Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, amepongeza hatua ya kutoa mafunzo maalum kwa madaktari kuhusu tathmini za ulemavu kutokana na ajali na magonjwa ya kazi, akisisitiza kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa ustawi wa afya ya wafanyakazi na sekta ya ajira kwa ujumla.
Akizungumza mjini Iringa wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendelea katika ukumbi wa Royal Palm, Serukamba amesema kuwa madaktari wanapaswa kuzingatia mafunzo hayo ili kuboresha uwezo wao wa kutathmini na kutoa huduma bora kwa wafanyakazi walioathirika na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi.
Mafunzo hayo yanawashirikisha madaktari kutoka mikoa ya Iringa, Njombe, Songwe, Rukwa, Mbeya, Katavi, na Ruvuma, na yanafanyika kwa siku tano kuanzia 28 Oktoba hadi 1 Novemba 2024.
Mkuu huyo wa mkoa amepongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa kuandaa mafunzo hayo, akisisitiza kuwa mafanikio ya sekta ya ajira nchini yanategemea afya na ustawi wa wafanyakazi. Ameeleza kuwa kuimarisha uwezo wa madaktari katika kufanya tathmini sahihi za ajali na magonjwa yatokanayo na kazi ni hatua muhimu katika kulinda na kuimarisha nguvu kazi ya Taifa.
"WCF inatekeleza majukumu muhimu kwa kuhakikisha wafanyakazi waliopata ajali au magonjwa kazini wanapata fidia stahiki. Mfuko huu hutoa mafao saba makuu, yakiwemo malipo ya matibabu, fidia ya ulemavu wa muda na wa kudumu, huduma za utengemao, na fidia kwa wategemezi wa mfanyakazi aliyefariki," amesema Serukamba.
Ameongeza kuwa hadi sasa WCF imetoa mafunzo kwa madaktari 1,606 katika awamu za awali, huku wengine 133 wakipatiwa mafunzo ya vitendo ili kuhakikisha wanufaika wa fidia wanapata huduma za afya za viwango na tathmini sahihi.
Serukamba pia amekumbusha madaktari kuwa ushiriki wao katika mafunzo hayo ni muhimu kwa kuhuisha leseni zao za kitaaluma kupitia alama za Maendeleo Endelevu ya Taaluma (CPD Points). “Utendaji bora wa madaktari utasaidia wafanyakazi kurudi kazini mapema na kuongeza tija na uzalishaji kwa Taifa,” amesema.
Akizungumzia mipango ya mafunzo hayo, Mkurugenzi wa WCF, Dk. John Mduma, amesema kuwa WCF ni taasisi ya hifadhi ya jamii chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, iliyoanzishwa Julai 2015 kwa lengo la kusimamia na kutekeleza Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura ya 263.
Kwa mujibu wa Mduma, mafao yanayotolewa na WCF ni pamoja na malipo ya matibabu, fidia ya ulemavu wa muda na wa kudumu, malipo ya huduma za utengemao, na msaada wa mazishi kwa wafanyakazi waliofariki kutokana na kazi. "WCF imekuwa ikitoa mafao haya kikamilifu kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki yao stahiki," amesema Mduma.
Serukamba amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa madaktari kufuatilia kwa makini mafunzo hayo na kutumia maarifa waliyopata kuboresha huduma kwa wafanyakazi waliopata majeraha au magonjwa kazini.
"Ni muhimu kuhakikisha wafanyakazi wanapata huduma stahiki na fidia kwa wakati. Mafanikio ya sekta ya ajira yanategemea ustawi wa afya ya wafanyakazi wetu," amehimiza.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED