RAIS Dk. .Samia Suluhu Hassan na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, jana aliwawatunuku kamisheni kwa maofisa wanafunzi 236 wa cheo cha Luteni Usu, kutoka kundi la 5/2021 la Shahada ya Sayansi ya Kijeshi (BMS) na kundi la 71/23 (Regular) katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA).
Kabla ya kutunuku kamisheni hizo, Rais Samia alikagua gwaride lililoandaliwa na maofisa wanafunzi hao ambao kati yao wanaume ni 196 na wanawake 40.
Katika maofisa hao waliotunukiwa cheo cha Luteni Usu kutoka kundi la 5/2021 BMS ambao jumla yao ni 75 na wamepata mafunzo chuoni hapo kwa miaka mitatu na kuhitimu shahada ya sayansi ya kijeshi.
Vilevile, katika kundi la 71/23 – Regular, maofisa wapya 95 wamepata mafunzo yao kwa muda wa mwaka mmoja na maofisa 88 wamepata mafunzo ya kijeshi kutoka nchi rafiki za Afrika na nje ya bara la Afrika.
Pia alitunuku shahada ya kwanza ya sayansi ya kijeshi kwa maofisa wapya 75 ambao kati yao wanaume 53 na wanawake 22.
Baada ya kutunuku kamisheni hizo, Rais alitoa zawadi kwa maofisa waliofanya vizuri katika fani mbalimbali. Katika kundi la 05/21 BMS, aliyefanya vizuri katika fani zote kwa ujumla ni Luteni Usu Cloud Ndaiga.
Kadhalika, aliyefanya vizuri katika taaluma ni Luteni Usu Xavery Malobana na aliyefanya vizuri katika Medani ni Luteni Usu Kelvin Adrian, huku aliyefanya vizuri kutoka nchi rafiki ni Luteni Usu Thabi Masuku kutoka Eswatini.
Kwa kundi la 71/23-Regular, aliyefanya vizuri katika fani zote ni Luteni Usu John Bahati na katika taaluma Luteni Usu Charles Charles. Katika medani, aliyefanya vizuri ni Luteni Usu Apha Gustav.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk.Stergomana Tax, alisema mafunzo ya shahada ya sayansi ya kijeshi ni muhimu kwa jeshi lakini pia kwa taifa.
"Umuhimu wa mafunzo haya unajidhihirisha kwenye umahiri wa jeshi letu katika kutimiza majukumu yake kwa ufanisi. Mafunzo haya huwajengea uwezo kwa kutekeleza operesheni za kijeshi kwa ustadi mkubwa na kuwaandaa kuwa viongozi wenye maadili, nidhamu na weledi wa kuongoza vikosi vya jeshi,” alisema.
Waziri Tax alisema kitaifa mafunzo hayo huhakikisha jeshi linapata viongozi wazalendo na wenye uwezo wa kulinda mipaka ya nchi na kukabiliana na vitisho vya ndani na nje ya nchi.
“Kwa ujumla, mafunzo haya yanajenga jeshi imara na taifa lenye uwezo wa kudumisha amani, usalama na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema.
Mkuu wa TMA, Meja Jenerali Jackson Mwaseba, aliwakumbusha wahitimu kutambua kuwa jeshi na taifa limewekeza fedha na rasilimali nyingi kwao ili kuhakikisha wanapata elimu bora kwa ajili ya manufaa yao binafsi, jeshi na taifa kwa ujumla.
"Taifa linahitaji wasomi walio na uzalendo, nidhamu, maadili mema ambao wataingia kuijenga nchi yetu kwa misingi endelevu, hivyo wahitimu mna dhamana kubwa ya kutumia taaluma zenu katika kutimiza wajibu wenu kutekeleza kwa vitendo," alisema Jenerali Mwaseba.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED