Sasa kila mwanafunzi na kitabu chake

By Restuta James , Nipashe
Published at 02:31 PM Feb 19 2025
Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba (kushoto), akizungumza kwenye mahojiano na Radio One jijini Dar es Salaam leo
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba (kushoto), akizungumza kwenye mahojiano na Radio One jijini Dar es Salaam leo

TAASISI ya Elimu Tanzania (TET), imeandaa mpango wa kuhakikisha kila mwanafunzi shuleni anakuwa na kitabu, ikiwa ni kusherehekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Aidha, ili kufikia lengo hilo, TET itashirikiana na wadau pamoja na wananchi kwa ujumla, kuwezesha uchapaji wa vitabu vya kutosha.

Akizungumza leo Februari 19, 2025 kwenye mahojiano maalumu na Radio One, leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba, amesema lengo ni kuweka uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja (1:1), kutoka hali ilivyo sasa kitabu kimoja, wanafunzi watatu (1:3).

“Tunasherehekea miaka 50 ya TET tukilenga kuhakikisha kila mwanafunzi ana kitabu chake…Machi 07, 2025 tutakuwa na matembezi ya hisani yanayolenga kukusanya fedha zitakazosaidia uchapaji wa vitabu. 

“Niwaombe wadau tushiriki matembezi haya ya hisani tukiunga mkono juhudi za serikali yetu katika sekta ya elimu,” amesema.

Vitabu
Dk. Komba amesema taasisi hiyo imeweka utaratibu utakaowezesha kila mwananchi kuchangia uchapaji wa vitabu hivyo, ili watoto wote nchini waweze kupata huduma hiyo muhimu.

“Niwaombe Watanzania kwamba unaweza kuchangia kiasi chochote kuanzia Sh. 2,000. Ukichangia 10,000 maana yake ni kwamba umewapatia watoto watano vitabu,” amesema.

Akijibu maswali ya wasikilizaji kuhusu idadi kubwa ya wanafunzi darasani, Dk. Komba amesema serikali imeendelea kufanya maboresho ikiwamo ujenzi wa shule mpya, kuongeza madarasa kwenye shule zilizopo na kuajiri walimu wapya, na kwamba kwa upande wa TET, wamewajengea uwezo walimu wanaofundisha madarasa yenye wanafunzi wengi, ili wayamudu.

“Tunaimani kubwa kwamba mitaala mipya itatekelezeka kutokana na mbinu ambazo tumeshawapa walimu, na mafunzo ambayo wataendelea kuyapata wakiwa kazini,” amesema.