KATIBU Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi Tanzania, Beng'i Issa ametambulisha mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi wa Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA) huku akiwahimiza wafanyabiashara kurasimisha biashara zao ili kunufaika na fursa mbalimbali za mikopo na uwezeshwaji.
Beng'I amebainisha hayo leo Novemba 15 mkoani hapa na kueleza kuwa idadi kubwa ya wafanyabiashara nchini hawajarasimisha biashara zao hali inayosababisha wakose fursa muhimu za uwezeshwaji.
“Ukishafanya biashara ambayo siyo rasmi na hujasajiliwa popote huwezi kupata fursa yoyote ikiwemo mikopo wa asilimia 10 wala zabuni za serikali,” amesema Beng'i.
Aidha amesema kuna sera ya serikali inayoelekeza kuhusu asilimia 30 ya manunuzi yanayofanywa na serikali kutakiwa yafanywe kupitia makundi maalum, wanawake vijana na wenye ulemavu lakini asilimia hiyo bado haijafikiwa hata kwa asilimia tano kutokana na watu kukosa fursa hiyo kwa kutokufanya shughuli rasmi.
“Ukirasmisha biashara zako unakuwa umefungua milango ya kuendelea mbele zaidi na hii ni kati ya vitu ambavyotumeviona hivyo kuamua kuja na mafunzo ya kuwaelekeza fursa zilizopo na nini wafanye ili kuzipata ikiwemo na namna ya kutumia mitandao vyema kutokana na kila jambo linalofanyika ndani ya serikali kuhitaji kupitia kwenye mfumo,” amesema Beng'i.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amesema serikali itaendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwaletea programu katika kila sekta ili waweze kuwekeza mitaji na kukua kiuchumi hususani katika shughuli za ujasiriamali.
Amesema mkoani hapa zaidi ya Sh.bilioni moja zimekopeshwa kwa wavuvi kwa kuwapatia boti za kisasa ili kuwawezesha wavuvi kupata tija kwenye uvuvi na mazao yatokanayo na Ziwa Victoria na kuwa zaidi ya Vikundi 35 vya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba ambavyo vimekopeshwa zaidi ya Sh.bilioni 4.4 na Benki ya Maendeleo ya kilimo (TADB) kwa ajili ya kuwainua kimtaji na kuwaondoa kwenye uvuvi wa zamani na kufuga kisasa.
"Mradi wa vijana wa unenepeshaji mifugo kwenye shamba letu la Mabuki umewawezesha vijana 35 kupata ujuzi wa ufugaji wenye tija na wameshahitimu na hivi karibuni serikali itawapatia vitalu kule Kitengule kwa ajili ya kufanya ufugaji,” amesema Mtanda.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED