Dk. Nchemba ataka utekelezaji ahadi ya mabadiliko tabianchi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:30 AM Nov 16 2024
Dk. Nchemba ataka   utekelezaji ahadi ya  mabadiliko tabianchi
Picha:Mtandao
Dk. Nchemba ataka utekelezaji ahadi ya mabadiliko tabianchi

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, amezitaka nchi zilizoendelea kutimiza ahadi yao ya kutoa dola za Marekani bilioni 500, sawa na dola bilioni 100 kila mwaka kwa ajili ya kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka 2025.

Dk. Nchemba alitoa kauli hiyo jana wakati akichangia hoja katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Mawaziri uliojadili namna ya kupata fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku, nchini Azerbaijan. 

Alisema ripoti ya Mkutano wa COP28, uliofanyika Dubai mwaka jana, inaonesha kwamba kuna kasi ndogo katika kutimiza ahadi ya Mkataba wa Paris katika kuhamasisha upatikanaji ama uchangiaji wa dola 100 bilioni ambapo kuna pengo la takribani dola bilioni 60 kila mwaka hali inayo ziathiri nchi zinazoendelea katika kupanga mipango ya maendeleo.  

Aidha, Dk. Nchemba alisema Tanzania inataka kuwe na uwazi katika namna fedha hizo dola bilioni 100 zinazotakiwa kutolewa kila mwaka kwa nchi zinzoendelea ili kuweka uwajibikaji kulingana na Mkataba wa Paris kuhusu suala hilo la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. 

Alisema kuwa mabadiliko ya tabianchi ni janga linalobomoa uchumi wa nchi zinazoendelea na kushauri matamanio na ahadi zinazotolewa na mataifa makubwa yawekwe katika vitendo ili kuzinusuru nchi zinazoendelea kutokana na madhara yanayosababishwa na mabadiliko hayo ya tabianchi. 

Dk. Nchemba alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea iliyoathirika na matokeo hasi ya mabadiliko ya tabianchi na inajitahidi kutumia rasilimali zake kukabiliana na athari hizo ikiwemo kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko lakini fedha hizo za ndani hazitoshelezi mahitaji. 

“Pia tunatoa wito wa kupitia upya usanifu wa kifedha wa kimataifa na utaratibu wa ufadhili chini ya mkataba ili kusaidia uhamasishaji wa fedha thabiti na za muda mrefu kwa kiwango cha uwekezaji unaohitajika na nchi zinazoendelea kupambana na shida ya mabadiliko ya tabianchi” alisema. 

Zaidi wa watu 50,000 wakiwemo wanadiplomasia kutoka zaidi ya nchi 200 wanachama wa Umoja wa Mataifa, wanakutana katika jiji la Baku, Azerbaijan kujadili namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutafuta vyanzo vya fedha za uhakika za kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia.