MKUTANO wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Kundi la G20 kutoa fursa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki mijadala inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika mapambano dhidi ya njaa na umaskini.
Pia kuchochea maendeleo endelevu na matumizi ya nishati mbadala.
Mkutano huo utakaofanyika nchini Brazil, unaotarajia kufanyika kwa siku mbili kuanzia Novemba 18, mwaka huu,
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga, Rais Samia amealikwa na Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva, na Mwenyekiti wa G20.
Taarifa hiyo ilisema Rais Samia amealikwa kushiriki mkutano wa jukwaa hilo lenye lengo la kukuza ushirikiano wa kimataifa kwenye masuala ya kiuchumi.
“Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuhudhuria katika mkutano wa G20. Mwaliko huu unatokana na heshima na ushawishi mkubwa ambao Rais Samia amejijengea katika majukwaa ya kimataifa,” ilisema taarifa hiyo.
Kadhalika ilisema pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo, Rais Samia anatarajia kushiriki mijadala hiyo na pia, kutumia jukwaa hilo linalokutanisha nchi zenye uchumi kubwa zaidi duniani kuelezea jitihada zinazofanywa na serikali kuhakikisha usalama wa chakula.
Pia kupunguza umaskini, kujenga maendeleo endelevu na kutafuta fursa za ushirikiano zitakazowaletea ustawi Watanzania kupitia sekta za uzalishaji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, akiwa nchini humo, Rais Samia atafanya mikutano ya pembezoni na taasisi kubwa za kifedha duniani pamoja na kukutana kwa mazungumzo na wakuu wa nchi na serikali pamoja na baadhi ya nchi wanachama wa G20 akiwamo mwenyeji wake wa Brazil.
Taraifa hiyo ilisema lengo la mazungumzo hayo ni kukuza na kuimarisha uhusiano wa uwili hususan katika sekta ya viwanda, biashara, kilimo, nishati utalii pamoja na kutafuta fursa mbalimbali za ushirikiano, uwekezaji na miradi ya pamoja.
Ushiriki wa Rais Samia katika Mkutano wa G20 unalenga kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuchangia ipasavyo mijadala muhimu ya kimataifa kuhusu maendeleo duniani na kunadi sera za uchumi za kimataifa zitakazochochea maendeleo na ustawi zaidi nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED