HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, jana ilizindua Kitengo cha Kuhifadhi na Kuratibu Maziwa ya Mama kuhakikisha watoto njiti wanapata maziwa ya mama zao kwa wakati.
Aidha, wataalam wa afya nchini wamesisitiza kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kupigania maisha ya watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya muda, ili kupunguza vifo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi, alisema hayo jana wakati akifungua maadhimisho ya kuelekea siku ya mtoto aliyezaliwa kabla ya muda (njiti) yaliyofanyika katika MNH–Mloganzila.
Alisema lengo ni kufikia mkakati uliowekwa ifikapo mwaka 2030, vifo vya watoto wachanga kuwa chini ya vifo 12 katika kila vizazi hai 1,000 .
Prof. Janabi alisema kila watoto 1,000 kuna watoto wachanga wapatao 24 wanaofariki dunia ndani ya siku 28 za kwanza na kwamba mikakati ya kupunguza vifo hivyo haiwezi kuwa endelevu bila kushirikiana wadau katika sekta ya afya na kuboresha ujuzi wa kuhudumia watoto hao.
Alisema serikali kupitia Wizara ya Afya, imekuwa ikiratibu progamu mbalimbali ambazo lengo lake ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na walio chini ya miaka mitano, programu hizo ni kama kumsaidia mtoto kupumua baada ya kuzaliwa, kupanua huduma za watoto wachanga kwa kujenga wodi za watoto wachanga hospitali za mikoa na wilaya na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ya namna ya kuhudumia watoto wachanga.
Bingwa Bobezi wa Watoto Wachanga MNH, Dk. Martha Mkony, alisema katika Afrika takribani mtoto mmoja kati ya 10, huzaliwa kabla ya wakati na watoto hao hukabiliwa na matatizo mbalimbali kama vile kupumua, maambukizi na hatari za ukuaji kwa muda mrefu.
“Pamoja na kuwapo kwa changmoto hizo, lakini bado kuna matumaini kupitia juhudi za serikali, kwani kuna maboresho ya kutia moyo katika utunzaji wa watoto wachanga nchini kwa kuboresha vituo vya afya na hospitali za kuhudumia watoto wachanga na kujengwa pamoja na kusomesha wataalam wa afya,” alisema Dk. Mkony.
Maadhimisho hayo yameenda sambamba na uzinduzi wa Kitengo cha Kuhifadhi na Kuratibu Maziwa ya Mama kwa kuhakikisha watoto hao wanapata maziwa ya mama zao kwa wakati kwa kuWa watoto wanaozaliwa kabla ya muda wanakuwa na uzito mdogo unaosababisha kuhitaji kiasi kidogo cha maziwa.
“Mama ana uwezo wa kutoa maziwa mengi kiasi kinachobaki kinahifadhiwa, hivyo ni rahisi mama akiruhusiwa kurejea nyumbani anakwenda na maziwa yake. Hii inasaidia mpango wa kuhakikisha watoto wachanga wananyonyeshwa miezi sita bila kupewa chochote,” alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED