RIPOTI MAALUM: Ukame ulivyobadili asili jamii ya Wamasai

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 09:06 AM Nov 16 2024
Mkazi wa Longido, mkoani Arusha, Jackline Filex akipanga mayai katika mashine maalum ya kuangulia vifaranga kwa ajili ya kuwauzia wananchi wenzake ambao ni wafugaji wa jamii ya Kimaasai.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Mkazi wa Longido, mkoani Arusha, Jackline Filex akipanga mayai katika mashine maalum ya kuangulia vifaranga kwa ajili ya kuwauzia wananchi wenzake ambao ni wafugaji wa jamii ya Kimaasai.

UTAMADUNI unaotajwa kuwa na nguvu barani Afrika sasa umetikiswa. Wakati zamani ilikuwa ‘haramu’ kwa jamii hiyo kufuga na kula mifugo yenye miguu miwili kama vile kuku, sasa wamegeuka kuwa walaji na wafugaji wazuri wa viumbe hao.

Vilevile, zamani jamii hiyo haikuruhusu watu wake kula mboga za majani, lakini sasa si tu ni wakulima, bali pia watumiaji wake.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii, umebaini shida kuu ni ukame uliotokana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo madhara yake yanatikisa si Tanzania tu bali duniani kote.

Neema Group ni moja kati ya vikundi vya ufugaji wa nyuki vilivyofanikiwa kiuchumi na kuongeza hamasa katika jamii ya Kimasai iliyoko eneo la Kimokouwa, Wilaya ya Longido, mkoani Arusha.

Losinyati Laizer, mkazi wa Kimokouwa, anasema wao ni wanufaika wa mradi wa ufugaji nyuki waliowezeshwa na Shirika la World Wildlife Fund (WWF), ili kunusuru uharibifu wa mazingira na ukataji miti ovyo.

Anasema matukio ya uchomaji mkaa, ujangili na uwindaji haramu wa wanyamapori, yamebadili maisha yao tangu walipoanza kurina asali na kuuza kila baada ya miezi mitatu.

“Katika kikundi chetu tuko watu 25 na tumepewa mizinga ya nyuki 15, ufugaji huu umetusaidia sana. Tunatarajia wiki hii kurina asali iliyoko kwenye mizinga. Makadirio yetu hapa ni kuvuna lita 1,200 za asali ambayo tukiuza tutapata Sh. milioni 1.2.

“Tutaiuza na yale mazao ya nyuki, kwa mfano masega tunayatengeneza tupate nta ili tutengeneze sabuni, dawa za kuchua, mafuta ya kupaka na dawa ya kupaka mdomo unaopasuka.

“Mradi huu wa nyuki unatunusuru sisi jamii ya kifugaji ya Kimasai tusifanye tena biashara haramu na tusifanye tena ujangili wa wanyamapori ili tuendeleze maisha yetu, tusomeshe watoto na tuajiri wengine,” anasema Losinyati.

Anasema kwa sasa bei ya asali imezidi kupaa ambapo kilo moja ni Sh. 10,000 na kwa Dar es Salaam, inauzwa kati ya Sh. 15,000 hadi Sh. 20,000.

Losinyati anasema mradi huo utakwenda kupanuka kwa kuongeza wigo, kwa kuwa watajenga makazi bora na wataongeza kipato chao na kukua kiuchumi.

Mwanamke huyo anasema hajutii kuwekeza nguvu nyingi katika mradi huo, tofauti na ufugaji wa asili wa ng’ombe na mbuzi waliouzoea.

“Tunawashukuru Shirika la WWF, kupitia Mradi wa Land for Life. Hivi sasa tumeanza kunaona mabadiliko kiuchumi. Kwa kweli ukataji wa miti kwa ajili ya uchomaji mkaa umepungua, kwa sababu unajua nyuki, pia wanategemea miti kuchavusha asali.

“Lakini pia tutaendelea kutoa elimu kwa wengine wanaofanya uharibifu wa mazingira, waache na wajiingize katika biashara ya ufugaji wa nyuki na ufugaji wa kuku, ambao ni rafiki kwetu na mazingira,” anasema.

Losinyati anasema nyuki wanawasaidia ndani ya mashamba yao kuchavusha mazao, kwa hiyo asilimia kubwa ya biashara haramu ya uwindaji wanyamapori na uharibifu wa mazingira umepungua, kwa sababu mradi wa nyuki umewasaidia.

Anabainisha kwamba kwa miaka mingi jamii ya wafugaji wa Kimasai ilijikita katika ufugaji mbuzi, ng’ombe na kondoo, lakini hawakuwa na ujuzi wa ufugaji nyuki wala kuku.

Mkazi Mwingine wa Kimokouwa, mama wa watoto wa tatu, Peipei Losinyati (25), anasema ufugaji wa nyuki umewasaidia wanawake kujiinua kiuchumi, sasa wanaweza kuwasomesha watoto katika shule za mchepuo wa Kingereza na shule za umma.

Pia wamepiga hatua kibiashara na wanaendeleza biashara zao ndogondogo, kutokana na fedha wanazopata kupitia ufugaji wa nyuki na kuku.

Peipei anasema biashara nyingine wanazofanya kwa kutumia kipato cha mauzo ya asali na mazao yake, ni kuuza bidhaa nyingine kama sukari, majani ya chai, mayai na chumvi huku vijijini.

Mkazi mwingine wa Kimokouwa, Nagelii Laizer (33) ambaye ni mama wa watoto watatu, anasema Shirika la WWF limekuwa msaada mkubwa wa kiuchumi ndani ya jamii yao.

“Walivyokuja kutupa mafunzo, walitaka tuwafundishe na wenzetu namna ufugaji nyuki na kuku unavyoweza kubadili maisha yetu kiuchumi.

“Tunamwona nyuki ni mdogo lakini ni mdudu ambaye ni kitega uchumi kipya cha jamii za Kimasai,” anasema Nagelii.

Hadi sasa, kuna aina zaidi ya 20,000 za nyuki duniani, lakini maarufu zaidi ni; nyuki wa kazi ambao ni wa kike, waumbaji watafutaji malighafi ya asali na wa kiume, wako katika uzazi zaidi.

Tanzania ina aina mbili kuu za nyuki, nyuki wanaouma na wasiouma. Nyuki wasiouma huishi ndani ya matundu chini ya matawi makubwa ya miti, katika vichuguu vya mchwa na hata chini ya mapaa ya nyumba.  

Inaaminika nyuki wasiouma, asali yao ina uwezo mkubwa kutibu maradhi kuliko ya wanaouma. Nao wako katika makundi: Nyuki wa kazi (Apis mellifera) na nyuki wa kiume (Drones). 

Pia, kuna Malkia (Queen Bee), ambaye majukumu yake ni kuzalisha mayai na kuongoza ‘koloni’. Anazalisha kemikali inayoitwa ‘feromoni’ inayowasaidia nyuki wengine kudumisha utaratibu wa ‘koloni’. 

Sera ya Taifa ya Ufugaji wa Nyuki ya Mwaka 1998, lengo lake ni kuimarisha mchango wa kudumu wa sekta hii, kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.

Inajumuisha kwa pamoja nyuki wanaouma na wasiouma, bila kujali masuala ya umiliki na usimamizi. Sera inahusu pia makundi ya nyuki wasiofugwa na wale wanaofugwa pamoja na nyuki wengine ambao hukusanya mbochi (nectar) au chavua (pollen) kama chakula chao.

Kuhusu ufugaji kuku na biashara ya kuuza vifaranga wa kuku, mjasiriamali Jackline Filex (29), mkazi wa Longido, ambaye anafanya kazi ya kuangua vifaranga kwa njia ya kisasa, anasema kazi hiyo imewafanya wasahau kuuza nyama inayotokana na shughuli za uwindaji haramu wa wanyamapori.

Anasema awali walikuwa wakiuza nyamapori zinazotoka katika ushoroba wa wanyamapori wa Kitendeni, ambao ni mapito ya wanyamapori wanaohama kati ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro na Hifadhi ya Amboseli ya nchini Kenya, kwa ajili ya kutafuta malisho na maji.

“Ninawashukuru WWF, kwanza kwa kututoa tulipokuwa mwanzo katika uwindaji haramu wa wanyamapori, wametuelimisha tumetoka huko baada ya kutuletea mradi wa kuku na mashine za kuangulia vifaranga, ambao sasa tunanufaika nao kiuchumi kwa kuuza vifaranga vya kuku wa mayai na nyama.

“Tangu waliponiletea mashine ya kuangua vifaranga, tumeshaangua vifaranga zaidi ya 400 kwa ajili ya vikundi vya kijamii. Tukitotolewa mitetea ya kuku tunabaki nayo, tunauza mayai na tunauza majogoo,” anasema.

Jackline anasema walikuwa wanapelekwa nyama za wanyamapori kwa ajili ya kuuza mitaani na kula majumbani.

“Tumegundua kwamba ni kosa kisheria, kwa hiyo sasa hivi hatufanyi tena hiyo biashara, kwa sababu kuna miradi ya kuku inalipa,” anasimulia.

WAZEE MILA WABARIKI

Mwenyekiti wa viongozi wa mila (Leigwanani), Lekishon Mollel anasema wamebariki vijana, wanawake na wanaume kufanya biashara hiyo.

Anasema viongozi wa mila wa jamii hiyo wameridhia hilo kwa sababu ina matokeo ya haraka ya kutoa kipato cha uhakika ambacho hakipigiwi kelele kwamba kina haribu mazingira.

Anasema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa sababu huko nyuma, watu hawakujua kuhusu utunzaji wa mazingira, lakini Shirika la Kimataifa la WWF, wametoa elimu kwa jamii hiyo kuhusu utunzaji mazingira na kujikita katika ufugaji wa nyuki na kuku ambao kwao sasa ni neema.

Anabainisha kwamba kinachowafanya hivi sasa wanawake kwa wanaume kugeukia ufugaji huo, ni changamoto ya ukame na uhaba wa malisho ya mifugo yao.

Mzee mwingine wa mila na mfugaji, Saruni Olekuru Kayongo, anasema tatizo la wanyamapori wakali kama simba, chui na fisi kuvamia maboma yao ya mifugo na kuila, ni miongoni mwa sababu zilizosukuma jamii yao kujikita katika ufugaji kuku na nyuki.

HALI ILIVYO

Meneja Mradi wa Land for Life, unaotekelezwa na Shirika la Kimataifa la WWF, Reguli Marandu, anasema wanafanya kazi za uhifadhi katika vijiji hivyo, na wanapozungumzia uhifadhi wanaangalia mazingira na wanyamapori.

Marandu anasema kuna miradi mingi imeanzishwa kwa ajili ya kuboresha kipato cha jamii zinazoishi pembezoni mwa misitu na inatekelezwa ikiwamo kilimo cha alizeti.

Anasema pia huangalia namna gani uhifadhi unavyosaidia jamii zinazozunguka mazingira hayo ambayo wanayahifadhi.

“Dhana ya WWF, tunataka jamii zile zinazoishi katika mazingira hayo pamoja na wanyamapori na mazingira yetu vyote viwe na ustawi mzuri,” anasema.

Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Nchini (TFS), Prof. Dosantos Silayo, akizungumzia matokeo chanya ya mradi wa ufugaji wa nyuki Longido, anasema wadau hao wa ufugaji nyuki, wanapaswa kujiandaa kimkakati kutuumia mkutano wa dunia wa ufugaji nyuki (Apimondia) utakaofanyika Arusha mwaka 2027 ili kujiinua kiuchumi na kuvutia watalii.

Anasema utunzaji mzuri wa mazingira utawezesha nyuki kuzaliana kwa wingi na kuwezesha uchumi kukua.