CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Chama kujadili kilichojiri katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika juzi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, kauli ya chama kuhusu uchaguzi huo itatolewa baada ya kikao hicho.
"Kamati Kuu ya Chama itakutana kwa kikao cha dharura kesho (leo). Kikao hicho kitajadili ajenda maalumu ya yaliyojiri kwenye kinachoitwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji 2024 na hatimaye kutoka na msimamo wa chama. Kauli ya chama itatolewa baada ya kikao hicho kumalizika," alisema Mrema.
Alisema kikao hicho kitaongozwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe.
Kikao hicho kimeitishwa wakati CHADEMA ikiwa miongoni mwa vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo, ikiwa na malalamiko ya kuwapo kasoro kwenye uchaguzi huo.
Miongoni mwa madai ya chama hicho ni wagombea na mawakala wao kukamatwa vituoni na katika maeneo mengine kuchelewa kuanza kupiga kura kwa madai ya kuchelewa kufikishwa kwa karatasi za kura au kuchanganya vitabu vyenye orodha ya wapiga kura, vingine kupelekwa kituo A au B.
Madai mengine ya chama hicho ni kukamatwa karatasi ambazo tayari zilibainika kuwa zina kura zilizopigwa kabla ya kuanza kwa zoezi la upigaji kura.
Wakati huo, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, amezitaka mamlaka kuwaachia bila masharti viongozi na makada wa chama hicho wanaoshikiliwa katika maeneo mbalimbali nchini.
ACHOMWA KISU
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ikana, wilayani Momba, Amos Sikamanga (41), amelazwa katika Kituo cha Afya Tunduma, akidaiwa kujeruhiwa kwa kuchomwa kisu cha utosi na wanaodaiwa viongozi wa CHADEMA.
Tukio hilo lilitokea juzi saa tatu asubuhi katika eneo la kituo cha kupigia kura cha Nakawale, kijijini Nakawale.
Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Momba, Chuki Sichalwe, alidai mwenyekiti wao huyo alijeruhiwa kwa kuchomwa na kisu kichwani sehemu ya utosi alipofika katika kituo hicho cha kupigia kura cha Nakawale kwa lengo la kukagua mawakala wa chama hicho wakati zoezi la kupiga kura linaendelea.
"Viongozi hao wa CHADEMA walikuwa wanamzuia mwenyekiti wetu kuingia katika chumba cha mawakala wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ofisi hizo, hivyo kuzuka vurugu zilizosababisha kuchomwa kisu," alidai Sichalwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba tayari jeshi hilo linawashikilia viongozi wawili wa CHADEMA kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.
Kamanda Senga aliwataja viongozi hao wa CHADEMA wanaoshikiliwa ni Gidion Siame (34) ambaye ni Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Momba na Fiston Haonga (57) ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee (BAZECHA) Jimbo la Momba, wote wakazi wa kijiji cha Nakawale, wilayani humo.
Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo, Kamanda Senga alisema uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha tukio hilo ni mihemuko ya kisiasa.
Alidai kuwa watuhumiwa walikuwa wanamzuia mwathirika kuingia katika chumba cha mawakala wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ofisi ya kijiji cha Nakawale.
"Mwathirika yuko Kituo cha Afya Tunduma anaendelea na matibabu na uchunguzi wa tukio hili unaendelea na pindi utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani," alisema Kamanda Senga.
*Imeandaliwa na Elizabeth Zaya (DAR) na Moses Ng'wat (SONGWE)
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED