CHUO Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimepokea ruzuku ya Sh. bilioni 12.5 kutoka Sweden kupitia Shirika la Maendeleo (SIDA).
Fedha hizo ni kwa ajili ya kufundisha wataalam wa afya katika ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu, kufanya utafiti na kuboresha ubunifu.
Akizungumza juzi wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba huo katika Kituo cha Umahiri wa Moyo na Mishipa ya Damu kilichoko Mloganzila, jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema mkataba huo utadumu kwa miaka sita, kuanzia Desemba 2024 hadi Juni 2030.
Alisema hatua hiyo ni ushirikiano ulioko kati yao na Sweden, ulioanza tangu mwaka 1980, ukilenga kukuza utafiti na mafunzo ya wataalam wa afya na kutoa fursa kwa wanafunzi kuchangia ubunifu na uvumbuzi.
Prof. Kamuhabwa alisema MUHAS itashirikiana na vyuo vikuu vitatu vya Sweden ambavyo ni Umeå, Karolinska, na Uppsala ambapo wanafunzi watakaonufaika na programu hiyo, watapata fursa ya kutuma sampuli za utafiti na kusoma baadhi ya masomo kwenye vyuo hivyo.
Alisema matokeo ya ushirikiano wao tayari yameleta mafanikio katika kuboresha miongozo, mifumo, na sera zinazohusiana na sekta ya afya.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, anayeshughulikia Utafiti na Uvumbuzi, Prof. Bruno Suguya, alisema mradi huo utatekelezwa kwa hatua tofauti.
Alisema kila mwaka programu mbalimbali zitafanyika chini ya usimamizi wa pamoja kati ya MUHAS na vyuo vya Sweden.
Alisema ripoti za utekelezaji wa mradi zitawasilishwa katika Ubalozi wa Sweden na kupitiwa na Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA) kwa ajili ya kupitishwa.
Alisema ruzuku hiyo itajikita kutekeleza utafiti katika magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu, huduma za mama na mtoto na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI
“Tunaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya utafiti katika sekta ya afya kwa ushirikiano na Sweden, na tunapata hati safi katika maeneo kama ukaguzi wa mahesabu na utoaji wa mafunzo bora,” alisema Prof. Suguya.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema MUHAS imekuwa moja ya taasisi kinara inayotoa ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za sekta ya afya nchini kupitia utafiti wake.
"Kwa miaka minne nikiwa Mwenyekiti wa Bodi, nimeona utafiti mahiri unaofanywa na chuo hiki, tuna uhakika kwamba fedha hizi zitaleta bunifu nyingi zaidi katika kutatua matatizo ya afya nchini," alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema MUHAS kwa mara nyingine, inanufaika na ufadhili kutoka Sweden kwa ajili ya kuimarisha utafiti katika maeneo nyeti ya sekta ya afya.
Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Macias, alisema ushirikiano wa Tanzania na Sweden katika utafiti wa sekta ya afya umeanza miaka 48 iliyopita na umelenga kuongeza uwezo wa MUHAS kushughulikia changamoto zilizoko katika sekta ya afya, rasilimali watu, sera na magonjwa.
Alisema wanatarajia MUHAS itaendelea kutoa mafunzo ya utafiti wa kiwango cha juu kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya nchini na kwamba ufadhili huo utaimarisha zaidi juhudi za chuo hicho katika kuzalisha wataalamu wabobezi.
Wakati wa ufunguzi wa kongamano la kidigitali katika sekta ya afya lililofanyika eneo la Mloganzila, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alisema, katika kipindi cha miaka mitatu, serikali imetumia Sh. trilioni 6.2 kuboresha sekta hiyo.
Alisema uboreshaji huo umehusisha ujenzi wa miundombinu ya utoaji huduma, ununuzi wa vifaa tiba, ikiwamo vya uchunguzi na dawa ili huduma za afya kuwafikia wananchi wengi.
Akielezea umuhimu wa kukuza utaalamu na utafiti, Waziri Mhagama alisema MUHAS inatoa wataalam wabobezi ambao wamesaidia kuimarisha huduma za afya nchini.
Alisema amefurahishwa na teknolojia inatumiwa na Sweden katika kutoa taarifa za viashiria ya ugonjwa wa saratani ya matiti na kizazi kwa kina mama.
Alisema teknolojia hiyo ina uwezo wa kutoa taarifa za mgonjwa kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali.
Waziri Mhagama alisema wamejipanga kutumia ubunifu huo ili kusaidia utoaji wa huduma za awali kwa wagonjwa wanaobainika mapema kuwa na viashiria vya saratani.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED