa sheria, kwani haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa.
"Tunatoa wito kwa Mhimili wa Mahakama nchini kuhakikisha uamuzi unatolewa kwa wakati kama ambavyo inavyoelekezwa na sheria na kanuni ili kuweza kuonyesha kuwa haki inatendeka na inapatikana kwa wakati, jambo ambalo litaongeza imani ya wananchi kwa Mahakama nchini," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED